Mahakama ilivyohitimisha shauri la umri wa kugombea uongozi

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Kuu Dodoma imetupilia mbali shauri la maombi ya ridhaa ya kufungua shauri la mapitio kupinga kanuni za uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2024, kwa kuwanyima haki ya kugombea watu wenye umri chini ya miaka 21.

Uamuzi wa kutupilia mbali shauri hilo umetolewa na Jaji Abdi Kagomba kufuatia pingamizi la awali lililowekwa na Serikali kupitia Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) dhidi ya shauri hilo, baada ya kukubaliana na hoja za pingamizi hilo.

Shauri hilo la maombi mchanganyiko namba 26314/2024 lilikuwa limefunguliwa na wakili mwandamizi wa kujitegemea, rais mstaafu wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) John Seka, dhidi ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na AG.

Katika uamuzi huo uliotolewa Novemba 4, 2024, ambao Mwananchi limepata nakala yake jana Ijumaa, Jaji Kagomba amekubaliana na hoja za pingamizi la Serikali kuwa wakili Seka hakuweza kuonesha namna yeye binafsi alivyoathirika  na masharti ya kanuni hizo.

Wakili Seka alikuwa akiomba kibali kufungua shauri la maombi ya mapitio ya mahakama kupinga kanuni hizo za mwaka 2024, zilizotungwa na Waziri wa Tamisemi kwa ajili ya kusimamia mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024.

Kanuni hizo ni kanuni za uchaguzi wa mwenyekiti wa kijiji, wajumbe wa halmashauri ya kijiji na mwenyekiti wa kitongoji katika mamlaka za wilaya, Tangazo la Serikali (GN) namba 571 la mwaka 2024.

Nyingine ni kanuni za uchaguzi wa mwenyekiti wa kitongoji katika mamlaka za miji midogo, GN namba 572/2024 na kanuni za uchaguzi wa mwenyekiti wa kijiji, wajumbe wa halmashauri ya kijiji na mwenyekiti wa kitongoji katika mamlaka za miji, GN namba 573/2024.

Kanuni nyingine ni kanuni za uchaguzi wa mwenyekiti wa mtaa na wajumbe wa kamati ya mtaa katika mamlaka za miji, GN namba 574/2024.

Wakili Seka alikuwa anadai kuwa kanuni hizo zinawanyima watu wenye umri wa kati ya miaka 19 na 21, haki ya kugombea nafasi ya kuchaguliwa katika uchaguzi huo.

Hivyo Wakili Seka aliiomba mahakama hiyo itamke na kuamuru kuwa raia wenye umri kati ya miaka 18 na 21,  wana haki ya kushiriki kugombea nafasi ya kuchaguliwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa  uliopangwa kufanyika Novemba 27, 2024,

Pia aliomba itamke kuwa kanuni namba 15[b] GN 571;  14[b] GN 572 ; 15[b] GN 573 na 15[b] GN 574 zote za mwaka 2024,  ziko kinyume na Katiba na ni batili kwa  kukiuka masharti ya Ibara namba 22[2], 13[1]; 13[2]; 13[4]; 26[1]; 26[2]; 21[1]; 22[2]; 29[1] na  29[2] za Katiba ya Tanzania.

Kisha aliiomba mahakama imuamuru na kumwelekeza Waziri wa Tamisemi kuwezesha raia watu wazima wenye umri kati ya miaka 18 na 21 kushiriki kikamilifu kama wagombea katika uchaguzi huo, ikiwemo mchakato wa uteuzi ili kuwapa nafasi waathirika wa kanuni hizo.

Hata hivyo, wajibu maombi mbali na kuwasilisha kiapo kinzani kujibu madai ya mwombaji, pia waliwasilisha pingamizi la awali, wakiomba shauri hilo lisipewe nafasi ya kusikilizwa bali litupiliwe mbali wakitoa sababu mbili.

Mahakama katika uamuzi wake imezingatia sababu moja tu ya pingamizi kuwa shauri hilo linakiuka masharti ya kifungu cha 4(2) cha Sheria ya Utekelezaji Wajibu na Haki za Msingi (Bradea) sura ya 3 na marekebisho yake.

