Baku, Azerbaijan. Watetezi wa mabadiliko ya tabianchi kutoka Afrika wamewasilisha ombi kwenye Mkutano wa 29 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP-29), kusisitiza hatua za haraka za mabadiliko hayo barani Afrika.
Wamewasilisha ombi hilo kwenye mkutano unaofanyika mjini Baku nchini Azerbaijan huku likiwa na saini zaidi ya 10,000 kwa Kikundi cha Wajumbe cha Afrika (AGN).
Ombi hilo, lililowasilishwa kwa Mwenyekiti wa AGN, Balozi Ali Mohamed, linahitaji wajumbe wa Afrika kuhimiza mustakabali wa nishati mbadala, fedha za mabadiliko ya tabianchi kwa usawa, na haki kwa jamii za Kiafrika zinazokumbwa na athari zinazozidi kuongezeka za mabadiliko hayo.
Mkurugenzi wa Programu wa Greenpeace Afrika, Murtala Touray amesema ombi hilo linawakilisha wasiwasi wa Waafrika ambao tayari wanahisi athari za uharibifu wa mabadiliko ya tabianchi.
“Ombi hili linawakilisha sauti za Waafrika wanaokutana na ukweli mchungu wa mabadiliko ya tabianchi. Tunawaomba wajumbe wa mazungumzo kuwajibisha kampuni za mafuta katika kusababisha uharibifu wa mazingira na kusaidia madhara kwa jamii zetu,” amesema Touray.
Moja ya madai muhimu ya ombi ni kuongezwa kwa uwekezaji katika suluhisho za nishati mbadala kote Afrika. Kwa kuwa umasikini wa nishati ni changamoto barani humo.
Ombi linataka kuhimiza mabadiliko ya matumizi ya nishati chafu kwenda kwa vyanzo vya nishati safi na endelevu kama vile nishati ya jua, upepo na umeme wa maji.
Akizungumza na Mwananchi leo, Mshauri wa nishati mpito Afrika kutoka Shirika la Kufuatilia Usimamizi wa Rasilimali za Asili (NRGI), Silas Olang’ amesema uharaka unaohitajika hivi sasa ni kukabiliana na athari zinazojitokeza.
Ametolea mfano kipindi ambacho bara la Afrika lilikuwa likihitaji fidia za hasara zitokanazo na athari, kwa sababu sio wasababishi wa athari hizo za hali ya hewa.
“Uharaka unaohitajika ni kukabiliana na athari zikiwemo mafuriko, ukame ambazo ni matokeo ya moja kwa moja yanayoonekana na yanayohitaji kuchukuliwa hatua za haraka.
Amesema Afrika imechelewa kuchukua hatua juu ya athari hizo kwani miaka inavyokwenda na athari zinaongezeka. “Ukiangalia nchi zetu yakitokea majanga hatuna uwezo wa kukabikiana nayo.
Mtetezi wa Mazingira, Fred Njehu amesisitiza dharura ya suala hili, akisema mustakabali wa Afrika lazima uwe wa nishati mbadala.
Takwa la wapigania haki za mazingira ni kupunguza utoaji wa hewa chafu na kulinda jamii zinazohitaji msaada dhidi ya uharibifu zaidi wa mazingira.
Hata hivyo, Greenpeace Afrika inasisitiza ombi la fedha za mabadiliko ya tabianchi ikisema ni jambo muhimu.
Ombi linataka fedha hizi ziwe ni ruzuku, badala ya mikopo, ili kuepuka kuzidisha mgogoro wa madeni katika nchi nyingi za Afrika. Zaidi ya hayo, ombi linadai kuwa wachafuzi wakubwa, hasa sekta ya mafuta walipie uharibifu waliosababisha kwa mazingira.
Ombi hili linakuja wakati muhimu kwa mataifa ya Afrika, ambayo yanatafuta ahadi kuhusu hatua za mabadiliko ya tabianchi na msaada wa kifedha.
Ombi hilo limefafanua kuwa makadirio yanaonyesha kwamba Waafrika milioni 118 huenda wakakumbwa na majanga yanayohusiana na mabadiliko ya tabianchi ifikapo 2030.