Kamara kumpisha Sowah | Mwanaspoti

DIRISHA dogo la usajili linatarajiwa kufunguliwa Desemba 15, mwaka huu na Singida Black Stars imeanza kujiimarisha mapema, ikitajwa tayari imemalizana na mshambuliaji raia wa Ghana, Jonathan Sowah kutoka Al Nasr Benghazi ya Libya.

Timu hiyo inayonolewa na Kocha Patrick Aussems, taarifa zinabainisha ujio wa mshambuliaji huyo unakwenda kumuondoa kipa Mohamed Kamara aliyetua  mwanzoni mwa msimu akitokea Horoya ya Guinea.

Kamara, raia wa Sierra Leone, anaachwa kutokana na kukosa namba katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo mbele ya kipa mzawa Metacha Mnata.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Black Stars kimeliambia Mwanaspoti Sowah tayari amemalizana na timu hiyo na dirisha dogo litakapofunguliwa ataungana na timu tayari kwa ajili ya kuitumikia.

“Ni kweli mchezaji huyo tumemalizana naye na ni suala la muda tu kuungana na timu kwa ajili ya kuongeza nguvu eneo la ushambuliaji.

“Tumedhamiria kuhakikisha tunakuwa na kikosi bora ambacho kitatupa matokeo mazuri na msimu ujao kupata nafasi ya kuiwakilisha nchi kimataifa,” alisema mtoa taarifa huyo na kuongeza.

“Bado tunaendelea na mchakato wa usajili kwa ajili ya kuboresha timu, ni mapema sana kuweka wazi majina ya wachezaji tunaowahitaji lakini muda ukifika kila kitu kitakuwa wazi.”

Kabla ya kutua Singida Black Stars, iliwahi kuripotiwa Simba na Yanga zilijaribu kutupa ndoano zao kipindi cha dirisha dogo msimu uliopita kuiwania saini ya Sowah wakati akiichezea Medeama ya kwao Ghana, lakini akatimkia Libya kabla ya sasa kukubali kutua Tanzania kujiunga na Singida Black Stars.

Ndani ya Singida Black Stars, mshambuliaji Elvis Rupia ndiye anayetegemewa zaidi kikosini hapo huku Joseph Guede akiwa ni mbadala wake.

Hata hivyo, timu hiyo pia ilitangaza kumsajili Victorien Adebayor dirisha kubwa lakini hadi sasa hajaanza kucheza huku ikielezwa ataanza kuonekana dirisha dogo litakapofunguliwa kutokana na awali usajili wake haukuwa umekamilika.

Related Posts