Wasaidizi wa nyumbani, maarufu kama ‘house girl’ ni watoto au vijana wadogo waliokulia katika mazingira ya kawaida, hasa ya kijijini.
Mabinti hawa huajiriwa na wazazi kwa lengo la kuwasaidia kumuangalia na kumtunza mtoto wakati wao wakiwa kazini.
Sambamba na malezi, wasaidiz hawa husaidia pia kufanya kazi za ndani kama vile usafi, kutunza nyumba na majukumu mengine kadiri yanavyojitokeza.
Kwa kawaida walezi hawa hupatikana kwa utaratibu usio rasmi unaotegemea mfumo wa kufahamiana na ndugu, jamaa na marafiki. Ndugu hawa wanaweza kuwaunganisha wazazi wanaomhitaji msichana anayetafuta kazi hizo za ndani.
Hakuna utaratibu rasmi unaowawezesha waajiri wenye uhitaji kuwa na uhakika na historia yake, ujuzi na tabia zake kwa jumla.
Hata hivyo, kwa kubahatisha inawezekana wazazi wakampata kupitia watu wanaofahamika.
Kwa jumla, msichana wa kazi ndiye mtu anayetumia muda mwingi kukaa na mtoto kuliko mtu mwingine yeyote kwenye familia.
Ndiye anayefahamiana na mtoto kwa karibu zaidi kwa sababu ndiye anayehakikisha mtoto anapata chakula na huduma nyingine za muhimu wakati wazazi wakiwa kazini.
Kwa upande mwingine, yamekuwepo matukio ya akina dada hawa kudaiwa kuwafundisha watoto tabia zisizofaa.
Matukio haya wakati mwingine hutokea katika mazingira ambayo binti mwenyewe hajui namna nyingine bora zaidi ya kukaa na mtoto.
Hata hivyo, wakati mwingine, huwa ni matokeo ya visasi wanapojisikia hawatendewi haki na waajiri wao.
Kwa mfano, mara nyingi, wasichana hawa huajiriwa bila mikataba. Malipo yao hayalingani na kazi nyingi wanazozifanya.
Wengi wao huwa wa kwanza kuamka na wa mwisho kulala. Hali ya kutokuridhika na mazingira ya kazi huongeza uwezekano wa vitendo visivyotarajiwa.
Kwa kuwa hakuna mzazi angependa nia njema ya kumtafuta msichana wa kazi ilete matatizo, tunapendekeza hatua nne za kuchukua katika kuboresha huduma za malezi kupitia akina dada hawa ambazo, kwa hakika, zinahitajika kwa wazazi wengi.
Wapo wasichana wanaotoka kwenye familia zilizokuwa na migogoro. Mazingira kama haya huwafanya wawe wepesi kugombana, kukwazwa hata kuwa tayari kuwaumiza wengine. Pia wapo wanaotoka kwenye familia zenye imani za kishirikina.
Fanya jitihada za kumfahamu kabla hujafanya maamuzi. Huwezi kumfahamu mtu kirahisi, lakini ni vyema kujua ametoka wapi, aliishi vipi na familia yake, misimamo yake na mambo mengine ya msingi. Ili hayo yawezekane, ni vizuri ukampata kupitia watu wanaomfahamu vizuri.
Muelimishe ajue wajibu wake
Mitafuruku mingi kati ya waajiri na hawa mabinti wakati mwingine inachangiwa na kutokufahamu majukumu yao ipasavyo.
Waajiri wengi huwa na matarajio makubwa kwa akina dada hawa, ingawa hawawasaidii kujua kile wanachopaswa kukifanya.
Ni vyema mara baada ya kufanya makubaliano naye, hakikisha anajua utaratibu kamili wa kazi. Afahamu anaamka saa ngapi, anatakiwa kufanya kipi siku nzima na kipi hapaswi kukifanya. Ukifanya hivyo unapunguza uwezekano wa makosa ya kutokujua jambo sahihi la kufanya.
Mfanye binti wa kazi awe sehemu ya familia yako. Mfanye ajisikie kupendwa kama mwanafamilia mwingine.
Mtu anayependwa huchangamka moyo na hivyo kuwa na hamasa ya kujituma. Sambamba na hilo, epuka mahusiano yasiyo ya kimaadili na msichana wa kazi.
Makosa kama hayo hujenga mazingira ya kudharaulika. Ukidharaulika, ni rahisi mwanao kuwa mhanga.
Aidha, mtengenezee mazingira bora ya kazi. Kwa mfano, unaweza kufikiria kumtengenezea utaratibu wa kujiendeleza kitaaluma.
Hakikisha unaonesha kutambua kazi anazozifanya. Kutambuliwa ni hitaji la msingi kwa kila mwanadamu. Kutambuliwa kunamjengea ari ya kujituma.
Onesha kwa vitendo namna unavyotarajia mtoto ahudumiwe. Binti atajifunza kwa vitendo. Unapopata muda fanya kazi za ndani kama unavyotarajia afanye yeye.
Pika, tenga chakula, fua nguo ili kuonesha kuwa unaishi matarajio yako. Unapofanya hivyo, binti atajifunza.
Kadhalika, tambua kuwa upo uwezekano wa mwanao kujifunza tabia usizozitarajia. Unaporudi nyumbani jua maendeleo ya mwanao kitabia.