Lushoto yaendesha mafunzo ya Chanjo ya Saratani ya Shingo ya Kizazi

Na Mwandishi Wetu

ZIKIWA zimebaki siku chache kabla ya kuanza kwa kampeni ya Chanjo ya Saratani ya Shingo ya Kizazi, Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto kupitia Idara ya Afya na Ustawi wa Jamii na Idara za Elimu Sekondari na Elimu Msingi na Awali imeendesha mafunzo kwa walimu na wahudumu wa afya katika Halmashauri hiyo.

Mafunzo hayo yaliyofanyika leo Aprili 19, 2024, yamelenga kuwaelimisha walimu wa afya mashuleni pamoja na wahudumu wa afya juu ya uwepo wa kampeni hiyo inayotarajia kufanyika kati ya Aprili 22 hadi 26, 2024 ikiwalenga wasichana wenye umri wa miaka 9 hadi 14.

Katika mafunzo hayo washiriki walielezwa juu ya umuhimu wa chanjo hiyo ambayo imelenga kuwalinda wasichana wenye umri huo dhidi ya saratani ambayo kwa mujibu wa takwimu ni moja kati ya saratani ambayo inaongoza kwa kuathiri wanawake wengi nchini ikifuatiwa na saratani ya matiti.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mratibu wa Chanjo Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, Zawadi Mweta amesema wametoa mafunzo hayo kwa walimu  ili wawe na uelewa wa chanjo hiyo na waweze hata kuelimisha jamii pindi wakihitaji kufanya hivyo.

Zawadi  ameeleza kuwa mwaka huu watachanja watoto kati ya umri wa miaka 9 hadi 14, lakini kuanzia Januari 2025 Chanjo ya Saratani ya Shingo ya Kizazi itatolewa kwa watoto wenye umri wa miaka 9 tu kwa dozi moja tu.

Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto imelenga kuwafikia watoto wote wenye umri huo wakati wa kampeni lengo likiwa kuhakikisha wasichana wote wanaostahili kupata chanjo wanapata ili kuwalinda na maambukizi ya saratani hiyo hatari.

Related Posts