Kuanguka kwa ghorofa Kariakoo: Tulimpuuza Lowassa

 

TAKRIBANI majengo 100 ya ghorofa jijini Dar es Salaam, zilimejengwa kinyume cha taratibu za ujenzi, Bunge lilielezwa.

Kwa mujibu wa ripoti iliyoundwa na aliyekuwa Waziri Mkuu na kujiuzulu, Edward Lowassa, kati ya ghorofa 505 ambazo zilikaguliwa, majengo 147 yamekutwa hayana nyaraka za ujenzi.

Lowassa aliunda tume baada ya jengo la hoteli ya Chang’ombe Village Inn, lililokuwapo maeneo ya Keko, kuanguka ghafla mwaka 2006.

Katika tukio hilo, mtu mmoja aliuwa na wengine kadhaa kujeruhiwa.

Wakati wa tukio hilo, kuliibuka madai kwamba kulikuwa na ukiukwaji katika ujenzi wake. Jambo ambalo lilimsukuma Lowassa, kuunda tume haraka sana ya kukagua ghorofa zote zilizopo jijini Dar es Salaam.

Aliyekuja kuchukua nafasi ya Lowassa – Mizengo Kanyanza Pinda, baadaye aliliambia Bunge kuwa “Tume ya ukaguzi ya Lowassa,” ilibaini pia ghorofa 81 zilikiuka masharti ya ujenzi.”

Aliongeza, “…ghorofa zingine 22 wamiliki wake hawakupatikana na zilijengwa bila kuzingatia taratibu na sheria za ujenzi.

“Can you imagine, mtu anaamua kupandisha ghorofa lake hapo bila kufuata taratibu za mamlaka husika, hii ni hatari kubwa,” alisema Pinda.

Waziri mkuu huyo alikuwa akifanya majumuisho ya hotuba ya bajeti ya matumizi ya ofisi yake bungeni kwa mwaka wa fedha 2008/09.

Alisema ghorofa nyingi zinazojengwa jijini Dar es Salaam, zinajengwa holela bila kufuata taratibu za ujenzi.

Lowassa aliunda tume, na kuagiza majengo yote yasiyofuata utaratibu; yale yaliyo katika hatari ya kubomoka kutokana na ujenzi wa ovyo, basi yabomolewe yote. Mpaka sasa, ikiwa ni takribani miaka 20, hakuna hatua iliyochukuliwa.

Kuibuka kwa taarifa za Tume ya Lowassa, kumeibuka muda mfupi baada ya watu watano kuripotiwa kufariki dunia, na zaidi ya 40 kujeruhiwa katika eneo la Kariakoo, baada ya ghorofa moja kuanguka jana majira ya saa tatu asubuhi.

Ghorofa hili, lilianguka wakati mafundi wa ujenzi wakiendelea na shughuli ya kuongeza maduka.

Hadi leo Jumapili, shughuli ya uokoaji zinaendelea huku watu takribani 40, wakiripotiwa kupokelewa kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya matibabu.

Taarifa ya leo asubuhi, imemnukuu mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, akieleza kuwa kuna watu bado wamenaswa kwenye kifusi.

Alisema, vikosi vya uokozi vimeweza kuwasiliana nao na juhudi za kuendelea kuwatafuta zinaendelea.

About The Author

Related Posts