Dar es Salaam. Shughuli za biashara katika eneo la Kariakoo mtaa wa Mchikichi na Congo zimesimama kwa muda, huku Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akitarajiwa kufika eneo la tukio muda wowote kuanzia sasa.
Tangazo la kuwasili kwa Waziri Mkuu limetolewa kupitia redio ya matangazo katika eneo la tukio.
Maelfu ya raia katika soko hilo wamesimamisha shughuli zao wakisubiri kuwaona ndugu zao waliofukiwa na kifusi katika jengo la ghorofa tano lililoporomoka saa tatu asubuhi.
Japo hakuna tukio la kifo lililothibitishwa hadi sasa, idadi ya majeruhi inazidi kuongezeka na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema wamepelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
Wakati mkuu wa mkoa akieleza hayo, majeruhi wengine wanaendelea kuokolewa na mwandishi wa habari hizi ameshuhudia wakiwekwa katika gari aina ya kirikuu na wengine kwenye gari la kubeba wagonjwa.
Baadhi ya majeruhi walioondolewa katika vifusi hivyo, wameeleza wapo wenzao waliokwama chini wakiomba msaada wa haraka uwafikie.
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji likishirikiana na baadhi ya wafanyabiashara, wanaendelea na ufukuaji wa vifusi, huku nguvu ikiongezwa na raia wa kigeni waliojumuika na vikosi vya Zimamoto kufanya Uokoaji.
Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili Profesa Mohamed Janabi, ni mmoja wa wataalamu wanaongoza uokoaji.
Wengine ni Kamanda wa Polisi mkoa wa Dar es Salaam Jumanne Muliro, Naibu Spika wa Bunge Musa Zungu, Mkuu wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo.
Hadi sasa kelele za ving’ora za magari ya wagonjwa ndizo zilizotawala mitaa yote ya Kariakoo, huku Jeshi la Polisi likionya wananchi kuondoka karibu na eneo la tukio kurahisisha shughuli ya uokozi.