Mamilioni yakusanywa ibada ya kumuaga Mafuru

Dar es Salaam. Ule msemo wa kufa kufaana ni kama umetokea kwenye Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA) Magomeni baada kukusanya zaidi ya ni Sh134 milioni na dola 6,000 wakati wa ibada ya faraja ya kanisa kwenye tukio la kuaga mwili wa Lawrence Mafuru.

Mafuru, aliyekuwa katibu mtendaji wa Tume ya Mipango alifariki dunia Novemba 9, 2024 nchini India alipokuwa akipatiwa matibabu, leo ameagwa kanisani hapo kabla ya kuzikwa kwenye makaburi ya Kondo, Tegeta.

Katiba ibada ya faraja kanisani, Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila aliyekuwa miongoni mwa waliotoa salamu za rambirambi alianzisha harambee hiyo.

Katika salamu zake za rambirambi alisema,” kama tuna huruma kwa mtu aliyelala tukayaonyeshe matendo kwa kile kizazi alichokihudumia Mafuru,” alisema na kuahidi mkoa wake kuchangia Sh5 milioni.

Baada ya kauli hiyo, Askofu Mkuu wa Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA), jimbo la Kasikazini mwa Tanzania, Mchungaji Mark Malekana alisimama na kusema, jukumu hilo kwa kuwa halikuwa limepangwa, anampa Chalamila ushemasi ili kulisimamia.

Kwa utaratibu wa makanisa ya Kiadventista, mashemasi wakiongozwa na shemasi mkuu ndio wanasimamia zoezi la sadaka kanisani.

“Ili halikupangwa, lakini Chalamila ameanzisha wazo la akili,  jengo letu (jengo jingine lililopo pembezoni mwa kanisa mama la Magomeni) lipo katika hatua ya kukamilika,  mwezi ujao linafunguliwa, hivyo namteua Chalamila kusimamia hilo kama shemasi,” alisema mchungaji Malekana.

 Alifafanua kwamba nyumba ya ibada siyo ya Wadventist,a ni nyumba ya ibada ya Mungu kwa mataifa yote na yeye kama Mchungaji Malekana anachangia Sh1 milioni.

Aliyefuatia kuchangia ni Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka aliyewaita Daud wa Break Point na watu wengine kadhaa na kuelekeza kuwa umoja wa watu wa Musoma unachangia ujenzi wa kanisa hilo Sh10 milioni.

Kisha Naibu Katibu Mkuu wa CCM, alichangia Sh10 milioni na kiasi kama hicho kilitolewa na Kitila Mkumbo, mbunge wa Ubungo.

Baada ya Kitila, Katibu tawala wa Mkoa wa Dar, Dk Toba alisema wameshauriana na Chalamila hivyo wanaongeza fedha na watatoa Sh15 milioni.

Januari Makamba alisema kiitifaki hapaswi kukizidi chama chake, hivyo yeye na familia yake wamechangia Sh5 milioni

Mkurugenzi mtendaji wa CRDB, Abdulmajid Nsekela amechangia Sh20 milioni, Profesa Adolf Mkenda na mkewe Beatrice ambaye ni Msabato wamechangia Sh5 milioni, Richard Kasesela Sh5milioni na Mfuko wa Pensheni wa NSSF umechangia Sh5 milioni.

Taasisi ya Bankable imechangia Sh10 milioni, Kamati ya maandalizi ya msiba iliyoongozwa na msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu imechangia Sh10, milioni na kisha Chalamila akapanda tena na kutoa dola 5,000 ambazo alizikabidhi kwa mchungaji Malekana naye akazikabidhi kwa mhazini wa kanisa.

Harambee hiyo imeendelea kwa watu mbalimbali kuahidi kutoa Sh3 milioni na Mchungaji Malekana kushauri ili kwenda na muda, huduma ya ibada iendelee na watu wapewe namba ya Lipa wachangie na kuwa wakati wa kuaga mwili wengine wangepita na kuchangia.

Mafuru alikuwa muumini wa kanisa la Magomeni SDA na kwa nyakati tofauti alihudumu kama shemasi na kisha mzee wa kanisa kwa miaka mitatu.

Aidha katika ibada hiyo, Mchungaji Malekana aligusia namna ambavyo mabinti wa Mafuru wamemwelezea baba yao na kutania kwamba kuna familia huwa zinapata wakati mgumu kujadili watakachosema watoto, maana hawana cha kusema.

Alisema wapo ambao wataigiza kwa kusema, “tumekumisi lakini wakitoka pale (kwenye mazishi) wanasema afadhali mgogoro umeondoka, mama naye anasema afadhali ameondoka,” alisema Mchungaji Malekana na kusababisha waombolezaji kuangua kicheko.

Ametoa kisa kimoja na kusema, kilikuwa cha kutatiza cha mgogoro wa mke na mume.

“Yule mke alisema, mchungaji hujui tu, ‘huyu mwanaume ni wa hovyo na hata kufa hataki’, nikasema kwani mlipatana ananza yeye?” alisema na kusababisha tena waombolezaji kuangua kicheko, kisha akasisitiza kitabu cha Mafuru kiendelee kuandikwa ndani ya kila mmoja.

Related Posts