Arusha. Serikali ya China imeahidi kuisaidia Tanzania kufikia lengo lake la kutembelewa na watalii milioni tano ifikapo 2025, sambamba na kuzalisha mapato ya dola bilioni sita kutoka sekta ya utalii.
Kulingana na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) hadi mwezi Julai 2024, idadi ya watalii waliowasili nchini ilikuwa 2,026,378, na hivyo kuwepo na pengo la watalii 2,973,622 ili kufikia lengo hilo la mwaka 2025.
Na imeelezwa kuwa lengo la serikali ni kuzalisha dola bilioni 6 (takribani Sh15.6 trilioni) kutoka kwa watalii ifikapo mwaka 2025.
Pia mpaka kufikia Julai, 2024, mapato kutoka sekta ya utalii yalifikia dola 3.534 bilioni (Sh9.1 trilioni) hivyo kuacha pengo la dola 2.466 bilioni (Sh6.24 trilioni).
Leo, Jumapili Novemba 17, 2024, katika hafla ya uwekaji jiwe la msingi la Kituo cha Taarifa cha Ngorongoro – Lengai Geopark, kilichofadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China, Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingian, amesisitiza dhamira ya nchi hiyo kuendelea kusaidia Tanzania kufanikisha malengo yake ya utalii.
“China, kama rafiki wa muda mrefu wa Tanzania, imeendelea kuunga mkono maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya nchi hii kwa zaidi ya miaka 60 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia. Katika miaka ya hivi karibuni, tumekuwa tukitoa msaada wa moja kwa moja katika kukuza sekta ya utalii, na tunaahidi kuendelea kufanya hivyo,” amesema Balozi Mingian.
Amebainisha kuwa kituo hicho ni mradi wa kipekee unaolenga kuhifadhi urithi wa kijiolojia wa Tanzania, na ni juhudi ya kwanza ya aina yake kufadhiliwa na China nje ya mipaka yake.
“Huu ni upendeleo wa kipekee kwa Tanzania, na tunaamini mradi huu utakuwa kichocheo cha ushirikiano wa kimkakati kati ya nchi zetu mbili, huku ukitoa jukwaa la kubadilishana maarifa katika nyanja za utalii na utamaduni,” amesema Balozi huyo.
Aidha, amesifu utajiri wa Tanzania katika rasilimali za asili za utalii, akitaja vivutio vya kimataifa kama Mlima Kilimanjaro, Hifadhi ya Serengeti, Visiwa vya Zanzibar na Hifadhi ya Ngorongoro, akisema malengo ya kuongeza idadi ya watalii yanaweza kufikiwa kwa urahisi.
Balozi Mingian pia amesema juhudi za China kutangaza utalii wa Tanzania, akitolea mfano wa filamu ya Tanzania Amazing, iliyotengenezwa kwa ushirikiano wa Kim Dong, mwigizaji maarufu wa China na balozi wa utangazaji wa utamaduni na utalii kati ya nchi hizo mbili.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Uhifadhi wa Urithi wa Utamaduni na Jiolojia, Dk Agness Gidna amesema kituo hicho ambacho kitagharimu zaidi ya Sh22 bilioni, kitakuwa mfano kwa maonyesho ya vipengele mbalimbali vya urithi wa Hifadhi ya Ngorongoro.
“Kituo hiki kitatoa taarifa kuhusu urithi wa kijiolojia, historia ya milima na mabonde, wanyama waliopo na masuala mengine muhimu ya kijiografia na kiutamaduni,” amesema Dk Gidna.
Ameongeza kuwa kituo hicho kitakuwa na sehemu za maonyesho, makumbusho na ukumbi wenye uwezo wa kuhudumia zaidi ya watu 100.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Pindi Chana amesisitiza umuhimu wa kushirikisha wananchi katika utekelezaji wa mradi huo, akisema hilo litasaidia katika usalama na utunzaji wa mradi.
Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Dk Elirehema Doriye amesema mradi huo utawasaidia wakazi wa maeneo ya Karatu, Ngorongoro, Monduli na Longido kwa kutoa fursa za kiuchumi kupitia utalii wa miamba.
Mwenyekiti wa Bodi ya NCAA, Jenerali Mstaafu Venance Mabeyo amesema kazi ya ujenzi inasimamiwa kwa viwango vya kimataifa na inatarajiwa kukamilika Mei 2025.
“Hii itahakikisha kuwa watalii wanaanza kufurahia vivutio vya kituo hiki baada ya kukamilika,” amesema Mabeyo.