Hekaya za Mlevi: Sasa imbeni “miskanka mishisha”…

Dar es Salaam. Waswahili waliposema “Pombe siyo maji” hawakukosea hata kidogo. Ilitokea siku moja tukitayarisha mazishi ya rafiki yetu aliyetutoka siku moja kabla.

Tukaliandaa kaburi kwa jinsi ilivyotakiwa, lakini tukiwa njiani kurudi msibani tukakiona kivuli. Tukaona si vibaya tukapate moja mbili za kutoa uchovu pamoja na kupunguza makali ya msiba. 
Tulikuwa kadiri ya watu sita tukiongozana na mpwa wa marehemu.

Basi tukapiga vyombo hadi vikatukolea. Uchovu uliisha lakini stori zikawa zimenoga hasa tulipokumbushana vituko vya marehemu aliyekuwa chama letu kwenye tungi. 

Kila tulipojiandaa kutoka, mmoja wetu aliuliza: “Kwani saa hizi watakuwa na ratiba gani kule?” Mwingine akajibu: “Saa hizi wanakula, kwani tuna njaa?” Wa tatu akashauri: “Kama ni njaa hata hapa si kuna misosi? Au tupate ‘one for the road’ kabla ya kutimka?”

Mtu wa mwisho kuchangia maongezi ndiye aliyeharibu kabisa. “Jamani, sisi jukumu letu tumekwisha kulikamilisha.

Tuna haja gani ya kukimbizana wakati tunazika kesho? Au kuna mwanakwaya humu?” Alipoona sote tukiwa kimya tukitafakari, na ukizingatia tafakari hizo ziliongozwa na pombe tuliyokwisha kuinywa, hakuna aliyebisha. 

Akamgeukia mhudumu: “Lete ugali na mboga zote, ongeza na raundi nyingine!”

Amini usiamini, niliamshwa na kilio saa nane za usiku. Niliinuka kitini nihamie jamvini nikiamini nipo msibani, lakini muziki niliousikia ulinikatalia.

Astakafiru!!! Nilipozungusha macho kwa “waombolezaji” nikauona msafara uleule niliokuja nao kupunguza uchovu tulipotoka makaburini. Watatu walikuwa wakinywa huku wakilia, na wawili walishaangusha sakafuni. Nilijuta kukubali ushauri wa ibilisi tuliyeongozana naye.

Haraka tuliamshana na kuanza safari ya kurudi msibani. Palikuwa na umbali wa urefu wa kiwanja cha mpira tu, lakini ilituchukua masaa mawili njiani. Wote (kasoro mimi) walikuwa wakianguka kila baada ya hatua chache, wakalia kwa mayowe hadi kuwaamsha popo tuliowapita njiani.

Waombolezaji kule msibani walitoka kwa kudhani kuwa kumetokea msiba mwingine hapo mtaani.  Ukweli halikuwa jambo la kusimulia, lakini nimelazimika kwa sababu maalumu tu.

Sababu yenyewe ni kwamba nilijiuliza kwa nini wenzangu walipandwa na mzuka baada ya kupiga vyombo. Nakumbuka wakati uliopita vijana walicharuka kwa utoro wa kuzamia ughaibuni kwa madai kwamba maisha ya Bongo nuksi.

Wenyewe walijiita mabaharia, lakini walidandia meli kama usafiri tu na si vinginevyo. Baadhi walifanikiwa kupata vibarua humohumo melini, wengine walitoswa kwenye maji marefu na wengine walifanikiwa kujificha mpaka wakaingia Ulaya.

Wenyewe walikuwa na usemi wao, ati “Bora kuzaliwa mbwa Ulaya kuliko kuzaliwa binadamu Bongo”.

Hivyo mtu alikuwa radhi kujificha kwenye dampo la melini mwezi mzima kwa imani kuwa “wan dei yes”. Lakini pamoja na yote hayo, wale waliofanikiwa kuingia ughaibuni waliishi kama digidigi. Walijua fika kwamba huko ugenini dakika yoyote ile kingenuka.

Ndio maana walitembea “full package” wakati wakitafuta vibarua mtaani. Kwa vile hawa jamaa walitorokea huko bila kujipanga, walijikuta wakitafuta vibarua vya ujira wa siku mitaani. Kwa vile hawakuwa na vibali, walichukuliwa kuwa wahuni na wahalifu.

Hivyo wakawa “wanted”. Kila mmoja wao alivaa suruali tatu, fulana tatu, mashati matatu na akiba yake yote ya fedha ilikuwa mfukoni. Ikitokea bahati mbaya akarukiwa mtaani, angerudishwa kama alivyokutwa. Hakukuwa na wasaa wa kushikishana “kitu kidogo” wala kupelekwa magetoni kuchukua chochote.

Hivyo walirudishwa wakiwa na hali mbaya zaidi. Ndipo kwa mara ya kwanza tukaona ubaya wa msongo. Vijana wakazagaa mitaani na kujidunga madawa ili kupunguza msongo.

Kijana alipojidunga pale kando ya mfereji alijisikia akiwa mbele ya fukwe za Oman. Hapa ndipo nilipothibitisha uongo wa kilevi, kinazipandishia hisia zako mwenyewe wakati wewe unaamini kuwa kinakupa majibu.

Ajabu ati hivi leo watu wanalazimisha dawa za kulevya, skanka na shisha kuwa sehemu ya starehe. Huku uswazi ili sherehe itajwe kuwa imefana, basi iwe na shisha.

Huu ni uongo mkubwa kwani Mamlaka ya Kupambana na Kudhibiti Dawa za Kulevya imesanua kila kitu. Mamlaka imesema kulingana na utafiti uliofanyika, wavuta skanka na shisha wamekuwa wakijiliwaza kuondokana na majanga yao, wala si kustarehe.

Utafiti unaonesha kuwa wamama na masista du ndio wateja wakubwa wa mimoshi hiyo inayochanganywa na madawa. Wenyewe walipohojiwa walikiri kufikwa na masahibu yaliyowaganda kama kuvunjika kwa mahusiano na kuteleza kiuchumi.

Wachache walisema kuwa walidanganywa kwamba hiyo ni starehe kama zingine, lakini wakajikuta wamenasa kwenye uraibu. 

Vijana wanamichezo na wasanii hunasa kwenye mtego kama huo kwa kudanganywa kuwa wakipata stimu basi vaibu lao linaongezeka. Waliotumia walinasa mapema kwenye uraibu, na wakajikuta wanafanya kazi kwa nguvu ili kuuridhisha uraibu wao. Uwezo wa kazi ulipokwisha wakabaki kuwa ombaomba. 

Utashangaa kuwa hata watoto nao wamo kwenye kadhia hii. Pita usiku kwenye kijiduka kinachouza kinywaji “cha buku”. Utamkuta mwanafunzi wa sekondari aliyefeli somo la Chemistry akikuchanganyia “vya buku” vitatu na energy. Mikupuo miwili tu, unakwenda chali. Sasa anatumika dukani hapo kama mtengeneza Cocktail. 

Related Posts