Dube akabidhiwa Wasudan CAFCL | Mwanaspoti

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga,  Ally Kamwe amesema mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi Al Hilal utakuwa na kaulimbiu ya ‘Watake wasitake, tutafungua milango iliyofungwa’ huku akimkabidhi mchezo huo, Prince Dube ambaye kwa siku za karibuni amekuwa akilalamikiwa hafungi.

Kamwe anaamini kwenye mchezo huo straika huyo atafunga, ikiwa hadi sasa amefunga bao moja kwenye michuano ya CAF, katika hatua za awali , huku akiwa hana bao Ligi Kuu Bara.

“Tarehe 26 ni 𝐃𝐔𝐁𝐄 𝐃𝐀𝐘, nyie si mnasema hafungi, sisi tunakwenda kufungua kila kilichofungwa, nendeni pia mkaandike Kauli mbiu ‘Watake Wasitake, tutafungua milango iliyofungwa’.

Amesema tiketi za mchezo huo zimeanza kuuzwa leo kwenye vituo mbalimbali na bei zake zipo kama ifuatavyo;

• VIP A 30,000
• VIP B 20,000
• VIP C 10,000
• Machungwa na Mzunguko 3000

Yanga inauendea mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza michezo miwili mfululizo kwenye Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam FC na Tabora United.

Yanga dhidi ya Al Hilal utakuwa ni mchezo wa kisasi kwa Yanga kwani walitolewa kwenye mashindano hayo na Wasudani hao msimu wa 2022-2023.

Katika msimu huo wa 2022-2023, timu hizo zilikutana hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kusaka tiketi ya kutinga makundi na mechi ya kwanza iliyopigwa Benjamin Mkapa, Oktoba 8, 2022, zilifungana bao 1-1.

Mchezo wa marudiano uliopigwa Oktoba 16, 2022, kwenye Uwanja wa Al-Hilal, jijini Omdurman Sudan, Yanga ilichapwa bao 1-0, na kutolewa kwa jumla ya mabao 2-1 kisha kuangukia Kombe la Shirikisho Afrika na kufika fainali.

Msimu huo ambao Yanga ilifika fainali ilicheza na USM Alger ya Algeria na mechi ya kwanza Dar es Salaam ilipoteza kwa mabao 2-1, Mei 28, 2023, kisha marudiano ikashinda 1-0, Juni 3, 2023 na kukosa ubingwa kwa faida ya bao la ugenini.

Related Posts