Dar es Salaam. Viongozi wa dini nchini kwa nyakati tofauti wametoa kauli kuhusu mwenendo wa mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji, wakiitaka Tamisemi kutenda haki katika hatua zilizobaki za kampeni hadi matokeo kutangazwa.
Wamezungumzia changamoto zilizojitokeza kuanzia uandikishaji wapigakura hadi uteuzi, huku wagombea wa upinzani wakienguliwa kwa sababu mbalimbali, yakiwemo makosa madogo-madogo ya kukosea majina, herufi, anuani au kutokuwa na udhamini wa chama ngazi ya chini.
Viongozi waliozungumzia uchaguzi huo ni Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), na Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania.
Kutokana na kuwapo malalamiko mengi kuhusu wagombea kuenguliwa, Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi, Mohamed Mchengerwa aliongeza muda wa uwasilishaji wa rufaa hadi leo Ijumaa Novemba 15, saa 12.00 jioni badala ya Novemba 13, akizitaka kamati za wilaya kuitisha fomu za wagombea wote
Rais wa TEC, Askofu Wolfgang Pisa akitoa tamko la baraza hilo leo Novemba 15, 2024 ametaka mchakato wa uchaguzi huo wa Novemba 27, ufanyike kwa misingi ya uwazi, uhuru na haki, bila upendeleo.
TEC imesisitiza uchaguzi uhakikishe unaheshimu ukuu wa mamlaka ya wananchi kuhusu viongozi wao wanaopatikana kwa njia za kura.
Baraza hilo linataka Tamisemi kutambua kwamba, ina jukumu kubwa la kuhakikisha mchakato wote wa upigaji kura unafuata misingi ya demokrasia na wale walioshinda kihalali wanapaswa kutangazwa.
“Tunasisitiza wasimamizi wa uchaguzi wasimamie kwa haki bila kupendelea chama chochote, ukiukwaji wa matakwa ya wananchi unasababisha kuwepo kwa viongozi wasio chaguo la watu.
“Kiongozi anayepatikana kwa mabavu, kwa uongo au kutangazwa bila kupata kura nyingi husababisha kutoaminika na kukiukwa kwa misingi ya demokrasia. Ukitumia nguvu na ulaghai katika kupata kiongozi, basi kiongozi huyo, lazima atumie nguvu na ulaghai kuwaongoza watu katika kipindi chake chote cha uongozi,” amesema na kuongeza:
“Huyo sasa siyo kiongozi na hastahili kuwa kiongozi, na huko ni kulikosea heshima Taifa na wale wanaohusishwa na uchaguzi; sasa kuna sababu gani kusema tunafanya uchaguzi, halafu tunatumia nguvu na ulaghai?”
TEC imesema isingependa kuona nchi ikitumbukia kwenye vurugu zinazosababishwa na uchaguzi mbovu.
Ili kuondokana na hali hiyo, baraza limesema njia ya uhakika ni kupata viongozi watakaoendesha uchaguzi wa serikali za mitaa kwa njia ya haki, uhuru na uwazi, utu, demokarsia na upendo.
Amesema serikali za mitaa ndilo eneo ambalo raia hushiriki kuchangia na kupanga maendeleo ya nchi, kuanzia ngazi ya mtaa hadi Taifa.
“Raia hudai kutekelezewa haki zake na Serikali katika ngazi zote, pia raia hupata fursa ya kutathimini utendaji na uwajibikaji na uwazi wa Serikali katika ngazi ya mtaa hadi Taifa,” amesema.
Amesema serikali za mitaa ni chombo muhimu na lengo lake ni kupeleka madaraka kwa wananchi, na maendeleo ya kweli ya watu yanayoletwa na watu, lakini hilo litawezekana kama kutakuwa na viongozi wazuri waliochaguliwa kwa haki.
“Madhara ya kutokuwa na uchaguzi huru ni makubwa, watu wengi wamekuwa wakilalamika kuhusu mchakato wa uchaguzi huu, wakikumbuka yale yaliyojitokeza katika uchaguzi miaka iliyopita. Wananchi wameshuhudia namna mchakato wa uandikishaji ulivyoendeshwa kumekuwa na upendeleo wa wazi uliofanywa na watendaji kwa kuwaengua wagombea wa vyama vya upinzani.
“Jambo hilo limetoa doa kubwa kwa Taifa letu, hata pale kiongozi mwenye dhamana alipojitahidi kutoa muda zaidi wa kukata rufaa bado haijaondoa doa hilo katika uchaguzi wa mwaka huu,” amesema.
Katibu Mkuu wa Bakwata, Alhaj Nuhu Mruma amesema kupitia majukwaa tofauti viongozi wakuu wa baraza hilo, wakiongozwa na Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir wamekuwa wakisisitiza uchaguzi huo, uwe huru, haki na wenye weledi.
