Dar es Salaam. Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) imewataka wauzaji wakubwa wa kemikali kuacha kuwauzia wauzaji wa kati na wadogo wa bidhaa hizo ambao hawajasajiliwa kufanya biashara hiyo.
Angalizo hilo limetolewa kupitia taarifa ya Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti wa GCLA, Daniel Ndiyo, katika kikao cha wadau wanaojihusisha na uingizaji na usambazaji wa kemikali bashirifu (zinazoweza kuchepushwa na kutumika kihalifu), kilichofanyika jijini Dar es Salaam Novemba 14, 2024.
Kikao hicho kiliandaliwa na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali na kufanyika katika Ofisi za Kanda ya Mashariki.
“Wadau wote wa kemikali lazima wasajiliwe na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa mujibu wa sheria, pamoja na kutimiza maazimio tuliyoweka ili wafanye biashara zao kwa usalama na kulinda afya za binadamu na mazingira,” amesema mkurugenzi huyo.
Kamishna Msaidizi wa Sayansi Jinai kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Ziliwa Machibya alisema kemikali bashirifu ni hatari katika mazingira ya matumizi ya dawa za kulevya, hivyo, amewasihi wadau wa biashara hizo kufuata taratibu za usajili ili kemikali hizo ziweze kutumika katika malengo yaliyokusudiwa.
Kwa upande wake, Geoffrey Jato, mdau wa kemikali hizo, ameipongeza Mamlaka kwa kuwapa elimu na kuendelea kuweka ushirikiano wa karibu na wadau wa kemikali, jambo ambalo limewatatulia changamoto mbalimbali, zikiwemo usajili.
“Elimu tuliyoipata ya usajili wadau wengi hawakuwa nayo, ila kwa sasa kutakuwa na ongezeko la wadau kujisajili na kupata elimu ili wanapofanya manunuzi ya kemikali au uzalishaji waweze kufanya kwa usalama,” amesema Jato.