Dar es Salaam. Licha mifuko ya uwekezaji kuwa na faida nyingi, kumekuwepo na mwitikio mdogo wa wananchi kujiunga nayo huku elimu ndogo ikitajwa kuwa sababu.
Hayo yamebainishwa leo Ijumaa Novemba 15, 2024 na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Kampuni ya Uwekezaji ya UTT Amis, Faustine Kamuzora katika mkutano mkuu wa wawekezaji wa mifuko hiyo.
Kamuzora amesema wakati Watanzania wakiwa zaidi ya milioni 60, waliowekeza kwenye mifuko hiyo hawazidi milioni moja, hivyo elimu zaidi inahitajika ili wajue umuhimu wake.
“Wananchi katika hili wanapaswa kujua kwamba usipokuwa na uwezo wa kutengeneza fedha wakati umelala, ni hatari kwako na badala yake ni lazima kila siku ukimbizane na biashara na kila senti unayoipata na wakati mwingine mambo yanaweza yasiwe mazuri kwako katika kukimbizana huko.
“Hivyo, unavyowekeza fedha kwenye mifuko kama hiyo, mtaji wako unaendeshwa na wataalamu ambao wanajua vile soko linavyoenda na kukuzalishia faida kila uchwao,” amesema mwenyekiti huyo.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa UTT Amis, Simon Migangala amesema taasisi hiyo ina jumla ya mifuko sita – Ukwasi, Hatifungani, Umoja, Watoto, Kujikimu na Wekeza maisha.
Migangala amesema kutokana na mazingira mazuri ya uwekezaji, uhimilivu wa soko na matumizi ya mifumo ya teknolojia, mifuko yote hiyo ndani ya mwaka mmoja tangu 2023, mitaji yake imeongezeka kutoka Sh1.2 trilioni hadi kufika Sh2.2 trilioni.
“Kwa upande wa faida ya mifuko yote, pia imefanya vizuri kwani hakuna mfuko uliokuwa chini ya utendaji wa asilimia 12 na yote kwa pamoja imezalisha si chini ya Sh250 bilioni.
“Tunaendelea kuwakaribisha wawekezaji kuendelea kuwekeza katika mifuko hiyo kwani ni sehemu nzuri ya kukuzia mitaji kwa watu ambao wanapenda kuweka akiba kwa ajili ya maisha yao ya baadaye,” amesema mkurugenzi huyo.
Hata hivyo, Migangala amesema wakati mwingine mifuko hii inaweza kutumika katika kukuza mitaji kwa malengo ya baadaye, mfano kama kwa miaka miwili ijayo unataka kujenga nyumba, kwa kutumia mifuko hiyo, unaweza kutimiliza malengo yako hayo.
Katika mkutano huo wa siku tatu, pamoja na mambo mengine, Migangala amesema watakuwa na mada fupifupi kwa washiriki wa mkutano huo ambazo zitawaongezea ujuzi kuhusiana na mambo ya uwekezaji.
Mmoja wa wawekezaji, Adelina Gabrieli, mshiriki na mkazi wa Sinza, amesema alianza kuwekeza kwenye mfuko huo miaka 20 iliyopita baada ya kustaafu kazi na faida anayoipata huwa ikimsadia kufanya shughuli zake ndogondogo za biashara.
Lilian Simuda, mkazi wa Mbezi, amesema anachokiona bado wananchi hawajawa na imani na mifuko hiyo na kuona kuweka hela ni kama unaenda kubahatisha katika kupata faida.
Lilian ameshauri watendaji waendelee kutoa elimu ikiwemo kwa wananchi wa kawaida na kuwaondolea wasiwasi katika utendaji kazi wake.