NABI: Mtafurahi! Ataja mambo matano kocha mpya Yanga SC, atuma salamu

MASHABIKI wa Yanga wanasubiri kuiona timu yao ikianza maisha mapya bila ya Miguel Gamondi ambaye ndoa yake na klabu hiyo ilisitishwa juzi, Ijumaa.

Wakati Gamondi anaondoka, Yanga imemtambulisha Sead Ramovic kuwa mrithi wake huku matarajio yakiwa ni kuendeleza kile ambacho kimefanywa na mtangulizi wake.

Sasa wakati kukiwa na mashaka kidogo kwa baadhi ya mashabiki wa Yanga huku wale wapinzani wao nao wakitoa maneno ya kejeli juu ya kocha huyo mpya raia wa Ujerumani kwamba hamna kitu, lakini wameambiwa jambo la kuwatuliza na kocha wao wa zamani, Nasredine Nabi.

Nabi ambaye aliinoa Yanga kuanzia Aprili 2021 hadi Juni 2023 na kumuachia kijiti Gamondi, amewatoa hofu mashabiki wa Yanga kwa kuwaambia: “Mtafurahi, Yanga imepata bonge la kocha.”

Kocha huyo Mtunisia ambaye alishinda mataji mawili ya Ligi Kuu Bara kipindi anainoa Yanga huku akiiwezesha timu hiyo kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2022/2023, amesema anamfahamu vizuri Ramovic, hivyo hakuna haja ya kuwa na hofu naye.

Akizungumza na Mwanaspoti kwa njia ya simu kutoka Afrika Kusini anakoifundisha Kaizer Chiefs, Nabi alisema Ramovic ni kocha mzuri ambaye anafundisha soka la kisasa.

Nabi ambaye aliiacha Yanga akiwa ameweka rekodi za kibabe ikiwemo ya kucheza mechi 49 za ligi bila ya kupoteza, alisema viongozi wa Yanga wamefanya maamuzi sahihi ya kumchukua Ramovic ambaye mbali na kushambulia pia ni mzuri wa kuifanya timu yake kukaba kwa haraka inapopoteza mpira.“Ndio nimesikia kwamba Yanga imefanya mabadiliko kwenye benchi la ufundi, kwanza niwapongeze viongozi kwa kumpata kocha mwingine bora ambaye mimi sina mashaka naye kabisa.

“Namjua Sead (Ramovic) ni kocha kijana lakini falsafa ya soka lake limenivutia sana tangu nimemjua, naamini Yanga itacheza vizuri sana kwa kushambulia na kukaba kwa nguvu.

“Hapa Afrika Kusini tangu nilipofika tukajikuta tunakuwa marafiki kwa muda mfupi, kila mmoja alikuwa anavutiwa na mbinu za wenzake, hivyo ni wazi Yanga imepata kocha mzuri.

“Unajua nawapenda sana mashabiki wa Yanga, napenda kuona wanaendelea kufurahi, hiyo ni familia yangu na kama utakumbuka wakati naondoka nilisema kwenye gazeti lenu kwamba watu wasiwe na wasiwasi kwani walionileta mimi hapo (Yanga) wanabaki ambao ni viongozi wa juu wa hiyo timu na wameendeleza hilo, sasa wamepata mtu sahihi,” alisema Nabi.

Nabi amewatumia salamu wachezaji wa Yanga akisema kama kuna asiyetaka kujituma au kuendekeza starehe abadilike haraka kwa kuwa Mjerumani huyo sio muumini wa kuvumilia hayo wala kusumbuliwa na mchezaji anayejiona ana jina kubwa.

“Nadhani kitu ambacho naweza kuwaambia wachezaji wa Yanga wajitume lakini pia wajichunge na nidhamu, Sead ni kocha ambaye anataka kwanza mchezaji awe na nidhamu ya hali ya juu, haogopi presha wala havumilii utovu wa nidhamu kisa unafanywa na mchezaji mwenye jina kubwa, atawafukuza, hilo ni muhimu wakazingatia.

“Mashabiki wa Yanga nadhani wampe ushirikiano, atawafurahisha tu, hilo sina mashaka nalo, bahati nzuri anakwenda kukutana na timu yenye wachezaji bora.

“Timu pinzani kwa Yanga zijipange, ukweli ni kwamab hajatoka klabu kubwa sana lakini kwa timu anayokwenda kuifundisha ataipa mafanikio makubwa kwa kuwa ni kocha kijana mwenye njaa ya mafanikio,” alisema kocha huyo kipenzi cha mashabiki wa Jangwani.

Ana miaka 45. Alicheza klabu mbalimbali za Ligi za Ujerumani, Norway, Denmark, Serbia na Ukraine kama  mlinda mlango kabla ya kuhamia kwenye ukocha ambapo mwaka 2021 hadi 2024 aliifungisha TS Galaxy ya Afrika Kusini.

Kabla ya hapo, alikuwa kocha msaidizi katika timu ya FK Novi Pazar (Okt 1, 2021 – Des 31, 2020). Pia kocha msaidizi: Vladica Petrovic (mechi 32), Kenan Kolasinac (mechi 25), Zoran Maric (mechi 24), Nesko Milovanovic (mechi 16), Mladen Dodic (mechi 16), Marjan Zivkovic (mechi 16), Darko Tesovic (mechi 13), Izet Ljajic (mechi 9), Slavko Matic (mechi 8), Nebojsa Vucicevic (mechi 7), Stevan Mojsilovic (mechi 7), Petar Kurcubic (mechi 7), Zoran Govedarica (mechi 6), Radmilo Ivancevic (mechi 6), Radoslav Batak (mechi 5).

Related Posts