Pingamizi hilo lilisikilizwa Oktoba 31 2024 ambapo wajibu maombi waliwakilishwa na jopo la mawakili wa Serikali watatu lililoongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Hangi Chang’a huku mwombaji, Wakili Seka akijiwakilisha mwenyewe.

Jaji Kagomba baada ya kusikiliza hoja za pande zote na kupitia sheria husika, Katiba na mashauri rejea katika uamuzi wake, amesema kuwa anakubaliana na hoja hiyo ya pingamizi la Serikali kuwa shauri hili halistahili kusikilizwa kwa kuwa limekiuka masharti ya kifungu cha 4(2) cha sheria hiyo ya Bradea.

Amesema kuwa ingawa Ibara ya 30(4) ya Katiba inaipa Mahakama Kuu mamlaka ya kusikiliza shauri lolote, lakini pia kwa kuzingatia sheria nyingine zilizowekwa.

Kwa mujibu wa ibara hiyo, sheria hizo ni kwa ajili ya kusimamia utaratibu wa kufungua mashauri, kwa mujibu wa ibara hiyo;  kufafanua uwezo wa Mahakama Kuu katika kusikiliza mashauri yaliyofunguliwa chini ya ibara hiyo na kuhakikisha utekelezaji bora wa madaraka ya Mahakama Kuu.

Amesema kuwa hakuna ubishi kuwa Wakili Seka anatafuta kutekeleza haki chini ya Ibara za 12 mpaka 29 za Katiba na kwamba sheria pekee rasmi inayosimamia mashauri hayo ni Bradea na kanuni zake.

“Vilevile hata Ibara ya 26(2) ya Katiba ambayo shauri hilo limefunguliwa chini yake, inamtaka mwombaji kufuata taratibu zilizowekwa na sheria katika kuchukua hatua za kulinda na kuhifadhi Katiba”, amesema Jaji Kagomba na kusisitiza:

“Taratibu hizo si nyingine zaidi ya zilizotungwa chini ya Sheria ya Bradea na kanuni zake zikiwemo kuwasilisha kiapo kinachomtaka mdai kuonesha namna gani binafsi ameathirika na kanuni anazotafuta ridhaa ya kuzipinga.”

Hvyo Jaji Kagomba amesema kuwa Wakili Seka alipaswa kuwasilisha kiapo kuwa yuko katika kundi la umri wa wanaonyimwa haki ya kugombea kati ya miaka 18 na 21, ili kukidhi matakwa ya kifungu cha 4(2) cha Sheria ya Bradea.

Hata hivyo,  Jaji Kagomba amesema kuwa katika mazingira maalumu mtu anayefungua shauri kwa ukiukwaji wa Katiba usiohusiana na maslahi yake binafsi bali kwa maslahi ya umma kama vile kulinda haki za makundi ya watu wasiojiweza wasioweza kutetea haki zao.

Amesema mtu wa namna huyo anaweza kufungua shauri chini ya Ibara ya 26(2) bila kuwajibika kuzingatia masharti ya kifungu cha 4(2) cha Sheria ya Bradea, kuonesha namna yeye binafsi alivyoathirika na ukiukwaji huo wa masharti ya Katiba.

“Kwa kuzingatia mjadala huo hapo juu ninaona kuwa sababu ya kwanza ya pingamizi la awali ina mashiko. Kwa hakika shauri hili halina ustahilifu kwa kutozingatia masharti ya kifungu cha 4(2) cha Bradea. Mwisho wake kinatupiliwa mbali”, amesema Jaji Kagomba.

Wakati pingamizi hilo liliposikilizwa, Wakili wa Serikali Mwandamizi Jacqueline Kinyasi alidai kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 4(2) cha Bradea, mwombaji alipaswa kuonesha katika kiapo kuwa yuko katika kundi la umri ulioathirika, lakini hakufanya hivyo.

Akijibu hoja hiyo, Wakili Seka alidai kuwa Mahakama ya Rufani katika kesi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali dhidi ya Jeremiah Mtobesya (Wakili wa kujitegemea), rufaa ya madai namba 65 ya mwaka 2016, suala la haki ya kisheria haliwezi kuibuka kwa shauri lililofunguliwa chini ya Ibara ya 26(2) ya Katiba kama ilivyo kwa shauri hilo.

Related Posts