WANAFUNZI 40 WATAKAOPATA UFAULU WA JUU MASOMO YA SAYANSI KUPATA UFADHILI CHUO KIKUU DAR

Na Gideon Gregory, Dodoma.

Ili kuwezesha na kuimarisha huduma ya utoaji na upatikanaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu wenye sifa na uhitaji, Serikali itatoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi 40 wenye ufaulu wa juu kwenye masomo ya sayansi hususani wanafunzi wa kike waliohitimu Mtihani wa Taifa ya Kidato cha Sita na shahada ya awali kupitia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Hayo yameelezwa leo Mei 07,2024 Bungeni Jijini Dodoma na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2024/25.

“Serikali itaendelea kukusanya madeni ya mikopo iliyoiva ya kiasi cha Shilingi Bilioni 198 kutoka sekta ya umma na kuimarisha makusanyo kutoka sekta binafsi na isiyo rasmi aidha, itatafuta wanufaika wapya 40,000 wenye marejesho ya mikopo iliyoiva ikijumuisha wanufaika wapya 5,000 wenye mikopo chechefu kutoka sekta binafsi na isiyo rasmi,”amesema Prof. Mkenda.

Pia ameongeza kuwa Serikali itaanza kutoa ufadhili kwa ajili ya shahada za juu ikiwemo eneo la fani ya mionzi na nyuklia.

Sambamba na hayo amesema katika mwaka wa fedha ujao Serikali itaendelea kukuza ujuzi wa uandishi na kuhamasisha tabia ya usomaji na kuimarisha matumizi ya maktaba katika ngazi zote za elimu kwa kuandaa Rasimu ya Sera ya Taifa ya Huduma za Maktaba nchini.

“Serikali itaendelea kusimamia na kuratibu utoaji wa Tuzo ya Kitaifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu yenye lengo la kuhamasisha uandishi na usomaji wa vitabu, kutunza historia na utamaduni wa Mtanzania na kuinua sekta ya uchapaji nchini. Tuzo hizo zitatolewa kwa waandishi mahiri wa riwaya, hadithi fupi na ushairi,”amesema.

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeliomba Bunge liidhinishe jumla ya shilingi Trilioni 1.96 kwaajili ya matumizi ya kawaida, mishahara na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Related Posts