Unguja. Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud amezifariji familia zilizopoteza vijana wao katika vifo vyenye utata, huku akizitaka kuwa na subra kwani serikali inao wajibu kutafuta ukweli wa jambo hilo.
Novemba 9, 2024 saa 12.00 asubuhi dereva wa gari aina ya Dayna, Msina Sharif (39) na msaidizi wake Abdala Bakari (28) walifariki dunia na wengine wawili Mohamed Issa (10) na Hamza Abdalla Abasi (10) wote wanafunzi wa Shule ya Msingi Kidoti walijeruhiwa.
Katika taarifa iliyotolewa na polisi kwa waandishi wa habari Novemba 10, 2024 kupitia kwa Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi Makosa ya Jinai Zanzibar, Zubeir Chembera ilieleza taarifa za awali za tukio hilo zinaonyesha watu hao wamekufa baada ya gari lao kugonga mti na kusababisha vifo lakini uchunguzi zaidi unaendelea kubaini kiini.
Pamoja na uchunguzi, Chembera alisema polisi wameunda kamati maalumu kwa ajili ya kuchunguza tukio hilo ambalo taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii na iliyotolewa na Chama cha ACT-Wazalendo zilidai watu hao wamepigwa risasi na polisi kwa sababu walikutwa na mchanga kinyume cha taratibu.
“Tunautaarifu umma kufuatia tukio hilo la kusikitisha, imeundwa tume huru ya uchunguzi ili kufanya uchunguzi wa haraka kujua kiini cha tukio hilo ikiwa ni pamoja na sababu ya gari hilo kukimbia na magari mengine kushambulia askari, na askari kufyatua risasi baada ya uchunguzi kukamilika umma utajulishwa,” alisema Chembera.
Alisema siku ya tukio askari polisi na askari wa vyombo vingine vya ulinzi na usalama wakiwa kwenye operesheni maalumu katika mkoa huo, Wilaya ya Kaskazini A, Kijiji cha Kidoti walikutana na gari la mizigo aina ya Toyota Dyana lisilo na namba za usajili.
Kwa mujibu wa Chembera, polisi walitilia shaka gari hilo na kulisimamisha ili kulifanyia upekuzi lakini halikusimama badala yake dereva aliongeza mwendo kuwakimbia polisi.
“Gari hilo lilikaidi na kukimbia likipiga honi, hivyo kuhamasisha magari mengine yaingie barabarani yakiwa yamepakia watu na kuanza kulishambulia gari la polisi kwa mawe, askari walifyatua risasi juu kutahadharisha kusimama na kutawanya magari yaliyokuwa yanashambulia askari hao kwa mawe,” alisema.
Alisema dereva wa gari hilo aliendelea kukaidi hivyo gari lilipoteza mwelekeo na kugonga mti wa Mkungu na kusababisha dereva wa gari hilo Msina Sharif na msaidizi wake Abdala Bakari kupoteza maisha.
Novemba 10 hiyohiyo, Msemaji wa Ofisi, Kamati ya Wasemaji wa Kisekta, Chama cha ACT-Wazalendo Zanzibar, Hamad Mussa Yussuf alisema wanalitaka Jeshi la Polisi Zanzibar kutoka hadharani kueleza waliofanya tukio hilo na kuchukua hatua za haraka.
“Hiki ni kitendo cha mauaji, tunalitaka Jeshi Polisi lisema waliofanya tukio hili kisha hatua za haraka zichukuliwe dhidi ya waliohusika kwani watu wanadaiwa kupigwa risasi,” alisema.
Akizungumza baada ya kuzitembelea familia hizo jana Novemba 15, 2024 Othman alisema linapotokea jambo kama hilo kwa yoyote aliyehusika ni wajibu wa Serikali kuutafuta ukweli na kuuweka hadharani bila kuficha ili jamii iweze kufahamu kile lilichotokea.
“Njia hiyo ni muhimu katika kusaidia pia kuzuia matukio ya namna hiyo yasiweze kujirejea na inasaidia kupatikana ukweli na sababu zilizofanya kutokea jambo kama hilo na haki iweze kutendeka,” amesema.
Katika taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari kupitia kitengo cha habari ofisi ya Makamu wa Kwanza, Othman amesema bila Serikali kutafuta ukweli halisi na ukafahamika ni vigumu kutatua tatizo lililosababisha hali hiyo na kudhibiti isijirudie.
Amewapongeza wananchi hao kwa ustahimilivu wao kwenye jambo hilo licha ya kuwepo changamoto kubwa iliyojitokeza.
Othman amesema hali hiyo itasaidia kuweka jitihada na Serikali kutimiza wajibu wao wa kudhibiti matatizo kama hayo.
Amewaahidi wananchi hao kwamba, Serikali itahakikisha kila mwenye haki kwenye jambo hilo itapatikana na kuwasihi waendelee kuwa watulivu kama walivyoonyesha wakati tukio lilipotokea.
Kuhusu kuhusishwa kwa polisi katika vifo hivyo, Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Chembera amesema kama taarifa zilivyotolewa watu hao waligonga mti lakini bado kamati iliyoundwa inaendelea na uchunguzi ikimaliza kila kitu kitawekwa hadharani.