BINGWA wa Samia Supa Cup, Kata ya Msasani anatarajiwa kuvuna Sh4 milioni baada ya Diwani wa Kata hiyo, Luca Neghest ametangaza kwenye uzinduzi wa mashindano hayo.
Neghest alisema hayo wakati wa uzinduzi rasmi uliofanyika kwenye ufukwe wa Coco (Coco Beach) na kushirikisha mamia ya wadau wa michezo ambao, pia walishiriki matembezi maalum kwa ajili ya ufunguzi wa mashindano hayo.
Kulikuwepo pia na michezo mbalimbali na burudani kutoka bendi namba moja nchini, African Stars ‘Twanga Pepeta’.
Alisema zawadi hiyo itakuwa kwa mashindano ya soka na mchezo wa rede kwa wanawake na washindi wa pili watazawadiwa Sh2 milioni kila mmoja.
Mshindi wa kwanza kwa mchezo wa drafti atapata Sh2 milioni na wa pili Sh1 milioni, huku upande wa bao, mshindi ni Sh 1 milioni na wa pili Sh500,000.
Alisema maandalizi ya mashindano hayo yaliyopangwa kuanza Desemba 9, 2024 yanaendelea vizuri na yanatarajiwa kuwa na ushindi na msisimko mkubwa.
“Kila mwaka, Kata ya Msasani imekuwa nikiandaa mashindano ya Diwani Cup, safari hii tumebadilika na kuandaa mashindano ya Samia Supa Cup kwa lengo la kutambua uongozi wake bora katika sekta mbalimbali.”