Kilombero. Wakati uchaguzi wa serikali za mitaa ukitarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024, Jeshi la Polisi nchini limejipanga kuimarisha usalama na utulivu siku ya uchaguzi, ili wananchi washiriki katika upigaji kura ikiwa ni sehemu ya kutimiza haki yao ya kikatiba.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Jeshi hilo (IGP), Camilius Wambura alipokuwa katika hafla ya utoaji wa kamisheni kwa maofisa 1036 katika chuo cha maofisa wa Jeshi la Polisi Kidatu kilichopo katika Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro.
IGP Wambura amesema Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na majeshi mengine ya ulinzi na usalama, watahakikisha kuwa amani na utulivu unapatikana na kutamalaki muda wote kabla na baada ya uchaguzi.
“Mimi nikiwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, nawaomba wananchi mjitokeze katika kutimiza haki yenu ya kikatiba mkiwa na amani na utulivu, kisha mkaendelee na majukumu yenu ya kila siku. Tumejipanga vizuri sana kuhakikisha tunu hii ya amani tuliyoirithi itakuwepo na kuendelea katika vizazi vijavyo,” amesema IGP Wambura.
IGP Wambura amewakumbusha wahitimu wote katika kuhakikisha wanatambua umuhimu wa vyeo walivyovipata katika majukumu yao ya kila siku ikiwa ni pamoja na wao kwenda kuwa kiungo muhimu katika kusimamia nidhamu kati yao na askari wa chini yao.
“Napenda kuwakumbusha jambo moja muhimu, vyeo mlivyosomea ni dhamana na vinaongeza mzigo mkubwa kimajukumu katika mabega yenu na ni daraja na kiungo muhimu katika miundo ya majeshi yote duniani. Ni usimamizi wa nidhamu na ufuatiliaji wa kila siku wa shughuli zinazofanywa na askari walioko chini yenu,” amesema IGP Wambura.
Kaimu Mkuu wa Chuo cha Maofisa wa Jeshi la Polisi Kidatu, Goodluck Kessy mafunzo ya miezi miwili waliyoyatoa kuanzia Septemba 15, 2024 kuwa ni pamoja na utawala wa polisi, uongozi, usalama barabarani, jinsia, polisi jamii, sheria ya makosa ya jinai na huduma kwa mteja.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Wakili Dunstan Kyobya amewataka wahitimu wote wajiepushe na vitendo viovu na badala yake wawe chachu ya mabadiliko katika jeshi hilo.