Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema hadi saa 4:00 asubuhi ya leo Jumapili, Novemba 17, 2024 watu 13 walikuwa wamepoteza maisha na majeruhi 84 kuokolewa katika ghorofa lililoporomoka, Kariakoo jijini Dar es Salaam.
Pia, amemuagiza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuongoza timu ya wataalamu wa ujenzi kukagua majengo yote ya Kariakoo na kumpa taarifa, huku akilitaka Jeshi la Polisi kupata taarifa ya kina kutoka kwa mmiliki wa jengo hilo na jinsi ujenzi ulivyokuwa.
Rais Samia amesema hayo leo Jumapili, akiwa jijini Rio de Janeiro nchini Brazil kupitia taarifa kwa umma iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu.
“Serikali itabeba gharama zote za waliojeruhiwa na kuhakikisha waliopoteza maisha wanastiriwa ipasavyo, nitoe pole kwa ndugu, jamaa na marafiki,” amesema Rais Samia.
Ameongeza: ‘’Hadi sasa sababu za kitaalamu za jengo kuporomoka hazijachunguzwa na kubainishwa na kipaumbele chetu ni kufanya uokozi.”
“Namtaka Waziri Mkuu kuongoza timu ya ukaguzi majengo kufanya zoezi la kukagua majengo yote ya Kariakoo tupate taarifa kamili ya hali ya majengo ya Kariakoo ilivyo. Jeshi la Polisi lipate taarifa kamili kwa mmiliki wa jengo kuhusu ujenzi ulivyokuwa,” amesema.
Rais Samia amesema taarifa zote hizo zikipatikana zitawekwa wazi na Watanzania watapata taarifa kamili.
Ndilo swali linaloulizwa na wengi baada ya wafanyabiashara waliokuwa na maduka kwenye jengo hilo lililoporomoka, nao kushindwa kumjua.
Hata hivyo, Mwananchi lilizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ambaye alisema kuhusu mmiliki wa jengo, suala lake bado linashughulikiwa na vyombo maalumu vya dola.
“Mara baada ya kujiridhisha na taarifa ya vyombo hivyo, tutawapa taarifa kuhusu mmiliki wa jengo hili ni nani, kwa sasa linafanyiwa kazi,” alisema Chalamila.
Wakati Chalamila akijibu hivyo, wafanyabiashara waliokuwa wamepanga kwenye ghorofa hilo lililopo mtaa wa Mchikichi Kariakoo, walisema hawajawahi kumuona mmiliki halisi wa jengo hilo zaidi ya mtu anayedaiwa kuwa ndiye msimamizi.
Jengo hilo ambalo ni la ghorofa nne, sehemu ghorofa ya kwanza ilikuwa sehemu ya maduka na ghorofa ya pili mpaka ya nne zilikuwa za kuhifadhia mizigo.
“Hilo ghorofa lilikuwa na maduka mengi si rahisi kuhesabu kwa sababu hata sehemu ya ghorofa tunazohifadhia mizigo zina stoo zaidi ya kumi, kwa hiyo ni ngumu kujua idadi yake,” alisema Shija Maganga.
Naye mbeba mizigo wa maduka yaliyopo katika ghorofa hilo, Hamidu Ally alisema jengo hilo linahifadhiwa mizigo na watu tofauti na kutokana na uhitaji wa sehemu kwa ajili ya biashara, ndiyo maana wahusika waliamua kuongeza sehemu ya chini.
“Licha ya kutaka kuunganisha njia kuungana na ghorofa nyingine iliyopo Mtaa wa Aggrey ambalo lilibomolewa pia, walikuwa wanafanya ujenzi wa kutanua vyumba huko chini,” alisema Hamidu.
Alisema watu hawamfahamu mmiliki hasa wa jengo hilo na wanaofika hapo ni wasimamizi ambao huwa hawafiki mara kwa mara bali huja kipindi cha kukuasanya kodi kwa wapangaji.
