DORIS MOLLEL FOUNDATION YAZIFIKIA HOSPITALI 85 NCHINI KWA KUTOA VIFAA TIBA VYENYE THAMANI ZAIDI 1.5 BILIONI

NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV

TAASISI ya Doris Mollel Foundation katika jitihada za kusaidia watoto wanaozaliwa kabla ya wakati, mpaka sasa tayari wamezifikia hospitali 85 nchi nzima katika kuchangia vifaa tiba kama mashine za kupumulia, vitanda n.k, vyenye thamani ya zaidi ya bilioni 1.5.

Ameyasema hayo jana Novemba 16, 2024 Dkt. Sylvia Rambo akimwaakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo, Doris Mollel katika Mafunzo kwa waandishi wa habari kuhusu jinsi ya kuandaa makala za watoto njiti wakati wakiadhimisha Siku ya Mtoto Njiti Duniani.

Aidha, walikuwepo wazazi wa watoto waliozaliwa kabla ya wakati, wameiomba serikali kuingilia kati, ikiwemo gharama kubwa za kuwahudumia watoto njiti, jambo ambalo linakatisha tamaa ya kuokoa maisha ya watoto wao.

Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Watoto na Mjumbe wa Bodi ya taasisi hiyo, Albert Chota amesema kuna wajibu wa serikali kuongeza idadi ya wahudumu wa afya, ambao wataisadia kuokoa maisha ya watoto njiti.

Sambamba na mafunzo hayo, pia kumezinduliwa jarida kuhusu huduma nafuu kwa akina mama wa watoto njiti.

Mtandao wa Familia za Watoto Njiti ulizinduliwa pia kwa ajili ya kuleta uchechemuzi kwenye sera mbalimbali za huduma ya afya zinazowahusu watoto wanaozaliwa kabla ya wakati, kutoa elimu, upembuzi yakinifu, kuondosha imani potofu kwenye jamii pamoja na kushirikiana na serikali na wadau wengine.

Maadhimisho ya Siku ya Mtoto Njiti Duniani huadhimishwa Novemba 17 kila mwaka.









Related Posts