Dar es Salaam. Wakati Serikali ikieleza kuwa inaendelea na uchunguzi kubaini chanzo cha kuporomoka kwa jengo la Kariakoo, fundi aliyekuwa akifanya ubomoaji ameeleza sababu na hali ilivyokuwa.
Jengo hilo liliporomoka mapema leo Jumamosi Novemba 16, 2024. Taarifa za awali kutoka kwa mashuhuda, zinaeleza ndani ya jengo hilo la kibiashara, kulikuwa na watu kadhaa waliokuwa wakifanya ununuzi katika maduka ya jengo hilo.
Tukio la kuanguka kwa jengo hilo linaelezwa na fundi ujenzi ambaye alipewa kazi ya kubomoa eneo la chini ya ghorofa akisema jengo hilo lilikuwa dhaifu.
Amesema wao ndio walipewa kazi ya kubomoa kuta za chini ndani ya jengo hilo lililoporomoka kwa lengo la mmiliki kuongeza eneo la kupanga wafanyabiashara.
Ushuhuda huo unatolewa na James Magnus mkazi Tandika akisema kazi hiyo walianza Novemba 14,2024 wakiwa watatu na kazi yao ilikuwa ni kubomoa kuta ndani ya ghorofa kwa chini.
Katika kazi hiyo ya ubomoaji amesema walikuwa watatu wakitumia nyundo za kugonga mawe, lakini katika kutekeleza shughuli hiyo walibaini kuta zilezile ndizo zilizokuwa na nguvu ya kushikilia jengo
“Tulikuwa tukigonga nyundo kwenye nguzo za chini udongo unashuka kwa sababu saruji iliyotumika ilikuwa hafifu,” amesema.
Magnus amesema wakati akifanya kazi hiyo leo ikiwa ni siku ya mwisho wakati wakiendelea na kazi, walianza kusikia sauti ndani ya jengo hilo kwa chini na ndipo alipiga kelele kuwashtua wenzake na kila mmoja alikimbilia eneo lake kuokoa uhai.
“Baada ya kuona zege linabomoka kwenye nondo niliwashtua wenzangu, jamani eeeh tunaondoka ndipo kila mtu akakimbilia eneo lake mimi nilitoka chini kuja juu, kulikuwa na watu wengine ndani ya jengo hilo,” amesema.
Magnus amesema kwa uzoefu wake jengo lile halikuwa na saruji ya kutosha wakati wa ujenzi, kwani nguzo zilizoshikilia jengo hilo kwa chini hazikuwa imara.
Amesema hata matofali ndani ya jengo hayakuwa imara
Magnus amesema baada ya kukimbilia nje ya jengo hilo alipata michubuko na ndipo akachukuliwa na mtoto wa mzee aliyewapa kazi na kuwapandisha bajaji na kuwapeleka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili akiwa na mwenzake.
Joseph Jerome, fundi mwingine amesema amepata majeraha ya miguu na mikono wakati akitoka ndani ya jengo hilo.
“Alhamisi ndio nilianza kazi ya ubomoaji mtaa wa Kariakoo, kazi hii nilipata baada ya kumaliza kazi ya kupakia nondo ndipo nikaambiwa kuna kazi ya kuvunja jengo kupanua kwa chini,” amesema.
Wakati alipotembelea eneo hilo la ajali, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema uchunguzi utafanyika kubaini sababu ya jengo hilo kuporomoka huku mafundi ujenzi wakieleza chanzo cha tukio.
“Kariakoo ni soko la kimataifa na tunategemewa na nchi zaidi ya nane … lile jengo lilikuwa la zamani sio jipya kwa nini limebomoka leo wataalamu wetu watatuambia,” amesema.
Amesema amezungumza na majeruhi waliolazwa hospitalini na wanaendelea vizuri huku akivitaka vyombo vya ulinzi kutumia taaluma zao vizuri kuokoa maisha ya wananchi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) Profesa Mohamed Janabi amesema majeruhi wote 40 wamefanyiwa kipimo cha Ultrasound kubaini kama kuna dalili zozote za damu kuvuja ndani ya mwili.
Katika Hospitali ya Muhimbili tangu asubuhi majeruhi 40 wamepokelewa, 33 tayari wameruhusiwa saba pekee wakiendelea na matibabu.