‘Nizalie nitakuoa’ neno lililozima ndoto za wengi

Dar es Salaam. Unaweza kujiona mwenye kismati na bahati ya kipekee katika dunia hii yenye wanawake zaidi ya bilioni 4, kwa wewe kuambiwa neno ‘nizalie nitakuoa’ na mwanamume unayempenda.

Neno hili huja na sura ya unyenyekevu na upole, huku nia mbaya ikijificha kwenye kivuli cha upendo na mapenzi ya dhati. Maswali binafsi kama kwa nini ndoa hii ije na masharti anayopaswa kujiuliza binti huyu, siku zote hufichwa kwenye msemo wa Kiswahili wa ‘mapenzi ni upofu.’

Upofu huu umeathiri mabinti wengi mijini na vijijini, wakubwa kwa wadogo, huku kauli ‘nizalie nitakuoa’ ikizima ndoto zao.

Ni maneno mawili yenye nguvu ya ulaghai ambayo yamechangia kupunguza idadi ya wasomi wa kike nchini na kusababisha maisha magumu kwa wengi, huku athari kubwa zikimkumba mwanamke.

Matumizi ya lugha ya ulaghai yamegeuka kuwa njia rahisi ya kuwarubuni mabinti na matokeo yake, yamesababisha wengi wao kukatiza masomo yao na wengine kutotaka kusoma kabisa.

Na baadhi ya watu wanasema maneno hayo mawili yamesababisha migogoro kwenye baadhi ya familia kwa kuleta machozi, kukatisha masomo na kuwa mwanzo wa safari ngumu ya maisha magumu kwa baadhi ya wasichana wengi.

Bibiana Bayo, binti wa miaka 23, alijikuta akiachana na ndoto zake akiwa na miaka 16, baada ya kupumbazwa na maneno hayo. Akizungumza na Mwananchi akiwa katika Kijiji cha Dongobesh mkoani Manyara, Bayo anasimulia safari ya maisha yake iliyojaa changamoto na mikasa.

Anasema umbali kutoka nyumbani kwao hadi shuleni ni takriban kilomita 20, hali iliyomfanya kupanga chumba na kutumia siku za mwisho wa wiki kufuata mahitaji nyumbani.

Anasema alikuwa akikodisha baiskeli kutoka kwa muuza duka lililokuwa jirani na ghetto alilokuwa amepanga, kusudi aende mara moja nyumbani na arejee mapema.

Muda ulivyozidi kwenda, Bayo anasema yule kijana muuza duka alianza kujenga mazoea naye na akafikia hatua ya kumuuliza huwa anafuata mahitaji gani nyumbani kwao ambayo yeye angeshindwa kumpatia.

“Basi nilipomueleza akaanza kunipa matumizi ambayo hata nyumbani sikuwa nikiyapata na hatimae tukawa wapenzi,” anasimulia Bayo.

Bayo anasema yule kijana alimuahidi kumlinda akipata ujauzito, huku akimuahidi kumuoa kama ikitokea.

Bila uelewa wa masuala ya ujauzito, Bayo anasema kuna siku alikutana kimwili na muuza duka huyo, lakini aliingiwa na woga ghafla akahisi huenda ana ujauzito, baada ya siku kadha kupita akaamua kwenda hospitali kuthibitisha kama kweli.

“Sikuwa najua chochote kuhusu kupata ujauzito wala kuhesabu siku zangu, nakumbuka kila baada ya tendo nilikuwa nakimbilia hospitali kupima ujauzito,” anasimulia Bayo, mtoto pekee katika familia yao.

Hata hivyo, anasema jibu pendwa na lililokuwa linampa furaha na faraja wakati wote ni pale anapofanyiwa vipimo na kujibiwa kuwa hana ujauzito.

 Anasema ilifikia wakati majirani na wanafunzi wenzake walianza kumuona ni wa tofauti baada ya habari kusambaa kwamba ana ujauzito.

“Ilibidi nimshirikishe mwenzangu kuhusu kupima ujauzito, alishauri tukahakikishe hospitali ili tupate uhakika, baada ya vipimo majibu yalithibitisha kuwa nina ujauzito wa miezi minne,” anasema Bayo.

Anasema majibu yale yalimuumiza sana na alishikwa na woga, huku akifikiria ugumu wa maisha ya nyumbani kwao na pia akihofia hasira za wazazi wake.

Lakini anasema kwa upande wa kijana yule muuza duka, alipobaini hali hiyo, akaanza kumshawishi atoe ujauzito ule.

“Nilimkatalia nikihofia madhara ya kimila yanayohusishwa na utoaji mimba katika jamii yetu,” anasimulia Bayo.

Hivyo anasema aliamua kumweleza baba yake kuhusu ujauzito wake. “Baba alilia sana, akaniuliza kwa nini nimeamua kufanya hivyo wakati nilikuwa tegemeo lake,” anasimulia binti huyo.

