Dar es Salaam. Leo Novemba 16, 2024 wakazi wa Kariakoo wameshtushwa na tukio la kuanguka kwa ghorofa lenye ghorofa nne.
Ajali hiyo imesababisha hofu kubwa, huku mamia ya watu wakiendelea kukusanyika eneo hilo kushuhudia juhudi za uokoaji.
Kwa mujibu wa mashuhuda, ghorofa hilo lilianguka ghafla saa tatu na dakika tano asubuhi wakati mafundi ujenzi walipokuwa kazini wakitoboa kwa ajili ya kuongeza sehemu ya maduka.
“Tulianza kusikia kelele za mtikisiko, kisha kwa ghafla jengo zima likaanguka. Wananchi wameshindwa kujiokoa na zoezi la ujenzi lilianza tangu jana hivyo angetaka urahisi angebomoa tu jengo lote,” amesema mmoja wa mashuhuda, Harrison Shayo.
Vikosi vya uokoaji kutoka Jeshi la Zimamoto na Uokoaji vilifika eneo la tukio ndani ya muda mfupi na kuanza kazi ya kuondoa vifusi kwa kutumia vifaa maalum. Hata hivyo, changamoto kubwa ni upungufu wa mashine nzito za kunyanyua vifusi, jambo linalosababisha kazi hiyo kuchukua muda mrefu.
Majeruhi waliokolewa wamepelekwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu. Wakati huo Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo Profesa Mohamed Janabi akiwepo katika zoezi la kuwasaidia majeruhi.
Tukio hili limeibua maswali mengi kuhusu ubora wa majengo yanayojengwa katikati ya jiji.
Wataalamu wa ujenzi walioko eneo la tukio wamesema kuna uwezekano wa jengo hilo kuanguka kutokana na matumizi ya vifaa duni au ukosefu wa ufuatiliaji wa taratibu za ujenzi.
“Kwa sasa tukifuatilia majengo mengi yanabomolewa eneo la Kariakoo ili kujengwa upya na kuboresha zaidi, lakini pia hali ya ufuatiliaji ni muhimu hususani kwa majengo mapya yanayoendelea kujengwa,” amesema Hamis Mwinyi ambaye pia ni mmoja wa mainjinia anayesimamia ujenzi katika mtaa wa Nyamwezi.
Akizungumza mmoja waokoaji ambaye ni askari wa jiji, Ibrahimu Mussa amesema amewasaidia watu zaidi ya 10 ambao aliwaona kwa karibu huku wakibaki wengine katika eneo la koridoni.
“Nilifika kwenye usawa wa ngazi na kuwasaidia baadhi yao kwa kuwashika mkono na kuwavuta nje waliobaki wengi wao wapo chini na nimetoka kwa sababu ya kuzidiwa na hali ya hewa,” amesema
Viongozi watembelea eneo la tukio
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amefika katika eneo tukio na kutoa pole kwa familia za walioathirika pia akiwataka wananchi waliopo kwenyewe maghorofa ya jirani washuke chini.
Pia, yupo Naibu Spika na Mbunge wa Ilala Mussa Zungu, Mkuu wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo na kamanda wa Kanda Malaamu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro.