Dar es Salaam. Matumizi ya mkaa na kuni, mbali na kusababisha uharibifu wa mazingira, yametajwa pia kuwa chanzo cha magonjwa manane ya mfumo wa upumuaji, ambayo yanahatarisha afya ya watumiaji, wengi wakiwa wanawake.
Magonjwa hayo ni pamoja na saratani, mtoto wa jicho, kikohozi, mafua, pua kubana, macho kuwasha au kuwa mekundu, na kutoa machozi.
Hayo yameelezwa leo, Novemba 15, 2024, na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Mfumo wa Upumuaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk Mwanaada Kilima, aliposhiriki katika kampeni ya upandaji miti iliyofanyika katika Shule ya Sekondari ya NHC, Ubungo jijini Dar es Salaam.
Dk Kilima amesema mazingira na afya ni mambo yanayokwenda sambamba, hivyo kuna haja ya kutunza mazingira ili kupunguza vifo vinavyotokana na matumizi ya nishati chafu ya kupikia.
Ameeleza kuwa matumizi ya nishati hizo si tu yanahatarisha afya ya watumiaji bali pia yanachangia magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama vile kiharusi, magonjwa ya moyo na shinikizo la juu la damu.
“Takriban Watanzania 30,000 kila mwaka hufariki kutokana na matumizi ya nishati chafu ya kupikia, na kwa bahati mbaya sehemu kubwa ya wanaofariki ni wanawake, kwa sababu wao hutumia muda mwingi jikoni kupika,” amesema Dk Kilima.
Ameongeza kuwa mfumo wa upumuaji wa binadamu umeundwa kuingiza oksijeni na kutoa hewa chafu ya kaboni, na si kuvuta gesi chafu na chembechembe zinazodhuru afya.
Kwa upande wake, Joyce Shebe, mwanzilishi wa Taasisi ya Climate Voice of Tanzania, amesema kuna umuhimu kwa Watanzania kuachana na matumizi ya nishati chafu ya kupikia, kwani kufanya hivyo ni kuhatarisha maisha ya sasa na ya baadaye.
“Tukisema tuendelee kukata miti, huko mbele tutakumbana na changamoto nyingi zaidi zinazotokana na mabadiliko ya hali ya hewa. Ni kweli kuwa baadhi yetu tunatumia kuni na mkaa kutokana na hali ya kiuchumi, lakini juhudi zinaendelea kutafuta suluhisho,” amesema Shebe.
Shebe amesema ndiyo sababu wameanzisha kampeni ya kupanda miti 2,500 katika maeneo ya Ubungo Msewe, Kituo cha Polisi Ubungo, Hospitali ya Wilaya Ubungo na Shule ya Sekondari ya NHC. Kampeni hiyo inalenga kukabiliana na athari za ukataji miti na mabadiliko ya hali ya hewa.
Mratibu wa Nishati Safi ya Kupikia wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk Elizabeth Mshote amesema mkoa huo umeweka mikakati ya kuhakikisha wakazi wake wanatumia nishati safi ya kupikia ili kutunza mazingira.
“Sisi wakazi wa Dar es Salaam tunatumia asilimia 68 ya mkaa unaozalishwa maeneo mengine. Kwa hiyo, tukibadilika tutakuwa tumeokoa mazingira yasiharibiwe,” amesema Dk Mshote.
Aidha, Ofisa Hifadhi ya Misitu wa Wilaya za Ubungo na Kinondoni, Daudi Nkya amesema kazi yao kubwa ni kuhakikisha miti inapandwa kwa wingi ili kupunguza gesi zinazodhuru binadamu na mazingira.