Mwanza. Mwakilishi wa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na Askofu wa Jimbo Katoliki la Bunda, Simon Masondole amewaonya madaktari wanaowashawishi wanawake kutoa mimba akiwaambia wao ni chombo cha Mungu cha kuokoa uhai.
Akizungumza leo Jumamosi Novemba 16, 2024 kwenye misa takatifu ya mahafali ya 17 ya Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Sayansi za afya na Tiba Shirikishi (Cuhas), Askofu Masondole amesema baadhi ya madaktari wamekuwa wakishawishi wajawazito kutoa mimba badala ya kutetea uhai.
“Leo hii sisi tunaweza kutetea uhai kwa namna hiyo? Tupo tayari madaktari? Madaktari wangapi tunahusika kuwashawishi wagonjwa kwa nguvu ili watoe mimba wanawake wanapokuja? Wewe ndio unafanya hiyo kazi ya kushawishi ili umtolee mimba…wewe uko hapa ili utetee uhai, usisahau hilo,” amesema.
Askofu huyo aliyewatunuku stashahada na shahada wahitimu 869 katika fani mbalimbali za afya, ameongeza kuwa iwapo madaktari watasahau jukumu lao hilo watakwisha kwa kuwa hata sheria ya nchi hairuhusu.
“Usipoteze mwelekeo daktari na nesi…kwahiyo tuwe wahudumu wazuri na Mungu atatueleza namna ya kutibu,”amesema
Ameongaeza: “Mnapokuwa madaktari muwe madaktari safi msikubali kuchafuliwa na ulimwengu mkajiingiza katika tiba za ajabu kinyume na maadili na maelekezo na ustawi wa tiba. Muwe madaktari watakatifu ambao watu watajisikia huru na raha kukukimbilia…nanyi oneni wagonjwa wanaokuja ni mfano wa yatima na wajane.”
Katika hatua nyingine, Askofu Masondole amesema sekta ya afya ambayo wataihudumu, ni huduma ambayo ina maadui wengi katika jitihada za kutafuta dawa, kutafuta ustawi wa mwanadamu, kutafuta mtu awe salama au mwenye furaha ambayo ni wito wa daktari.
“Maadui pia wako pale…upotoshaji katika huduma hii ni mwingi mno, kuna watu wamevamia tena kuna mchanganyiko wa vitu mbalimbali na tiba ambazo pengine tukizitumia vizuri italeta umoja na ukamilifu katika tiba,’’ amesema.
Amesema katika fani hiyo pia kuna mgawanyiko wa madaktari wakweli ambao wanatibu vizuri na kumuweka Mungu mbele na wavamizi ambao wamejiweka kama mamluki kwa ajili ya kuharibu kazi hiyo nzuri.
“Tunataka muwe wacha Mungu kwa sababu kumtumikia Bwana ni kuchukia uovu…katika ubobevu wako wote, wewe ni chombo cha Mungu, jitambue kwamba Mungu anakutumia mwanadamu hana nguvu, tunapambana katika tiba, tunapambana na magonjwa na zaidi tunapambana na kifo.
Askofu wa Jimbo Katoliki la Rulenge – Ngara na Mwenyekiti wa Baraza la Chuo cha Cuhas, Askofu Severin Niwemugizi amewataka wahitimu hao wa kada za afya, kutumia maarifa na ujuzi, walioupata kujenga jamii yenye afya bora na kupeleka faraja kwa wanaoenda kwao kupata huduma mbalimbali za afya.
“Tunategemea msiuache uadilifu, bali mkautumie zaidi huko mwendako. Mjijengee sifa nzuri na kuwa mabalozi wazuri wa chuo chenu na taaluma zenu…muwe tayari kwenda kutoa huduma, bila kujali hadhi ya mnaowahudumia. Hii ndiyo sadaka ya kumpendeza Mungu,” amesema.
Naye, Makamu Mkuu wa Cuhas, Profesa Erasmus Kamugisha amewataka wahitimu hao kuzingatia maadili, uadilifu na weledi watakapojiajiri au kuajiriwa ili wasiiaibishe taaluma ya afya.
“Msiende kuishi na kutenda matendo ambayo hatukuwafundisha, mkaishia kuziaibisha taaluma za afya huko kwenye jamii. Jamii ikiona msomi amefanya sivyo ndivyo, wao hudhani ni taaluma yake na si vinginevyo,” amesema.
Mhitimu wa shahada ya uzamili wa afya ya jamii, Dk Sebastian Pima amesema elimu waliyoipata wanaenda kuitumia kutatua changamoto za afya ambazo wananchi wanakumbana nazo na kuwa watatumia taaluma hiyo kwa manufaa ya jamii.
Katika mahafali hayo, wahitimu wamemaliza mafunzo yao katika programu 14, kati ya 15 zinazofundishwa chuoni hapo ikiwemo ya udaktari, radiografia, maabara tiba, ufamasia, uuguzi, sayansi na ufundi maabara wa tiba, sayansi za uchunguzi na tiba kwa mionzi na uchunguzi wa vinasaba ambao walikula viapo vya maadili kabla ya kutunukiwa shahada.