Arusha. Mkuu wa Mkoa wa Arusha (RC), Paul Makonda kwa mara ya kwanza amejibu tuhuma dhidi yake iliyomuhusisha katika shambulio la kupigwa risasi Makamu Mwenyekiti wa Chadema- Bara, Tundu Lissu.
Shambulio hilo lilitokea alasiri ya Septemba 7, 2017 akiwa ndani ya gari nyumbani kwake eneo la Area D, jijini Dodoma akijiandaa kushuka, baada ya kutoka kuhudhuria vikao vya Bunge vilivyokuwa vikiendelea.
Zaidi ya risasi 30 zilipigwa kwenye gari hilo na 16 zikimpa sehemu mbalimbali ya mwili wake. Alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Dodoma kwa matibabu ya awali na usiku uleule alihamishiwa Hospitali ya Nairobi nchini Kenya kwa matibabu.
Januari 2018, Lissu alihamishiwa nchini Ubelgiji kwa matibabu zaidi hadi aliporejea Tanzania mwaka 2020. Ni tukio lililoibua mijadala maeneo mbalimbali hususan eneo lilipotokea ambalo wanaishi viongozi wa serikali wakiwemo mawaziri na naibu spika wa Bunge kwa wakati huo.
Mara kadhaa, Lissu ambaye wakati mkasa huo unamtokea alikuwa Mbunge wa Singida Mashariki na Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni amekuwa akimtuhumu Makonda kuhusika na shambulio hilo.
Lissu ambaye kitaaluma ni mwanasheria amekuwa akidai Makonda ambaye wakati huo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam alihusika na tukio hilo akisema hata siku linatokea Makonda hakuwa jijini Dar es Salaam, alikuwa Dodoma kuendesha genge hilo.
“Hii ni mara ya tatu au ya nne nimemtaja Paul Makonda hadharani, ushahidi nilionao na taarifa nilizonazo ni kwamba Paul Makonda, ndiye aliyeongoza kikosi kazi (anataja hoteli aliyofikia), ndio maana siku ile hakuwepo Ikulu kwenye shughuli ya Magufuli, basi alikuwa ananishughulikia Dodoma,” alisema Lissu, Septemba 2024 alipozungumza na waandishi wa habari.
Siku hiyo ya Septemba 7, 2017, Rais wa wakati huo, John Magufuli alikuwa anapokea ripoti ya uchunguzi kuhusu mchanga wa madini ambao husafirishwa nje ya nchi makontena kwa makontena.
Leo Jumapili, Novemba 17, 2024, Makonda anawasilisha ripoti ya miezi sita ya utendaji kazi wake katika nafasi hiyo mkoani Arusha na moja ya swali aliloulizwa ni tuhuma ambazo zimekuwa zikitolewa na Lissu dhidi yake kuwa alihusika kwenye shambulio hilo.
Makonda amesema tuhuma hizo dhidi yake hazina ukweli kwa sababu siku ya tukio alikuwa kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam kwenye kampeni ya matibabu na hata Serikali ingekuwa na mpango wa kufanya hivyo wasingemtumia yeye (Makonda) ambaye hajawahi kwenda hata ng’ambo.
“Lissu nimemsikia hata mimi na nimeendelea kumsikia ila kwa hali aliyonayo siwezi kumshangaa na ninafarijika ameniona ninafaa kumsaidia kujenga ‘carrier’ yake ya siasa.”
Ukifika hatua unatajwa na makamu mwenyekiti kwa tuhuma nzito kama hizo tena mwanasheria bingwa ambaye anajua milango yote ya Mahakama ndani na nje ya nchi, nilitarajia kwamba angeshaongoza kufungua kesi mahakamani,” amesema.
Makonda amesema asingependa kuhangaika kubishana na Lissu na hakuna Rais anayeweza kutoa maelekezo kuunda kikosi kilichopo nyuma ya vikosi vyake na kufanya mambo ya aina hiyo.
“Nimesikia mambo mengi sana watu wanamsingizia Magufuli ‘he was a good man’ na alikuwa na mapenzi makubwa na wananchi wake,” amesema Makonda huku makofi yakipigwa na washiriki wa tukio hilo.