Washiriki Guru Nanak wamuenzi Pano

WASHIRIKI wa mbio za magari ya Guru Nanak, wamemuenzi dereva Pano Calavria, aliyefariki dunia hivi karibuni, kutokana na jitihada zake za kuutangaza mchezo huo nchini na kuwa kivutio cha madereva kutoka nje ya nchi.

Pano aliyefariki dunia akiwa na umri wa miaka 78 baada ya kuugua muda mrefu, kifo chake kimetokea kipindi ambacho madereva wa Tanzania na nchi jirani wakienda jijini Arusha kushiriki mbio za magari ya Guru Nanak, ambayo yamevunja rekodi ya kwa kuwa na idadi kubwa  ya madereva  kutoka nje ya nchi.

 “Familia ya mbio za magari haitamsahau Pano kwa mchango wake wa kuileta dunia nzima ya mchezo huu Tanzania na kuufanya kuwa ni kichocheo cha utalii,” alisema David  Matete kutoka Amapiano Team ya Dar es Salaam.

Awadh Bafadhil alisema familia ya mbio za magari inamuenzi Pano kama mhamasishaji mzuri wa ushindani akiwa pia ameshiriki naye katika mashindano mengi ya ndani na nje ya nchi.

“Jina la Pano halitapotea katika kumbukumbu za wapenzi wa mbio za magari akiwa ni mmoja wa madereva wa awali wa Subaru Impreza. Tunasikitika sana kutokuwa naye hapa Arusha kwenye mbio za magari za Guru Nanak,” alisema Bafadhil.

Bafadhil aliongeza, mwaka 2006 ndiyo ulikuwa bora  sana kwa Pano Calavria na Watanzania katika mbio za magari kwa Afrika Mashariki kutokana na ushiriki wao kwa wingi mbio za magari Kenya na Uganda za KCB Rally ya Kenya na Pearl  of  Afrika Rally ya Uganda na kuungana na Kirit Pandya, Navraj Hans  na Omar Bakhressa kama madereva wa waliowahi kufanya vizuri katika nchi hizo.

“Mimi nikiwa namuongoza  dereva Issa Mohamed wa Tanga, tulimaliza kwa shida mbio za KCB, lakini Pano aliendesha vizuri na kumaliza 10 bora wakati Pandya, Navraj Hans(Kenya na Omar Bakhresa (Uganda) walimaliza katika top-five.

Baadhi ya wanachama wa STADO waliokuwa karibu na Pano walisema gwiji huyo alisaidia kuwaunganisha madereva wa Tanzania na majirani kutoka Kenya, Uganda na Zambia.

Related Posts