Lakini kwa kuwa alikuwa na ahadi ya yule kijana kwamba akipata mimba atamuoa, anasema alimweleza baba yake juu ya mipango ya kuolewa akiwa na ujauzito.

Lakini anasema hali haikwenda kama alivyoaminishwa, hivyo baba yake naye alivyoona kimya cha muda mrefu, alikasirika na akamtaka amlete mchumba huyo baada ya siku tatu lakini hakufika.

Hata hivyo anasema baada ya majadiliano marefu na baba yake, akaamua kumpeleka kwa mama yake mdogo anayeishi Arusha.

Alipofika akamwambia asikubali kuolewe bali arudi shule akatimize ndoto yake.

“Wakati mama anasema hayo, baba alisema ndani ya siku nne napaswa kuolewa na mwanamume yeyote mwenye uwezo wa kutoa mahari aliyotaka baba. Nikaamua kutoroka kwenda kwa mjomba, nikamweleza ukweli, akanipokea,” anasimulia.

Hata hivyo, anasema baba yake alimfuata tena kwa mjomba wake siku hiyo hiyo jioni akiwa na hasira na alikuwa anataka kumpiga, lakini mjombaake alimnusuru.

“Siku moja baba alifika akiwa na kijana ambaye tayari alikuwa ametoa mahari na alikuja kwa lengo la kunichukua, lakini nilikataa. Siku iliyofuata nikajifungua,” anasema binti huyo.

Anasema licha ya kujifungua salama, baba yake alimgeuzia kibao mama yake kwamba alikuwa anajua mpango mzima wa yeye kupata ujauzito.

“Kuna siku alimsema sana mama na akampiga mpaka akamvunja kidole,” anasema Bayo.

Anasema baada ya mtoto wake kufikisha mwaka mmoja na miezi minne, alianza mchakato wa kutafuta shule ili kurejea masomoni.

“Nilianza kutafuta shule ili mama mdogo anisomeshe, lakini kwa bahati mbaya mama mdogo alifariki dunia kabla hata sijapata shule, hii iliniumiza sana, nikabaki sijui cha kufanya, nikawa na maswali mengi kichwani kwamba nitarudije shuleni na nani atanisomesha,” anasema.

Anasema baadaye alikumbuka ahadi ya baba mtoto wake kuwa asiwe na hofu, akipata mimba atamuoa na atamsomesha mtoto akishakua. Hivyo alimkumbusha juu ya ahadi hiyo, lakini akamjibu kwamba akimzalia mtoto wa pili, ndiyo atamsomesha.

Bayo anasema kwa kuwa alimuamini, akabeba ujauzito wa pili kwa sharti la mpenzi huyo ataenda kutoa mahari kabla ya kumzalia mtoto huyo.

“Nilikuwa na ujauzito wa pili, lakini nikiwa mjamzito nikaona dalili za kutotimizwa kwa ahadi ya kunirudisha shuleni, kwa sababu ilikuwa kila nikimkumbusha ananitupia maneno makali ya kukatisha tamaa,” anasema Bayo.

Anasema alipoona hakuna dalili, mwaka 2022 aliamua kujiingiza kwenye siasa na kwa kuwa ulikuwa ni mwaka wa uchaguzi, aliomba kugombea nafasi ya ukatibu kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), akilenga kama angefanikiwa angepata fedha za kujikimu na watoto wake.

“Nilishinda nikawa napata fedha, hizo ziliniwezesha kukodi pia shamba ambalo nililima nikapata mahindi ya kutosha,” anasimulia.

Ng’ombe wa masikini hazai

Pamoja na jitihada zote alizozifanya Bayo, mwisho wa siku anasema baada ya kuvuna mahindi yake, mume wake alivizia muda aliokuwa ameenda kanisani, aliyachukua yote na kwenda kuyauza na hakumpatia hata senti moja.

“Nilijaribu kuhoji kwa nini amefanya hivyo, nikaambulia kipigo,” anasema.

Anasema hakukata tamaa, anasema kuna siku akiwa kwenye shughuli zake za kichama, aliona tangazo la elimu ya bure kwa watoto wa kike waliopitia changamoto na kushindwa kumaliza kuhitimu masomo yao.

“Nililifuatilia tangazo hilo na kupiga simu shuleni, nilipata maelekezo na nikaambiwa niripoti shuleni hapo Januari, 2023 tayari kwa kuanza masomo, nilifanikiwa kupata mahitaji kiasi na sasa nipo hapa nasoma, kama mtahiniwa wa kujitegemea,” anasema Bayo.

Anasema hivi sasa yuko kidato cha tatu na nne na sasa anafanya mtihani wa Taifa wa kidato cha nne.

