Iringa. Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi ameungana na mamia ya waombolezaji katika mazishi ya aliyekuwa Katibu wa CCM Wilaya ya Kilolo, Christina Kibiki (56).
Mazishi hayo yamefanyika leo Novemba 15, 2024 katika Kijiji cha Ugwachanya, Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa na kuhudhuriwa na makada wa chama hicho pamoja na viongozi wa chama na Serikali, ndugu, jamaa na marafiki wa kiongozi huyo wa CCM.
Ibada maalumu ya kumwombea marehemu ilifanyika katika Kanisa Katoliki la Moyo Mtakatifu wa Yesu, Parokia ya Tosamaganga.
Christina anadaiwa kuuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia Jumatano Novemba 13, 2024.
Taarifa za awali zilieleza kuwa tukio hilo lilitokea Kijiji cha Njiapanda ya Tosa, Wilaya ya Iringa alipokuwa akiishi. Baada ya kushambuliwa, alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Tosamaganga ambako alifariki dunia.
Katibu wa CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla, alisema marehemu alikuwa anajiandaa kuhudhuria semina elekezi kwa makatibu mjini Dodoma jana Alhamisi, Novemba 14, 2024.
Akizungumza wakati akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya CCM, Dk Nchimbi ameeleza kuhuzunishwa na kifo cha kiongozi huyo aliyeacha alama muhimu katika uongozi wa chama wilayani humo.
“Chama cha Mapinduzi kimepoteza kiongozi mwaminifu na mwenye mchango mkubwa kwa maendeleo ya chama na jamii ya Kilolo. Tunatoa pole kwa familia, wanachama wa CCM na wakazi wa Kilolo kwa msiba huu mkubwa,” amesema Dk Nchimbi.
Wito wa kusamehe na kupendana
Katika hotuba yake, Dk Nchimbi amesisitiza umuhimu wa mshikamano, akiwataka Watanzania kujifunza kusamehe na kuonyesha upendo.
“Siyo Utanzania kumuona mwenzako akipita kwenye matatizo na wewe ukapita mbali. Kujilinda na kumlinda mwenzako ni dhamana ya kila mmoja wetu, kwa mujibu wa mafundisho ya kiroho na utu,” ameongeza.
Mauaji ya Christina yameibua masikitiko na hasira kwa jamii na wanasiasa. Mwenyekiti wa Chadema Jimbo la Iringa Mjini, Frank Nyalusi, alisema: “Tunaomba jamii, viongozi wa dini, wanasiasa na Serikali tukemee vitendo hivi vya kihalifu ili taifa lipone.”
Mbunge wa Iringa Mjini, Jesca Msambatavangu amewataka wananchi kujifunza kusamehe na kuepuka matumizi ya nguvu kutatua migogoro.
“Binadamu hukosea. Njia sahihi ya kutatua changamoto zetu ni kwa amani, si kwa kupigana au kuuana,” alisema Msambatavangu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Peter Serukamba amewahakikishia waombolezaji kwamba Serikali ipo kazini katika kuhakikisha wahusika wote wa mauaji ya Christina, wanakamatwa.
“Tunafanya uchunguzi wa kina kwa kushirikiana na vyombo vya usalama kutoka mikoa jirani. Lengo letu ni kuwafikisha wahusika kwenye mkono wa sheria,” amesema Serukamba.
Serukamba amesisitiza umuhimu wa kupendana na kuimarisha mshikamano ili kudumisha amani nchini.
Mazishi ya Christina yameacha alama kubwa huku jamii ikitafakari namna ya kujenga upendo na mshikamano kama sehemu ya kumuenzi.