Mahakama yakubali Oryx kusikilizwa kuhusu utekelezaji kulipa Sh460 bilioni

Dar es Salaam. Mahakama ya Rufani imekubali kuzisikiliza kampuni za Oryx Oil Company Limited na Oryx Energies SA katika shauri lao la maombi ya kusimamisha utekelezaji wa amri ya Mahakama Kuu ya kuilipa kampuni ya Oilcom Tanzania Limited, fidia ya  jumla ya zaidi ya Sh468 bilioni.

Katika uamuzi wake uliotolewa na jopo la majaji watatu, Rehema Mkuye (kiongozi wa jopo), Abrahamu Mwampashi na Paul Ngwembe, Novemba 13, 2024, mahakama hiyo imemuamuru Msajili wa Mahakama kupokea maombi ya kampuni hizo za Oryx ya kuomba kusimamisha kwa muda utekelezaji wa malipo hayo.

Mahakama hiyo imefikia uamuzi huo baada ya kutupilia mbali shauri la maombi ya kampuni ya Oilcom, iliyokuwa ikipinga uamuzi wa Jaji mmoja wa mahakama hiyo, uliotolewa na Jaji Dk Benhajj Masoud.

Awali, kampuni za Oryx ziliwasilisha maombi ya kusimamisha utekelezaji wa tuzo iliyotolewa na Baraza la Usuluhishi, ambalo liliziamuru kuilipa fidia Oilcom kiasi hicho cha pesa kufuatia shauri la usuluhishi wa ukiukwaji wa mkabata wa kibiashara baina ya pande hizo mbili.

Baraza la Usuluhishi katika tuzo hiyo iliyotolewa Novemba 30, 2023 na wasuluhishi  Jaji mstaafu wa Mahakama ya Rufani, Engera Kileo, Jaji mstaafu wa Mahakama Kuu, Sophia Wambura na Profesa Mussa Assad, waliiamuru Oryx kuilipa Oilcom Sh468 bilion.

Shauri hilo la usuluhishi lilifunguliwa na Oilcom ikizilalamikia kampuni za Oryx kukiuka mkataba wa ukodishaji wa magari ya kusafirishia mafuta, ambao pande hizo mbili ziliingia mwaka 2016.

Baraza hilo la usuluhishi katika uamuzi wake liliziamuru kampuni za Oryx kuilipa fidia kampuni ya Oilcom jumla ya Dola za Marekani 147,200,221 zaidi ya Sh468 bilioni.

Fedha hizo zinajumuisha malipo ya fidia ya hasara halisi, fidia ya hasara ya jumla ya Dola za Marekani 20,000,000.

Pia kampuni hizo ziliamriwa kulipa riba ya asilimia tano ya fedha hizo kwa mwaka, kutoka tarehe ya kufunguliwa madai mpaka tarehe ya kutolewa tuzo ya mwisho ya Baraza, na riba ya asilimia tatu kwa mwaka kuanzia tarehe ya kutolewa tuzo mpaka tarehe ya kumaliza malipo yote.

Kufuatia uamuzi huo wa Baraza la Usuluhishi, Oilcom ilifungua shauri la maombi Mahakama Kuu ikiiomba mahakama hiyo kuisajili tuzo hiyo iwe uamuzi wake (mahakama) kwa ajili ya utekelezaji kwa mujibu wa sheria.

Kampuni za Oryx zilipambana kujaribu kuzuia usajili wa tuzo hiyo mahakamani hapo baada ya kufungua mashauri mawili kwa nyakati tofauti kupinga usajili wa tuzo hiyo bila mafanikio, baada ya mahakama hiyo kuyatupilia mbali mashauri yake yote.

Hivyo mahakama hiyo katika uamuzi wake uliotolewa na Jaji Salma Maghimbi Mei 3, 2024 iliisajili tuzo hiyo iliyotolewa na Baraza la Usuluhishi na kuwa uamuzi wake ambao sasa unaweza kutekelezwa na kuziamuru kampuni ya Oryx, kuilipa Oilcom kama zilivyoamriwa na Baraza la Usuluhishi.

Baada ya Mahakama kusajili tuzo hiyo, kampuni hizo zilikata rufaa Mahakama ya Rufani kupinga uamuzi huo. Pia ziliwasilisha shauri la maombi ya kusimamisha utekelezaji wa malipo ya tuzo hiyo kusubiri usikilizwaji na uamuzi wa rufaa yao, lakini  msajili wa mahakama hiyo aliyakataa maombi hayo.

Kampuni za Oryx ziliwasilisha malalamiko yake kwa Jaji Masoud kuhusu  msajili kukataa maombi yao ya kusimamisha utekelezaji wa tuzo hiyo na Jaji Masoud baada ya kusikiliza malalamiko hayo, aliteungua uamuzi wa msajili akisema kuwa alikwenda nje ya mamlaka yake ya kisheria.

Hivyo Jaji Masoud aliamuru maombi yao yapokelewe na kusajiliwa.

Hata hivyo, Oilcom haikukubaliana na uamuzi huo wa Jaji Masoud, ndipo ikafungua shauri la kupinga uamuzi huo wa Jaji Masoud.

Lakini jopo la majaji hao baada ya kusikiliza hoja za pande zote katika uamuzi wake huo limetupilia mbali shauri la Oilcom kupinga uamuzi wa Jaji Masoud.

Badala yake imekubaliana na uamuzi wa Jaji Masoud kuwa msajili kukata kuyakataa maombi hayo ya Oryx kwa sababu ilizozitoa kuwa alikwenda nje ya mamlaka yake ya kisheria.

Akizungumzia uamuzi huo, wakili wa Oryx, Gaspar Nyika amelieleza Mwananchi kuwa kwa uamuzi huo,  sasa maombi ya wateja wake ya kusimamisha utekelezaji wa tuzo hiyo yatasikilizwa na kwamba yamepangwa kusikilizwa Jumatatu, Novemba 18, 2024.

“Kwa hiyo mahakama baada ya kutusikiliza itakubaliana na hoja zetu basi itatoa amri ya kusimamisha kwanza utekelezaji huo mpaka rufaa zetu zitakaposikilizwa na kuamriwa”, amesema Nyika.

Related Posts