Wakulima wa mwani Buyu walia kukosa njia

Unguja. Ukosefu wa njia umedaiwa kuwa kikwazo kwa wakulima wa mwani na uvuvi katika shehia ya Buyu, Mkoa wa Mjini Magharibi hivyo kurejesha nyuma jitihada zao za kujikwamua kimaisha.

Pia wamesema wana hofu ya kuondolewa kwa sababu eneo wanalopita ni la Kambi ya Kikosi cha Zimamoto na Uokozi, hivyo kuna wakati wanapokea kauli kutoka kwa baadhi ya maofia kuwa wataondolewa katika eneo hilo.

Wametoa kauli hizo leo Novemba 16, 2024 baada ya Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Shaabani Ali Othman kufanya ziara iliyowashirikisha viongozi wa shehia, wadi na uongozi wa Kikosi cha Zimamoto katika eneo hilo.

Zainabu Hussein Ali, mkulima wa zao hilo amesema baada ya kilimo changamoto yao ni wakati wa mavumo hawana njia maalumu kupitisha mazao yao, hivyo hulazimisha kupita maeneo ambayo hayana njia na kuhatarisha maisha yao.

“Hivi sasa hakuna njia, tunayoitegemea imezibwa, kwa hiyo tunapita kwenye mzunguko na mawe makubwa, huku kukiwa na vichaka. Kwa sasa tunapopita ni eneo la mtu lakini kuna njia ndogo, na kuna fensi zimeziba, tunatumia upande wa bahari kwa kujibana,” amesema.

Baada ya kusikiliza kero za wakulima, Waziri Shaabani amekishauri Kikosi cha Zimamoto na Uokozi Zanzibar katika Shehia ya Buyu kuwatengenezea njia ya kupita wakulima hao ili iwe rahisi wao kuendesha shughuli zao za kilimo.

Kuhusu kuondolewa,  amewatoa wasiwasi akisema wataendelea na shughuli zao kwa sababu tayari wameshazungumza na uongozi na hakuna jambo kama hilo.

Naibu Kamishna wa Kikosi cha Zimamoto, Mrisho Iddi Mbaraka amesema wamepokea ushauri huo na wapo tayari kuufanyia kazi kwa ajili ya usalama wa wananchi hao kuendesha shughuli za kuanika mwani pamoja na wapitanjia wengine katika eneo hilo.

“Tutaufanyia kazi kuwaandalia njia ili kuondoa sintofahamu hizi,” amesema.

Diwani wa Wadi ya Chukwani, Fatma Rashid Juma amesema kuwepo kwa njia ya uhakika ni jambo jema kwani haitawasaidia wakulima pekee, bali pia wananchi wengine kwa ajili ya shughuli zao za kila siku.

Amesema hatua hiyo itaondoa migogoro isiyokuwa ya lazima na kuleta umoja katika jamii hiyo.

Hata hivyo, amewataka wakulima kutoa ushirikiano wa pamoja katika utatuzi wa matatizo yanayojitokeza katika eneo hilo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uvuvi ya Chukwani Ramadhan Khamis amewataka wakulima kuwa walinzi baada ya kukamilika kwa njia hiyo ili kudhibiti vitendo vya uhalifu visijitokeze eneo hilo.

Related Posts