Arusha. “Nilipata taarifa za kuteuliwa na kutenguliwa usiku na ulikuwa usiku mrefu sana kwangu.” Haya ni maneno ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha (RC), Paul Makonda akielezea alivyopokea mabadiliko ya uongozi kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) hadi serikalini.
Makonda amesimulia hilo leo Jumapili, Novemba 17, 2024 wakati akiwasilisha ripoti ya miezi sita ya utendaji kazi wake katika nafasi ya ukuu wa Mkoa Arusha iliyofanyikia ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Arusha (AICC).
Shughuli hiyo imehudhuriwa na waandishi wa habari waliouliza maswali mbalimbali, wananchi na viongozi wa serikali na chama ndani ya mkoa huo.
Machi 31, 2024, Rais Samia Suluhu Hassan alimteua Makonda kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha akitoka kuhudumu nafasi ya Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, nafasi aliyoteuliwa na Halmashauri Kuu ya CCM, Oktoba 22, 2023.
Swali la aliwaza nini juu ya uteuzi huo wa ukuu wa mkoa ambao ni mdogo kuliko wa uenezi limeulizwa na Mhariri wa Maudhui ya Mitandao ya Jamii wa Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL), Zouhra Malisa.
Makonda amesimulia namna alivyopata taarifa za kutenguliwa na kuteuliwa kushika nafasi hiyo usiku, huku akisema hata nafasi ya mtendaji wa mtaa ni kubwa.
Amesema alipoteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha alipata mawazo ya namna gani ataanza kutekeleza majukumu yake mapya katika nafasi hiyo, ambayo aliwahi kuihudumu zaidi ya miaka mitatu nyuma.
“Nilipata taarifa za kuteuliwa na kutenguliwa usiku na ulikuwa usiku mrefu sana kwangu kwa sababu mimi maisha yangu nikipewa kazi naiwaza usiku na mchana.”
“Nilikuwa nawaza sasa ukuu wa mkoa wa Arusha kwangu haikuwa suala la nafasi ndogo kwa sababu aliyenipa nafasi kubwa ni huyohuyo aliyenipa hiyo uliyoiona ndogo ni huyohuyo.
Katika maelezo yake, Makonda amesema,”kwangu haikuwa shida hiyo, shida ukuu wa mkoa naanzaje nimeshasahau nilikaa nje ya serikalini miaka mitatu na miezi sita na nilishazoea kwenye chama na pilikapilika.
“Ilikuwa namna gani najipanga kurudi upya na kwa nguvu ileile kwenye mazingira yangu mapya ya kazi, kwangu nilijua ni mapenzi mkubwa ya Rais wangu kunipa nafasi eneo lingine la Serikali, kwa mtazamo wa mtu mwingine ni nafsi ndogo ila mimi hata utendaji wa mtaa ni nafasi kubwa sana,” amesema.
Huku akishangiliwa, Makonda amesema ukiwa na tabia ya kuhudumia watu hata ukipewa nafasi ya mtaa utafurahi kushiriki kutoa mchango kwa watu unaowaongoza.
“Arusha nilikuta ni watu wakarimu, na ninyi mliona wote wakati nateuliwa wakasema sasa ni mwisho wake wa siasa, huu ndio mwanzo wangu wa siasa. Walisema kule ataenda kukutana na wazee wa chuga watamnyoosha.
“Ni kwa sababu maelezo yamekuwa mengi kumtengeneza mtu mwonekano ambao siyo wake, nimekutana na watu wakarimu wenye upendo na bidii ya kufanya kazi ukikuta mtu anapenda ushirikina humu ni mgeni, huku watu wanatafuta pesa mambo mengine hawana,’ amesema.
Swali jingine lililoulizwa na Zouhra aliikuta Arusha ya aina gani na siku akiondoka anatamani akumbukwe kwa lipi, Makonda amesema,”alama ninayotamani kuiacha ni moja kubwa, awepo mtu mmoja kwenye maisha yake ambaye atashukuru Mungu mimi kuwa kiongozi wake.”
Kuhusu kero za wananchi mkoani humo amesema katika wiki ya haki ya kusikiliza kero za wananchi aliyoifanya wananchi zaidi ya 3,000 waliwasilisha kero zao.
Amesema kati ya hizo, kero 1,650 sawa na asilimia 52 zilihusu sekta ya ardhi.
Wakati huohuo Makonda amesema Desemba 1, 2024, Rais Samia Sulubu Hassan anatarajia kukutana na viongozi wa Ngorongoro na wazee wa mila jijini Arusha ili kufahamu changamoto na kuzipatia ufumbuzi.