Tabora. Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango ametoa rambirambi ya Sh5 milioni kwa familia ya aliyekuwa Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Nyahua Stesheni, Wilaya ya Sikonge mkoani Tabora, Said Maduka (47), aliyeuawa na kisha kuchomwa moto, wakati akipeleka wito wa mahakama kwa wananchi wake.
Rambirambi hiyo imetolewa leo Novemba 15, 2024 na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha kwa niaba ya Makamu wa Rais, ambapo alitoa ahadi hiyo alipofanya ziara ya kikazi wilayani humo Oktoba 2024.
Akielezea tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Sikonge, Colnel Maghembe amesema marehemu Maduka alipoteza maisha, baada ya kutoweka Septemba 9, 2024 na alikuwa mtendaji wa Serikali.
Alifikwa na umauti baada ya kuchomwa moto na wanaodaiwa kuwa wananchi wake alipokuwa akiwapelekea wito wa Mahakama.
“Kulikuwa na kesi mahakamani iliyokuwa ikiendelea dhidi ya wananchi aliokuwa akiwaongoza, Mahakama ikatoa wito (samansi) kwa ajili ya kuwaita wananchi hao kuhudhuria kesi, ikampa ili apeleke wito huo kwa wananchi hao. Wakati akitekeleza wajibu huo, katika mazingira hayo, akapotea na baadaye akapatikana Septemba 21 akiwa amechomwa moto uliounguza usafiri wake wa pikipiki na kubaki majivu,” amesema na kuongeza:
“Inadaiwa kwamba wananchi aliokuwa akiwapelekea ule wito waliamua kumchoma moto ili kupoteza ushahidi wa wao kuitwa kutokana na uzito wa kesi ilivyokuwa,” amesema Maghembe.
Hata hivyo, Maghembe ameongeza kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vya wilayani humo viliingia kazini ambapo watu wawili wanaodaiwa kutekeleza mauaji hayo walikamatwa, na kwamba taratibu zinafanyika ili waweze kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria kujibu tuhuma zinazowakabili.
Akizungumza wakati wa kukabidhi rambirambi hizo, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha amesema walichelewa kutoa rambirambi hizo sababu ya uchunguzi ili kubaini kuwa mabaki yale kama yalikuwa ya ofisa huyo.
“Makamu wa Rais alipewa taarifa za uwepo wa tukio hilo alipofanya ziara yake Oktoba 11, 2024 alipokuwa kwenye ziara katika wilaya hii na akatoa ahadi ya kuleta rambirambi ya Sh5 milioni kwa familia yake,” amesema na kuongeza:
Ndugu wa marehemu, Juma Maduka amemshukuru Makamu wa Rais kwa rambirambi hiyo, huku akitoa wito kwa vyombo vya sheria kuwachukulia hatua za kisheria waliohusika na mauaji ya ndugu yao.
“Tunampongeza Makamu wa Rais kwa rambirambi hii kwenye familia yetu, kiukweli tunatambua ndugu yetu hawezi kurudi ila tunashukuru Serikali kwa faraja,’’ amesema Maduka.