Dar es Salaam. Katika ulimwengu wa kisasa, uchaguzi ni daraja linalowaunganisha wananchi na viongozi wao wa kuchaguliwa, kuwezesha demokrasia kuimarika na kushamirisha maendelei ya nchi.
Lakini, kwa bahati mbaya, baadhi ya watu wamekuwa wakigeuza mchakato huo kuwa chanzo cha chuki, vurugu na mifarakano.
Kwa mujibu wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), uchaguzi ni mchakato wa kikatiba unaowawezesha wananchi kushiriki moja kwa moja katika kuchagua viongozi wa kuwawakilisha.
Takwimu za mwaka 2022 za shirika hilo zinaonyesha nchi 167 duniani zimeanzisha mifumo ya uchaguzi wa kidemokrasia, ikiwa ni ongezeko la asilimia 23 tangu mwaka 2000.
Katika demokrasia imara, uchaguzi unapaswa kuwa fursa ya mazungumzo ya kiungwana kuhusu mustakabali wa taifa, badala ya kuwa uwanja wa mapambano ya chuki.
Hata hivyo, ripoti ya Taasisi ya Kimataifa ya Demokrasia na Usaidizi wa Uchaguzi (IDEA) ya mwaka 2023, ilibaini katika nchi 33 duniani, uchaguzi umehusishwa na ghasia za kisiasa, hasa wakati wa kampeni na siku ya kupiga kura.
Chuki, ghasia wakati wa uchaguzi
Chuki na ghasia mara nyingi husababishwa na ukosefu wa elimu ya uraia, kukosa imani katika taasisi za uchaguzi na ubinafsi wa viongozi wa kisiasa.
Hali hii imeonekana hata hapa nchini, ambako ripoti ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) ya mwaka 2020 ilionyesha asilimia 21 ya migogoro ya uchaguzi ilitokana na lugha za uchochezi kutoka kwa wanasiasa.
Lugha kama hizo, vitisho, ghasia na kukosa Imani na mifumo vimetajwa mara kadhaa kuwa sababu za wananchi kutoshiriki kikamilifu katika upigaji kura.
Mathalan, katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2019, Tanzania ilirekodi idadi ndogo zaidi ya wapigakura, yaani asilimia 33 tu ya waliojiandikisha ndio walipiga kura.
Hii inaonyesha jinsi masuasla hayo yanavyoweza kudhoofisha mchakato wa uchaguzi.
Uchaguzi wa amani unavyosaidia demokrasia
Kwa mujibu wa ripoti ya Tume ya Uchaguzi ya Afrika Kusini (IEC) ya mwaka 2021, uchaguzi wa amani unachangia kwa asilimia 45 kuimarisha mshikamano wa kijamii na kupunguza mgawanyiko wa kisiasa.
Uchaguzi wa kidemokrasia, ambao unafanyika kwa uwazi na haki huimarisha imani ya wananchi kwa Serikali yao na kuwatia moyo kushiriki katika masuala ya maendeleo.
Mfano mzuri ni uchaguzi wa Ghana mwaka 2020, ambapo licha ya changamoto za kisiasa, asilimia 79 ya wapigakura walishiriki kwa amani, hatua ambayo iliwezesha nchi hiyo kutajwa kuwa mfano wa kuigwa barani Afrika, kwa mujibu wa IDEA, mwaka 2021.
Jukumu la wananchi, viongozi katika kudumisha amani
Kwanza, mwananchi anapaswa kuelewa kwamba uchaguzi si vita, bali ni nafasi ya kuchagua viongozi bora na elimu hii inapaswa kutolewa na Serikali, taasisi za kiraia na watu binafsi.
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) katika tamko lake la mwaka 2022 lilisisitiza kuwa uchaguzi wa haki unahitaji mshikamano wa kijamii na kuepuka lugha za matusi au uchochezi.
Pili, viongozi wa kisiasa wanapaswa kuwa mfano wa kuigwa kwa kuendesha kampeni za kistaarabu.
Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa aliwahi kusema mwaka 2004: “Demokrasia haiwezi kustawi kwenye mazingira ya chuki. Ni lazima tujifunze kuheshimu mawazo ya kila mmoja wetu.”
Kauli hii inaendelea kuwa na uzito mkubwa, hasa tunapokaribia uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024.
