Ruaha Girls imeibuka mbabe mara mbili dhidi ya Tarangire Girls katika michezo ya majaribio ya kriketi kwa nyota wa kike nchini, kwenye Uwanja wa UDSM, jijini mwisho wa juma.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Chama cha Kriketi Tanzaniai(TCA), Ateef Salim, michezo hii ya mizunguko 20 na 15, imezindua rasmi zoezi la kusaka wachezaji bora kwa ajili ya kikosi cha timu ya Taifa ya wanawake itakayoshiriki michuano ya dunia mwakani.
“Wachezaji hao watacheza mechi nyingi za majaribio ili kupata kikosi bora kwa ajili ya mchuano ya kimataifa,” alisema .
Katika mchezo wa kwanza wa mizunguko 15, Ruaha Girls ilipata ushindi wa wiketi saba, huku wa pili wa mizunguko 20, Tarangire wakipoteza kwa mikimbio mitano.
Mchezo wa kwanza, Tarangire Girls ndiyo walioanza kubeti na kutengeneza mikimbio 87, huku wakipoteza wiketi tano baada ya kumaliza mizunguko 15.
Ruaha Girls ilitumia mizunguko 13 kuzifikia alama za wapinzani wao na kutengeneza mikimbio 89 huku wakipoteza wiketi tatu. Vinara wa mchezo huo walikuwa ni Sophia Frank aliyetengeneza mikimbio 15 na kupata wiketi moja, Saum Borakambi, mikimbio 16 na Englide Geoffrey 13 na wiketi moja.
Ruaha Girls waliendeleza ubora wao dhidi ya Tarangire katika mchezo wa pili wa mizunguko 20, na kushinda kwa mikimbio mitano na ndio walioanza kubeti na kutandaza mikimbio 97 baada ya mizunguko 20 wakipoteza wiketi nne.
Tarangire walipata mikimbio 92 baada ya wote 10 kutolewa wakitumia mizunguko 19 kati ya 20 kuipa Ruaha ushindi mwembamba wa mikimbio 5.
Mkongwe Fatuma Kibasu alichangia ushindi wa Ruaha baada ya kupiga mikimbio 44 peke yake kutokana na mipira 46.
Nasra Hamza aliyepiga mikimbio 14 bila kutolewa na Getrude Mushi aliyeongezea mikimbio 12, pia walikuwa na mchango kwenye ushindi wa Ruaha Girls.