Zoezi la kufikisha misaada katika Ukanda wa Gaza linaendelea kuwa gumu huku usafirishaji wa misaada hiyo hadi katika eneo la kaskazini lililozingirwa ukiwa hauwezekani, hayo ni kwa mujibu wa afisa wa maswala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken na Waziri wa Ulinzi Lloyd Austin katika barua yao ya Oktoba 13 kwa Israel walimpa mshirika wao huyo orodha ya hatua mahususi ambazo Israel ilihitaji kuzifanya ndani ya siku 30 ili kukabiliana na hali inayozidi kuwa mbaya katika Ukanda wa Gaza. Hatua hiyo ni muhimu ili Israel iepuke vikwazo vya msaada wa kijeshi kutoka Marekani.
Na Israel yenyewe kwa upande wake imesema inajitahidi sana kusaidia kufikishwa misaada ya kibinadamu na mahitaji mengine huko Gaza.
Soma Pia: Israel yatakiwa kutekeleza hatua za kusitisha mapigano Gaza
Hata hivyo msemaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu, Jens Laerke alipoulizwa swali kwenye mkutano na waandishi wa Habari mjini Geneva iwapo upatikanaji wa misaada ya ulikuwa umeboreshwa alijibu.
”Kwa mtazamo wetu zoezi la upatikanaji wa misaada liko katika kiwango cha chini sana. Machafuko, mateso, kukata tamaa, vifo, uharibifu na watu wanapoteza makazi yao kwa kiwango cha juu ni mambo yanayotia wasiwasi mkubwa na hasa hali ilivyo katika eneo la kaskazini mwa Gaza, ambalo sasa limezingirwa. hali huko inakaribia sana kuwa haitawezekana kufikisha msaada huko.”
Laerke ameelezea wasiwasi kuhusu eneo la kaskazini mwa Gaza ambako wakaazi na familia zao wameamriwa kuondoka na kwenda katika eno la kusini huku mashambulizi ya majeshi ya Israel kwa mwezi mmoja mfululizo yakiendelea. Israel imesema operesheni yake huko inalenga kuwazuia wapiganaji wa Hamas kujipanga upya.
Hamas yasema iko tayari kusimamisha vita
Huku hayo yakiendelea Afisa mkuu wa Hamas ambaye ni mjumbe wa ofisi ya kisiasa ya Hamas, Bassem Naim, amesema kundi hilo “liko tayari kwa usitishaji vita” katika Ukanda wa Gaza na amemtaka Rais mteule wa Marekani Donald Trump, kuishinikiza Israel kukomesha vita.
Naim ameliambia shirika la Habari la AFP kwamba Hamas iko tayari kufikia makubaliano ya kusitisha vita ikiwa pendekezo la kusitisha mapigano litawasilishwa na kwa sharti kwamba litaheshimiwa na Israel.
Amesema Hamas imewafahamisha wapatanishi kwamba inaunga mkono pendekezo lolote litakalowasilishwa kwao ambalo litawezesha vita kusimama na Israel kuwaondoa wanajeshi wake kutoka Ukanda wa Gaza, kuwaruhusu watu waliokimbia vita kurudi kwenye makazi yao, kuachiwa mateka wa Israel na pia wafungwa wa Kipalestina.
Soma Pia: Israel yalaumiwa kwa mauaji ya halaiki
Naim ameongeza kusema makubaliano hayo pia yajumuishe misaada ya kibinadamu na kuanza mara moja kuujenga upya Ukanda wa Gaza.
Vyanzo: RTRE/AFP