Alhaj Mruma amesema kwa nyakati tofauti Bakwata imekuwa ikiishauri mamlaka husika kufanya maandalizi mapema kwa kila hatua ya uchaguzi huo, uende kwa usalama ili wananchi wasipate shida ya kupiga kura, sambamba na kusimamia haki.
“Haki ni jambo muhimu katika suala la uchaguzi, kwa sababu bila haki tunaweza kuvuruga amani. Dhana yetu (Bakwata) hatuamini katika kuengua watu zaidi, bali tuaamini katika kuwaelimisha na kurekebisha kasoro walizonazo ili kuwa na sifa za kugombea,” amesema alipotafutwa na Mwananchi kuzungumzia uchaguzi huo.
Alipoulizwa kuhusu wito wa Bakwata kwa hatua zilizosalia za uchaguzi huo, Sheikh Mruma amesema: “Wito wetu kila hatua inayofanyika iende kwa uwazi na haki, lakini yafanyike maandalizi yaliyokamilika ili kuondoa sintofahamu itakayosababisha uchaguzi kwenda tofauti.”
Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda amesema jumuiya hiyo inasisitiza haki, uhuru na weledi kwa hatua zilizobaki za mchakato wa uchaguzi.
“Tangu mwanzoni tulionyesha wasiwasi wetu kuhusu mwenendo wa uchaguzi huu. Tunaona hakuna tofauti na ule wa mwaka 2019 na 2020, lakini kwa hatua zilizobaki basi mamlaka husika zitende haki, uamuzi wa wananchi uheshimiwe, kusiwe na upendeleo kwa chama fulani.
“Kungekuwa na uwezo basi ungeahirishwa ili watu warudi mezani kuzungumza ili kuona wapi kwenye changamoto na kuzirekebisha, lakini kwa hatua ya sasa haiwezekani, ndiyo maana tunasisitiza haki itendeke kuanzia kwenye kampeni, kuhesabu kura hadi kutangazwa washindi,” amesema.
Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) katika tamko lake la jana Novemba 14, ilianisha kasoro tano ilizozibaini katika mchakato uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji kuanzia uandikishaji hadi ngazi ya uteuzi wa wagombea huku ikisisitiza umuhimu wa uchaguzi kusimamiwa na Tume Huru ya Uchaguzi (INEC).
Kasoro hizo ni pamoja na malalamiko kuhusu daftari la wakazi, kuenguliwa wagombea, vikwazo katika kuchukua na kurejesha fomu, mapingamizi ya rufaa, kutekwa na kujeruhiwa kwa wananchi kunakohusishwa na masuala ya siasa na uchaguzi.
“Kumekuwa na malalamiko kuhusu uandikishaji wa wapigakura wasiokuwa na sifa, ikiwemo kuwepo kwa majina ya watu waliofariki dunia. Ili kurekebisha karoso hizo, CCT imeitaka Tamisemi kufanya uhakiki wa daftari hilo ili kuhakikisha wananchi wote watakaopiga kura wanaokuwa na sifa stahiki,” alisema Askofu Fredrick Shoo ambaye ni mwenyekiti wa CCT.
CCT ilisisitiza umuhimu wa uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji kusimamiwa kwa haki na usawa. Hata hivyo, ilipongeza mamlaka kwa jitihada za kuhakikisha mchakato huo unafanyika kwa uwazi.
Askofu Shoo alisema CCT inawataka wasimamizi wa uchaguzi huo kutekeleza majukumu yao kwa uwazi, usawa kwa kuzingatia sheria zilizowekwa bila upendeleo wa aina yoyote.
“Tunatumia fursa hii kukemea na kuitaka wizara kuwachukulia hatua pale inapothibitika wasimamizi hawa wamefanya makusudi au kwa uzembe, hii itasaidia kurejesha amani kwa wananchi. Tunahimiza mamlaka husika kuzingatia usawa na uwazi katika kutangaza matokeo halisi ya uchaguzi kwa kuzingatia muda bila ucheleweshaji wowote ambao mara nyingi unasababisha kukosekana kwa imani kwa wananchi na matokeo husika,” amesema
Mbali ya hayo, viongozi hao kwa ujumla wamewasihi Watanzania kufuatilia kampeni, kujitokeza kwa wingi kupiga kura Novemba 27, kuchagua kwa hekima, na kulinda amani na utulivu.
“Tunaiomba Serikali ihakikishe demokrasia inatawala nchini na kutuma ujumbe ulimwenguni kwamba Tanzania ni kisiwa cha amani ambayo tupo tayari kuishi na kuilinda.
“Endapo viongozi watapatikana kwa haki wananchi hawahitaji kukumbushwa kuwaombea na kuwapa ushirikiano muda wote wa uongozi wao,” amesema Askofu Pisa.