Dar es Salaam. Ufafanuzi uliotolewa na Chadema ikikanusha kuwa na mpango wa kugawana madaraka maarufu ‘Nusu mkate’ umewaibua wadau wakionyesha hofu ya chama hicho kutumbukia kwenye mgogoro wa kiuongozi.
Mbali na hoja ya kugawana madaraka, ufafanuzi huo uliotolewa jana Novemba 14, 2024, pia umekanusha chama hicho kujihusisha na rushwa, kikisema madai hayo hayana ushahidi.
Licha ya ufafanuzi uliotolewa na Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje, John Mrema kutotaja waliotoa hoja hizo, inafahamika kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), Tundu Lissu alitoa kauli hizo alipozungumza na waandishi wa habari Novemba 12, 2024 mjini Singida alipoeleza mwenendo wa uchaguzi wa serikali za mitaa nchini.
“Tumedanganywa tukadanganyika, tumeletewa lugha laini ya uongo ya maridhiano. Tukaingiziwa vijineno vinavyosema hivi, msiwe wakali sana mtapewa Serikali ya nusu mkate,” alisema Lissu.
Mrema katika tamko hilo amesisitiza kuwa Chadema haijaacha kufanya mambo yake ya msingi ikiwamo kupigania mabadiliko ya Katiba na kutafuta mfumo bora wa uchaguzi.
Hata hivyo, akitoa maoni kupitia mtadao wa kijamii wa X (zamani twitter) kuhusu ufafanuzi wa Chadema uliowekwa kwenye mtandao huo, kada wa chama hicho aliyegombea ubunge wa Mbarali mwaka 2020, Liberatus Mwang’ombe ameandika:
“Hii ni taarifa ya chama changu ambayo imekuwa na comments nyingi sana negative (hasi). This explains something very serious (hii inamaanisha kuna jambo zito sana).”
Hata hivyo, kada mwingine wa chama hicho, Martin Maranja ameandika: “Ufafanuzi mzuri kwa wakati sahihi. Ahsante sana viongozi wa chama chetu, tusonge mbele.
“Focus, focus, focus (lenga). Adui yetu ni CCM. Kwa sasa tunalo jukumu moja kubwa mbele yetu, uchaguzi wa serikali za mitaa. Tumejiandaa kushiriki uchaguzi huu kwa nguvu zetu zote.”
Hii si mara ya kwanza kwa Chadema kufafanua kauli za Lissu ambaye mara kadhaa amekaririwa akidai kuwepo kwa fedha za rushwa ndani ya chama hicho, kauli zilizozua ukinzani miongoni mwa makada.
Hatua hiyo inatajwa kuwa dalili ya misuguano ndani ya chama hicho inayoweza kuleta mgogoro.
Mchambuzi wa masuala ya siasa, Bubelwa Kaiza amesema chama hicho kinapaswa kutumia njia tofauti kutanzua migogoro.
“Chama kinatakiwa kupata msaada wa kitaalamu kusaidiwa kuacha fikra za kitaasisi na kisisasa zinazowaongoza kwa sasa.
“Lissu asingejitokeza kusema anayoyasema nje ya chama, iwapo ndani kungekuwa na uhakika tatizo la rushwa kutatuliwa kupitia mfumo fanisi ndani ya chama,” amesema.
Bubelwa amesema tatizo linalokikabili chama hicho ni kuendesha chama kwa kufuata mfumo wa kidola unaotumiwa na CCM.
“Chama-dola hutumia vyombo vya usalama kusambaratisha migogoro ndani ya chama. Chadema hakiongozi dola. Hakina namna ya kutatua migogoro yake kwa kutumia mtazamo wa CCM. Hili ni kosa la kimuundo,” amesema.
Kwa mujibu wa Bubelwa kama Chadema haitaweka mfumo imara wa utatuzi wa migogoro yake ya ndani, huenda ikatumbukia kwenye mgogoro.
“Kuwepo kwa migogoro kwenye vyama vya siasa au taasisi nyingine ni jambo la kawaida, lakini kinachotakiwa kuzingatiwa ni kuwepo kwa utaratibu wa kimfumo wa kudhibiti, kuratibu na kutanzua migogoro pindi inapojitokeza,” amesema.
Lissu adai kuhujumiwa Same
Mvutano huo wa hoja unakuja wakati Novemba 9, 2024 Lissu alilalamika kuzuiwa kushiriki kwenye mkutano ulioandaliwa na Chadema wilayani Same Mkoa wa Kilimanjaro, akidai kuwepo kwa njama za viongozi wa chama hicho (hakuwataja) walioshiriki kuzuia mkutano huo.
“Kama kuna mtu anayejiita kiongozi wa chama au mwanachama anayeenda kushirikiana na watu wa Serikali kuzuia mkutano wa chama chake, mjiulize, huyo ni wa kwetu kiasi gani?”
Mbali ya hayo, zimetokea vurugu jijini Arusha katika uchaguzi wa viongozi wa Chadema mkoa huo, baada ya baadhi ya wanachama kudai kuwa uchaguzi huo uligubikwa na rushwa.
