Fundi mchundo adai jengo la Kariakoo lilikuwa dhaifu

Dar es Salaam. Wakati Serikali ikieleza kuwa inaendelea na uchunguzi kubaini chanzo cha kuporomoka kwa jengo la Kariakoo, fundi aliyekuwa akifanya ubomoaji, amedai miongoni mwa sababu ni udhaifu wa jengo hilo.

Jengo hilo liliporomoka mapema leo Jumamosi Novemba 16, 2024. Taarifa za awali kutoka kwa mashuhuda, zinaeleza ndani ya jengo hilo la kibiashara, kulikuwa na watu kadhaa waliokuwa wakifanya ununuzi katika maduka ya jengo hilo.

Tukio la kuanguka kwa jengo hilo limeelezwa na fundi ujenzi ambaye alipewa kazi ya kubomoa eneo la chini ya ghorofa, aliyedai jengo hilo lilikuwa dhaifu.

Fundi huyo James Magnus, ambaye hata hivyo hatambuliwi na Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) amedai wao ndio walipewa kazi ya kubomoa kuta za chini ndani ya jengo hilo lililoporomoka kwa lengo la kuongeza eneo la kupanga wafanyabiashara.

Amedai kazi hiyo waliianza Novemba 14, 2024 wakiwa watatu na kazi yao ilikuwa ni kubomoa kuta ndani ya ghorofa kwa chini.

Katika kazi hiyo ya ubomoaji, amedai walikuwa wakitumia nyundo za kugonga mawe, lakini katika kutekeleza shughuli hiyo walibaini kuta zilezile walizokuwa wakibomoa ndizo zilizokuwa na nguvu ya kushikilia jengo.

Wakati alipotembelea eneo hilo la ajali, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema uchunguzi utafanyika kubaini sababu ya jengo hilo  kuporomoka huku mafundi ujenzi wakieleza chanzo cha tukio.

“Kariakoo ni soko la kimataifa na tunategemewa na nchi zaidi ya nane … lile jengo lilikuwa la zamani sio jipya kwa nini limebomoka leo wataalamu wetu watatuambia,” amesema.

Amesema amezungumza na majeruhi waliolazwa hospitalini na wanaendelea vizuri huku akivitaka vyombo vya ulinzi kutumia taaluma zao vizuri kuokoa maisha ya wananchi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) Profesa Mohamed Janabi amesema majeruhi wote 40 wamefanyiwa kipimo cha Ultrasound kubaini kama kuna dalili zozote za damu kuvuja ndani ya mwili.

Katika Hospitali ya Muhimbili tangu asubuhi majeruhi 40 wamepokelewa, 33 tayari wameruhusiwa saba pekee wakiendelea na matibabu.

Related Posts