NYOTA wawili wa kimataifa wanaocheza Ligi ya Walemavu nchini Uturuki, wanaanza mechi za kwanza za ligi kwa vigogo nchini humo.
Kwenye ligi hiyo watanzania wawili, Ramadhan Chomelo anayekipiga Konya Amputee na Hebron Shedrack wa Sisli Yeditepe ndio wanacheza soka la ulemavu kwa msimu wa tatu sasa.
Ligi hiyo itaanza rasmi Novemba 24 na Chama la Shedrack likianza na Sahinbey Belediye SK iliyomaliza nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi.
Kwa upande wa Chomelo siku hiyo watakuwa na kazi mbele ya mabingwa watetezi Alves Kablo kwenye ufunguzi wa msimu mpya
Wakizungumza na nyakati tofauti, Chomelo alisema haitakuwa mechi rahisi kwa upande wao kutokana na ubora wa wapinzani wao.
“Msimu uliopita tulipokutana tulipoteza, maandalizi yanakwenda vizuri kuhakikisha tunaanza vizuri na ni mechi yetu ya ugenini hivyo timu inafanya kila kitu ingawa haitakuwa rahisi .”
Shedrack alisema zinapokutana timu mbili zilizoachana pengo kubwa inakuwa ni mechi ya kiushindani kila moja ikihitaji pointi tatu kuanza vizuri.
“Tulimaliza mkiani lakini hiyo sio sababu ya kupoteza mchezo mbele ya wapinzani wetu ambao walimaliza nafasi ya pili, tunaamini utakuwa mwanzo mzuri kwetu.”