Watoto wa Mafuru waelezea maisha ya wazazi wao

Dar es Salaam. Ni historia iliyoibua hisia za simanzi kwa waombolezaji, wakati watoto wa marehemu Lawrence Mafuru, Lona na Loreen walipokuwa wakimwelezea baba yao kwenye ibada ya mwisho ya kumuaga.

Mwili wa Mafuru utazikwa leo Novemba 15, 2024 kwenye makaburi ya Kondo, Tegeta baada ya ibada hiyo.

Mafuru aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango alifariki dunia Novemba 9, 2024 kwenye Hospitali ya Apollo nchini India alikokuwa akipatiwa matibabu.

Katika ibada ya faraja iliyofanyika katika Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA) Magomeni, mabinti hao wa Mafuru walitumia dakika 15 kumwelezea baba yao.

Wakiwa na nyuso za huzuni huku mama yao, Noela, aliyekuwa ameketi akiwatazama, mabinti hao waliokuwa sambamba na baba yao mdogo, Maira Mafuru walianza kwa kumshukuru Mungu.

Binti mkubwa, Loreen, anayesoma nchini Uingereza, ndiye alianza kumzungumzia baba yake, akisema alikuwa ni zaidi ya baba kwao.

“Hakuna tafsiri ya kumzungumzia, alikuwa ni ‘mentor (mwongozaji), tunashukuru kwa kumpenda mama (Noela), tutazidi kuendeleza legacy (urithi), kwetu alikuwa ni kila kitu,” amesema Loreen kwa huzuni na kuendelea:

“Mimi, Lona na mama tunakumbuka, tutalimisi tabasamu lako, asante kwa kila kitu, kwa heri,” amesema binti huyo mkubwa wa Mafuru.

Naye mdogo wake, Lona, amesema baba yao alikuwa ni sensor (kihisio) katika mwelekeo wao.

“Alikuwa ni mentor, kaka, mume na kila kitu kwa watu, najua baba alimpenda mama sana, upendo wake ulikuwa kwenye pilau, njegere na vitumbua,” amesema binti huyo akielezea aina ya vyakula alivyopenda kula baba yake na kusababisha waombolezaji kuangua kicheko.

Amesema baba yake pia alikuwa ni shabiki wa Yanga na Arsenal.

“Alikuwa akipenda kusema ‘yaani huyu kiazi muone’, alikuwa akisitiza bila kusoma huwezi kuelimika na bila kuelimika huwezi kuwa na nguvu, alifanya kila kitu kwa ajili yetu.”

“Alitupa mifano ya mume kumpenda mkewe, mimi na dada yangu, baba alikuwa rafiki, na alitusapoti, tunamshukuru baba na mama kwa kutuonyesha hilo,” amesema Lona huku akibubujikwa machozi na kubembelezwa na baba yake mdogo, Maira.

Baada ya watoto hao kumzungumzia baba yao, ibada kuu ya faraja ilianza saa 8:20 mchana ikiongozwa na Askofu Mkuu wa Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA), Jimbo la Kasikazini mwa Tanzania, Mchungaji Mark Malekana.

Mchungaji huyo amesema maisha ya Mafuru yamekuwa ya matendo ambayo yameendelea kuwepo hata baada ya kulala usingizi wa mauti.

Related Posts