MABAO mawili ya Simon Msuva na Feisal Salum katika kipindi cha kwanza yameipa Taifa Stars ushindi wa 2-0 dhidi ya Ethiopia, mchezo uliochezwa leo Novemba 16, 2024 kwenye Uwanja wa Pentecost Martyrs, Kinshasa nchini DR Congo.
Ushindi huu ni hatua muhimu kwa Stars katika harakati za kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 zitakazofanyika Morocco.
Msuva alifungua ukurasa wa mabao dakika ya 15 baada ya kupokea pasi nzuri kutoka kwa Novatus Dismas. Mashambulizi mfululizo ambayo Stars iliyafanya yalizaa matunda mapema na kuwapa Stars uongozi wa mapema katika mchezo.
Dakika ya 31, Feisal Salum aliongeza bao la pili na kuifanya Stars kwenda mapumziko kifua mbele. Licha ya Ethiopia kufanya mabadiliko kadhaa katika kipindi cha pili, Stars ilionekana kuwa bora.
Ushindi huo umeifanya Taifa Stars kufikisha pointi saba, ikiishusha Guinea yenye pointi sita na kupanda hadi nafasi ya pili katika Kundi H. Guinea itacheza baadaye saa 4 usiku dhidi ya DR Congo ambayo tayari imefuzu.
Kwa sasa, Stars inakabiliwa na mchezo mmoja nyumbani dhidi ya Guinea utakaopigwa Jumanne Novemba 19, 2024 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar. Ushindi katika mchezo huo wa mwisho wa hatua ya makundi utaihakikishia Stars nafasi ya kushiriki AFCON kwa mara ya nne katika historia yake.
Kocha wa Taifa Stars, Hemed Suleiman ‘Morocco’, alieleza furaha yake baada ya ushindi huo akisema: “Wachezaji wameonyesha moyo wa ushindani mkubwa. Ushindi huu ni motisha nzuri kuelekea mchezo wetu wa mwisho. Tutapambana kuhakikisha tunafanikisha ndoto ya Watanzania.”
Kwa upande wa Ethiopia, kocha wao, Mesay Teferi alikiri udhaifu wa kikosi chake, akisema walishindwa kuhimili kasi ya Stars katika kipindi cha kwanza, lakini aliwapongeza wachezaji wake kwa kuonyesha juhudi kubwa hasa katika kipindi cha pili cha mchezo.
Ushindi dhidi ya Guinea hautakuwa tu hatua ya kihistoria kwa Stars, bali pia utakuwa ishara ya maendeleo ya soka la Tanzania. Mashabiki sasa wanasubiri kwa hamu kuona kama ndoto ya kushiriki AFCON 2025 itatimia baada ya kushiriki mwaka 1980, 2019 na 2024 huku 2027 ikiwa ni zamu yetu kuandaa michuano hiyo sambamba na Kenya na Uganda.