Aidha, neno ‘nizalie nitakuoa’ kwa mara nyingine likachukua ndoto za Antonita James (19), mkazi wa Dongobesh mkoani Manyara, aliyeshindwa kuendelea na masomo akiwa na miaka 17 tu wakati huo.

“Niliahidiwa kuolewa endapo nitamzalia, ila nilipoupata, alinikana na sasa ninalea mtoto kwa kusaidiwa msaada mdogo kutoka kwa wazazi wangu, sina wa kunisomesha tena, wote wanaamini nilichezea pesa za wazazi wangu,” anaanza kusimulia binti huyo.

‘Nizalie nitakuoa’ linazima pia ndoto ya msichana Selina Sumawe (21), mkazi wa Dongobesh Manyara, aliyekuwa na ndoto ya udaktari ambayo ilitokomezwa akiwa na miaka 26 tu.

“Nilishawishiwa kwa kupewa matumizi madogomadogo na kuahidiwa endapo nitamzalia huyo mwanamume angenipa vitu vingi, ila tangu alipobaini kuwa nilikuwa na ujauzito, sikuwahi kumuona, wala mtoto hamfahamu baba yake mpaka sasa,” anasema Sumawe.

Vijana wa kiume wanasemaje

Hivi ni visa mkasa vinavyoendelea huko mtaani na baadhi ya vijana wa kiume waliozungumza na Mwananchi, wameeleza sababu za wao kutumia neno hilo la ‘nizale nitakuoa’, lakini kumbe wanaharibu ndoto za vijana wenzao wa kike.

“Ndoa siku hizi ni adimu, wasichana wengi wanawaza kuolewa kama njia bora ya yeye kupata mteremko wa kuhudumiwa, ndiyo maana neno hilo linawatesa,” anasema Twalib Juma (28).

Twalib, ambaye hivi sasa ni baba wa watoto wawili aliowapata kutokana na kauli hiyo ya nizalie nitakuoa, anasema alipovutiwa na mama wa mtoto wake wa kwanza kipindi hicho akiwa binti wa miaka 18, alimfuata na kumpa ahadi ya ndoa.

“Kipindi hicho mama Zaina alikua kidato cha nne, nilipomfuata kwa mara ya kwanza alinikataa na kudai anataka mtu wa kumuoa tu na si kumpotezea muda,” anasimulia Twalib.

Anasema kauli ile ilimfanya atoe ahadi hiyo ambayo hakuwa na uwezo nayo wa kuitimiza, bali alitaka tu kumpata binti huyo.

“Nilikuwa na miaka 25 na ili niwe naye ilibidi nidanganye, alipopata ujauzito aliniambia nikajitambulishe kwao, kitu ambacho sikuwa tayari kwa kweli,” anasema Juma.

Anasema na kupoteza ushahidi kabisa, aliamua kutoroka eneo hilo na kwenda kujificha mbali, akikwepa mkono wa sheria kwa sababu alikuwa kampatia ujauzito mwanafunzi.

Anasema alirejea baada ya binti huyo kujifungua baada ya kubaini kwamba hakuna kesi.

 Kijana John Peter (30) naye anakiri kutumia kauli hiyo kwa lengo tu la kumpata binti mwanafunzi aliyekuwa akimtongoza, lakini alikuwa anakataa akihofia ujauzito na malezi ya mtoto akijifungua.

“Ni ngumu sana kukataliwa unapotanguliza kauli hii yenye ahadi hewa ya ndoa, lakini pia, hutatumia nguvu kubwa kumpata umtakaye, japo wapo wachache sana wanaoshinda kauli hii,” anasema Peter.

Sababu za wengi kuangukia huku

Akizungumzia kadhia hiyo, Mwanasaikolojia Happy Haule anasema mabinti wengi wananaswa kwenye mtego wa kauli hiyo kutokana na msukumo wa kifamilia.

“Wazazi wengi nao huwataka watoto wao waolewe mara tu wanapomaliza chuo au wanapofikisha umri fulani, huku maswali kama lini unaleta mchumba yakigeuka na kuwa kero kwa mabinti zao,” anasema Haule.

Anasema sasa kauli hizo huwakera sana mabinti ndiyo maana humkubalia mwanamume yeyote anayemtamkia kauli hiyo bila kuwaza mara mbili.

“Hali nyingine inayomfanya msichana kuhisi anachelewa ni kuona marafiki zake wa karibu wakiingia kwenye ndoa,” anasema.

Pia, hali ngumu ya kiuchumi humfanya msichana kukubali mahusiano yoyote, hata kama anajua mtu huyo si sahihi kwake.

Aidha, Haule amewashauri wazazi na walezi kutambua kuwa nyakati zimebadilika, hivyo wanapaswa kupunguza maswali ya aina hiyo kwa mabinti zao.

Related Posts