Uchaguzi huu unaofanyika miezi minane baada ya Rais Faye na timu yake ya waliokuwa wapinzani wakubwa wa serikali kuingia madarakani, ni muhimu kwa kiongozi huyo kijana anayeelemea mrengo wa kushoto na ambaye alitumia kampeni yake kuahidi mageuzi makubwa ya kiuchumi, mfumo wa haki za kijamii na mapambano dhidi ya ufisadi.
Ahadi hizo zinatajwa kuwa ndizo ambazo ziliwavutia vijana walio wengi katika taifa hilo la Afrika Magharibi lenye ukosefu mkubwa wa ajira na kiwango cha juu cha ugumu wa maisha kumuunga mkono Faye.
Soma zaidi: Sonko awataka wafuasi wake kulipiza kisasi
Hata hivyo, bunge linaloongozwa na upinzani limeifanya miezi ya mwanzo ya serikali hiyo mpya madarakani kuwa migumu sana, jambo ambalo lilimfanya Faye kulivunja bunge mwezi Septemba na kuitisha uchaguzi wa mapema mara tu katiba ilipomruhusu kufanya hivyo.
“Nitarajia kwamba Pastef (chama kinachotawala) kitashinda uchaguzi huu kwa wingi wa viti ili kiweze kutekeleza mipango yake kwa ukamilifu,” alisema Pascal Goudiaby, raia mwenye umri wa miaka 56, mmoja wa mamia ya wengine waliokuwa wakingojea kupiga kura zao katika mji mkuu, Dakar.
“Kipaumbele ni ukosefu wa ajira, vijana wengi sana wanakabiliwa na ukosefu wa ajira,” aliongeza.
Faye alimteuwa shujaa wake, Ousmane Sonko, kuwa waziri mkuu, baada ya ombi la Sonko kuwania urais kukataliwa kufuatia mkwamo wa miaka mitatu kati yake na serikali ya wakati huo.
Uchaguzi wa kuimarisha madaraka
Faye na Sonko waliahidi kuugawanya uchumi na kuwa na vyanzo mbalimbali na kuingia kwenye ubia wa masuala ya kiuchumi, kupitia upya mikataba ya nishati na uvuvi na kujesha mamlaka ya Senegal, ambayo wanadai yameuzwa kwa mataifa ya kigeni.
Wachambuzi wanasema kihistoria wapigakura wa Senegal wamekuwa wakitumia uchaguzi wa bunge kumthibitisha rais wanayemtaka, na kwa sasa chama tawala cha Pasef ndicho kinachopendelewa nao.
Soma zaidi: Waziri Mkuu wa Senegal atoa wito wa ulipaji kisasi baada ya wafuasi wake kushambuliwa
“Nadhani kwamba yeyote uliyemuamini kwenye uchaguzi wa rais, unahitaji kumpa tena imani yako ili aweze kukamilisha alichoakianza,” alisema Toure Aby, mpigakura mwenye umri wa miaka 65, aliyeongeza kwamba wao wanataka maisha yawe rahisi kwa kila mtu, kwani kwa sasa kila kitu kimekuwa ghali yakiwemo mahitaji ya lazima kama vile maji, umeme na chakula.
Chanzo: AFP