Faida za uchaguzi huru, haki
Kwa mujibu wa Shirika la Transparency International mwaka 2023, nchi zilizo na uchaguzi huru na haki zina maendeleo ya haraka zaidi ya kiuchumi kwa asilimia 13 kuliko nchi zinazokumbwa na vurugu za uchaguzi.
Hii ni kwa sababu uchaguzi wa amani hujenga mazingira bora kwa uwekezaji na maendeleo.
Tanzania inaweza kujifunza kutoka kwa nchi kama Mauritius, ambayo imekuwa ikifanya uchaguzi wake kwa uwazi mkubwa tangu mwaka 1968.
Asilimia 91 ya wapigakura walioshiriki katika uchaguzi wa mwaka 2020 nchini humo waliripoti kuwa na imani na mfumo wa uchaguzi kwa mujibu wa Benki ya Dunia mwaka 2021.
Ili kuwa na uchaguzi mzuri, elimu ya uraia inapaswa kutolewa na Serikali na wadau kwa wananchi, hasa vijana ambao mara nyingi ndio wanaohusika katika vurugu za uchaguzi.
Kadhalika, uwajibikaji wa viongozi, vyama vya siasa vinapaswa kuchukua hatua kali dhidi ya wagombea au wanachama wanaohamasisha chuki.
Kuweka sheria madhubuti ili kuhakikisha kwamba lugha za uchochezi na vitendo vya chuki vinaadhibiwa ipasavyo.
Taasisi za kidini na viongozi wake wanapaswa kushirikiana na Serikali katika kuhubiri amani na mshikamano kabla na baada ya uchaguzi.
Zieleze kwa uwazi kuwa uchaguzi siyo chuki, bali ni mchakato wa kidemokrasia unaopaswa kuimarisha mshikamano wa kijamii na ustawi wa taifa.
Wakati tunapoelekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa Novemba 27, mwaka huu, ni muhimu kwa kila mmoja wetu, kama raia au kiongozi, kuhakikisha anashiriki katika kuufanya uchaguzi huu kuwa wa haki na amani.
Kwa maneno ya Nelson Mandela: “Demokrasia haimaanishi kuwa huru tu kupiga kura, bali pia kuishi kwa mshikamano bila woga wa matusi au chuki.”
Tunapaswa kulinda demokrasia yetu kwa kuhakikisha uchaguzi unakuwa mchakato wa kujenga, siyo kubomoa taifa letu.
Moja ya njia muhimu za kuimarisha demokrasia ni kuwashirikisha vijana kwa njia chanya katika mchakato wa uchaguzi.
Kundi hili linachukua asilimia 60 ya idadi ya watu barani Afrika kwa mujibu wa Umoja wa Afrika (AU) mwaka 2022, hivyo lina ushawishi katika kufanikisha uchaguzi wa amani.
Hata hivyo, mara nyingi vijana wanatumiwa vibaya na wanasiasa kwa kuchochea vurugu.
Katika ripoti ya Taasisi ya Kimataifa ya Vijana na Demokrasia (IYDI) ya mwaka 2023, ilibainika kuwa nchi zinazowekeza katika programu za elimu ya uraia kwa vijana zimepunguza kwa asilimia 30 matukio ya vurugu za uchaguzi.
Hili linaonyesha umuhimu wa kutoa mafunzo ya kina kuhusu thamani ya demokrasia na athari za chuki kwa maendeleo ya taifa.
Zaidi ya hayo, vijana wanapaswa kupewa nafasi za kushiriki katika uongozi wa vyama vya siasa na mchakato wa kufanya maamuzi.
Hatua hii inaweza kuhamasisha mshikamano na kuwapa ari ya kutetea amani badala ya kushiriki katika vurugu.
Nchin,i programu kama Mfumo wa Uwezeshaji Vijana wa Kitaifa (NYPF) zimeonyesha mafanikio katika kuwajengea vijana uelewa wa kidemokrasia, lakini juhudi hizi zinapaswa kuimarishwa.
Kwa pamoja, tukiwashirikisha vijana kwa hekima na busara, tutakuwa tumelinda si tu uchaguzi wa sasa bali pia misingi ya demokrasia kwa vizazi vijavyo.
Uchaguzi wa amani si tu wajibu wa viongozi na taasisi, bali wa kila mmoja wetu kama sehemu ya jamii inayotaka maendeleo.