Wakizungumzia uchaguzi huo jana Alhamisi Novemba 14, 2024, baadhi ya wanachama hao walidai kufukuzwa wakieleza hawatakubali kuchaguliwa viongozi wasiowataka.
Akijibu malalamiko hao, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema aliwataka wanachama kuzingatia nidhamu na kuheshimu misingi ya chama.
Akizungumza Novemba 13 baada ya kumalizika kwa uchaguzi uliompa ushindi Elisa Mungure kuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Mkoa wa Arusha, Lema alitoa onyo kali kwa wanachama waliotaka kuvuruga uchaguzi huo.
“Tukishindwa kudhibiti nidhamu, hiki chama kitapotea,” alisema.
Vurugu hizo zilitokea, ikiwa imepita miezi sita tangu uchaguzi wa kumpata mwenyekiti wa Mkoa wa Njombe uliowakutanisha Rose Mayemba na Ahadi Tweve ulipovunjika Mei 24, 2024.
Uchaguzi huo uliokuwa umerudiwa, ulivunjika baada ya baadhi ya wanchama kudai kuwa baadhi ya wajumbe kutoka wilayani Makete, hawakupaswa kushiriki kwa kuwa hawakuwa wajumbe halali. Uchaguzi huo haujarejewa mpaka sasa.
Chadema iko hatarini kutumbukia kwenye mizozo iliyoviangusha vilivyokuwa vyama vikubwa vya upinzani nchini, ikiwemo NCCR-Mageuzi ambayo katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1995 kilileta joto la kisiasa baada ya kumsimamisha aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, hayati Augustine Mrema.
Katika uchaguzi mkuu wa 1995, Mrema alishika nafasi ya pili nyuma ya hayati Benjamin Mkapa wa CCM.
Hata hivyo, chama hicho kiliingia kwenye migogoro kati ya Mwenyekiti Mrema na katibu wake Mabere Marando na hadi kufikia mwaka 1999, chama hicho kiligawanyika baada ya Mrema kuhamia TLP.
Chama cha Wananchi (CUF), nacho kiliingia kwenye migogoro mara kadhaa, mwaka 2012 Baraza Kuu la chama hicho kwa wingi wa kura lilimfukuza mmoja wa waasisi wa chama hicho, Hamad Rashid Mohammed na wenzake watatu.
Baada ya kufukuzwa, Hamad Rashid na wenzake walianzisha chama cha ADC alichopo kipo hadi sasa.
Kama hiyo haitoshi, CUF kiliingia kwenye mgogoro mwingine mwaka 2019 baada ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, hayati Maalim Seif Sharif Hamad na wenzake kujitoa kwenye chama hicho kwa kushindwa kuelewana na Mwenyekiti, Profesa Ibrahim Lipumba.
Baada ya kujitoa, Maalim Seif na wenzake walihamia chama cha ACT-Wazalendo.
Akijadili suala hilo, Makamu Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, Joseph Selasini amesema ndani ya vyama vya siasa kuna baadhi ya viongozi wanaojali masilahi binafsi badala ya malengo ya taasisi.
“Viongozi wengi huweka masilahi yao binafsi mbele kuliko yale ya wanachama na chama. Hapo hutokea ujenzi wa makundi ili kulinda masilahi hayo. Inaweza kuwa uongozi wa ndani ya chama au nje ya chama katika nafasi za kuchaguliwa,” amesema.
Selasini aliyeshuhudia mgogoro wa NCCR-Mageuzi kabla ya kuhamia Chadema, ambako pia aliondoka akizozana na uongozi, amesema baadhi ya viongozi hutoa ahadi nyingi kwa wanachama na zisipotekelezwa huleta uasi ndani ya chama.
“Uwazi katika matumizi unapokosekana na kuruhusu ufisadi na rushwa, baadhi ya viongozi na wanachama lazima watahoji hasa wakishindwa kupata maelezo katika vikao rasmi.
“Lugha za uchochezi ambazo hazina staha kwa viongozi wengine ili kuamsha hisia za wengine, ni sehemu ya kichocheo cha vurugu na mifarakano,” amesema.
Amesema baadhi ya viongozi hutumia umasikini wa wanachama kwa faida yao, ili kuwafanya wadumu madarakani.
“Tabia ya kukaa madarakani muda mrefu inawafanya viongozi kukosa mvuto na kuongoza kwa makundi. Hali inayosababisha upendeleo katika maamuzi.
“Pia ubaguzi kwa wanachama na viongozi na ukosefu wa elimu ya siasa ya kutosha kwa wanachama, kunawafanya washindwe kuifahamu vyema katiba ya chama chao,” amesema.
Ametaja pia propaganda za nje ya vyama hasa kutoka katika vyama mahasimu, kuwa ni sababu nyingine.
Kama una maoni kuhusu habari hii tuandikie kupitia Whatsapp 0765864917.