Dar es Salaam. Tanzania yang’ara katika vipengele vya uvumbuzi na bunifu bora zilizofanywa na watoto katika mashindano ya kukuza ubunifu wa masuala ya teknolojia na uhandisi, kwa watoto yanayojulikana kama Pan African Steam.
Pia imeibuka kidedea katika kipengele cha uwasilishaji na timu bora ya utendaji kazi.
Mashindano hayo yamefanyika jana Jumamosi Novemba 16, 2024 katika ukumbi wa Shule ya Msingi Aga Khan na kuwakutanisha wanafunzi takriban 200 kutoka nchi tatu za Afrika Mashariki ambazo ni Tanzania, Kenya na Uganda.
Kwa mwaka huu shindano hilo limefanyika kwa mara ya pili likiwahitaji washiriki kutumia vifaa mbalimbali vya michezo ya watoto.
Ambapo kwa vifaa hivyo walitakiwa kubuni mfano wa mji wa kisasa wenye maeneo yote muhimu ikiwemo njia kuu za usafirishaji.
Washiriki hao walitakiwa kutumia takriban dakika 50 kutekeleza wazo hilo wakiwa katika makundi ya watoto sita.
Akizungumza wakati wa shindano hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Young Engineers Tanzania, Benazir Kurji amesema lengo kuu la kuja na mashindano hayo ni kuwafundisha watoto ujuzi muhimu wa karne ya 21.
Pia kuanza kuwajenga watoto katika fikra za kibunifu na uvumbuzi na kufanya kazi kwa ushirikiano.
Vilevile kuanza kumtengeneza na kumuweka mtoto katika uwezo wa kutumia rasilimali zilizopo kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii.
“Ndio maana limelenga zaidi watoto kuanzia umri wa miaka 6-14 ili kuanza kuwajengea uwezo na kuwapatia ujuzi tangu wakiwa na umri mdogo”amesema.
Kwa upande wake Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Blandina Duwe amesema kuwa mashindano hayo ni muhimu kwa sababu inawasaidia wanafunzi kutumia ujuzi wao kutatua matatizo mbalimbali ya jamii ili kuleta maendeleo endelevu
“Sasa hawa watoto wetu wanapata fursa ya kubuni vitu mbalimbali ambavyo vinaweza kuisaidia jamii katika kutatua matatizo kama miundombinu, foleni za barabarani shindano walilolifanya hapa linaweza kusaidia kutatua matatizo haya,” amesema.