KOCHA Mkuu wa Mbuni FC, Leonard Budeba amesema kwa sasa kikosi hicho kinahitaji maboresho wakati dirisha dogo la usajili litakapofunguliwa Desemba 15, mwaka huu, ili kutengeneza balansi nzuri hususani katika eneo la uzuiaji na ushambuliaji.
Akizungumza na Mwanaspoti Budeba alisema ushindani msimu huu umekuwa mgumu na hali ya mwenendo wao sio mzuri hivyo, ni vyema kujipanga mapema kwa sababu kadri ambavyo ligi inasonga mbele ndivyo ambavyo kila timu inajipanga kufikia malengo.
“Tulivyoanza Ligi na sasa kumekuwa na matumaini kidogo, ingawa tumekosa balansi nzuri katika michezo yetu minane ambayo tumecheza hadi sasa hivyo, tunahitaji kurekebisha hali hiyo, changamoto ni eneo la ulinzi na ushambuliaji,” alisema.
Kocha huyo aliongeza katika kipindi hiki ataendelea kupambana na hali hiyo kuhakikisha hawadondoshi pointi nyingi ingawa dirisha dogo tu litakapofunguliwa Desemba 15, ataingia sokoni ili kuongezea nguvu maeneo hayo ambayo ndio uti wa mgongo.
Katika michezo minane iliyocheza kabla ya ule wa jana dhidi ya Green Warriors, timu hiyo imefunga mabao manane ikiwa na wastani wa kufunga bao moja kila mchezo, huku nyavu zake zikitikiswa mara tano hali inayomfanya Budeba kujipanga mapema.