Washitakiwa waomba wapelekwe Gereza la Keko

Dar es Salaam. Washitakiwa wawili waliofikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashitaka manne ya kusafirisha kilo 19 za dawa za kulevya aina ya bangi, wameomba wapelekwe Gereza la Keko na si lingine.

Washitakiwa hao, Hassan Magoha (42), mkazi wa Somangila na Hussein Hussein (32), mkazi wa Mbondole wametoa ombi hilo leo Novemba 15, 2024 muda mfupi baada ya kusomewa mashitaka na Wakili wa Serikali, Frank Rimoy, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Gwantwa Mwankuga.

Japokuwa gerezani si sehemu nzuri, lakini washitakiwa wameiomba mahakama iwapo watakosa dhamana, wapelekwe Gereza la Keko.

Baaba ya upande wa Jamhuri kuwasomea mashitaka, Hussein alinyoosha mkono kuomba nafasi ya kuzungumza, aliporuhusiwa na hakimu kuzungumza aliomba wapewe dhamana na iwapo itashindikana wapelekwe Gereza la Keko.

Mshitakiwa Hussein: Mheshimiwa hakimu, haya mashitaka tuliyosomewa hakuna sehemu iliyoonyesha jumla ya kilo za dawa za kulevya.

Hakimu: Unataka upate jumla ya idadi ya kilo hizo?

Hakimu: Mmh! lakini umesikiliza vizuri wakati mnasomewa mashtaka?

Hakimu: Zikijumlishwa unaweza kupata dhamana?

Hussein: Mheshimiwa hakimu, ombi letu lingine tunaomba kama tukikosa dhamana, tupelekwe Gereza la Keko.

Hakimu: Kwa nini Gereza la Keko na si gereza lingine?

Hussein: Mheshimiwa hakimu, kule Gereza la Keko kuna vitu vyetu.

Hussein: Kuna shuka zetu ambazo tunazitumia kujifunika.

Baada ya jibu hilo, watu waliokuwepo mahakamani waliangua kicheko.

Hakimu: Mbona sasa unasema kama mtashindwa kupata dhamana, wakati mimi bado sijatoa masharti ya dhamana.

Magoha aliporuhusiwa kuzungumza aliomba wapelekwe Keko akidai wana shuka zao huko.

Rimoy awali alidai washitakiwa wanakabiliwa na kesi ya jinai namba 32478 ya mwaka 2024 wakidaiwa kusafirisha bangi.

Magoha anadaiwa katika shitaka la kwanza kuwa Oktoba 19, 2023 eneo Mwanzo Mgumu, Kigamboni alisafirisha kilo 1.89 ya dawa za kulevya aina ya bangi.

Katika shitaka la pili, wote wanadaiwa Oktoba 20, 2023, katika Kata ya Msongola eneo la Mbondole, wasafirisha gramu 542.60 za bangi.

Katika shitaka la tatu, wanadaiwa kusafirisha kilo 11.93 za bangi kosa walilotenda Oktoba 20, 2023 eneo la Mbondole.

Wanadaiwa katika shitaka la nne, siku na eneo hilo, walisafirisha kilo 4.95 za bangi wakijua kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.

Baada ya kusomewa mashtaka walikana kuyatenda. Upande wa Jamhuri ulidai upelelezi umekamilika ukaomba terehe nyingine kwa ajili ya kuwasomewa hoja za awali (PH).

Kuhusu dhamana, ulidai mashitaka yanayowakabili yanadhaminika, hivyo uliomba Mahakama itoe masharti kwa mujibu wa sheria.

Hakimu Mwankuga alitaja masharti ya dhamana kwamba, kila mshitakiwa awe na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya Sh5 milioni kila mmoja.

Wadhamini hao pia wanatakiwa wawe na barua za utambulisho kutoka katika taasisi wanazofanyia kazi au barua ya Serikali za Mitaa.

Washitakiwa wameshindwa kutumiza masharti ya dhamana hivyo wamepelekwa rumande hadi Novemba 29, 2024 kwa ajili ya kusomewa hoja za awali.

Related Posts