Mmoja wa wapangaji, Amos John ambaye alikuwa anamiliki duka la nguo za kike katika ghorofa hilo, alisema hakuwahi kukutana na mmiliki zaidi ya dalali.
“Tulilipia kodi kwa dalali, na hata alipokuja kuchukua pesa kila mwezi hatukuwa na nafasi ya kumuuliza kuhusu mmiliki wa jengo. Tuliamini dalali ndiye mjumbe wa mwenye nyumba.”
Akizungumza kwa huzuni, Grace Mgeni, aliyekuwa akimiliki duka kwenye jengo hilo, alisema hakuwahi kumwona mmiliki wa jengo hilo.
“Nililipa kodi kwa dalali na mara zote tulidhani yeye ndiye mwenye jukumu la kuhakikisha kila kitu kiko sawa hivyo sina hata namba za mmiliki na simjui anaitwa nani,” alisema Grace.
Aliongeza kuwa hakuwahi kufikiria kwamba jengo hilo lingeweza kuwa hatarini na ndio maana hakuwaza kuwa na namba wala jina la mmiliki kwa kuwa alikuwa anakutana na aliyempangisha.
“Kulikuwa na nyufa kwenye kuta, lakini tulidhani ni mambo ya kawaida katika majengo ya zamani Kariakoo. Hatujui hata pa kuanzia sasa, kila kitu changu kimepotea,” alisema
Mama ashuhudia mabinti zake wakiporomokewa
Ni wakati mgumu kwa mama anayejulikana kwa jina la mama Neema aliyepoteza mabinti zake wawili, Neema Sanga (36) na mdogo wake Buli Sanga (24), katika ajali ya ghorofa lililoporomoka jana mtaa wa Mchikichi, Kariakoo jijini Dar es Salaam jana.
Mama huyo ambaye ni mmoja wa wamiliki wa duka katika jengo hilo, ni mkazi wa Tabata Barakuda jijini hapa.
Mwananchi limefika nyumbani kwake na kushuhudia mama huyo akilia kwa uchungu na kupoteza fahamu mara kwa mara huku akitamka jina la Mungu mara zote kila akizinduka.
Akisimulia namna familia hiyo ilivyopokea taarifa hizo za msiba, Ramadhani Thabith ambaye ni jirani wa familia hiyo, amesema mabinti hao huwa wanatoka kwenda dukani saa 12 asubuhi na huwa wakifunga duka lao saa 11 jioni.
Amesema siku ya tukio, watoto walimweleza mama yao aende kwenye jumuiya na wao wanaenda kufungua duka na baada ya kutoka huko angeungana nao.
“Wana kawaida ya kwenda jumuiya kila Jumamosi wote watatu, mama na watoto wake, lakini jana (juzi) walimwambia mama yao aende halafu wao wanaenda kufungua duka licha mama yao kuwaambia waende kwanza jumuia wakitoka ndiyo waende dukani,” amesimulia Thabith.
Anasema walipofika dukani walifungua duka kama kawaida yao…“Tulikuwa tumeongozana mimi nilikuwa naelekea pia kwenye biashara yangu ya kuuza viatu Mtaa wa Mhonda.”
Amesema walipofika dukani kwao, mama yao naye hakuchukua muda akawa amefika, lakini alitoka kwenda kuweka fedha kwa wakala, wakati anarudia ndipo ghorofa hilo likawa linaanguka.
“Wakati anarudi kuweka pesa alipogeuka, aliona ghorofa likianguka kwa hiyo alipata mshtuko na kuzimia, alipelekwa hospitali na kisha kurudishwa nyumbani,” anasema jirani huyo.
Kwa Mujibu wa Thabiti, binti mkubwa wa mama huyo ambaye ni Neema alifanikiwa kuzungumza na mtu aliyekuwa anatoa msaada wa uokoaji akamwambia asubiri ili watafute njia ya kumtoa.
“Baada ya kuambiwa asubiri na mtu ambaye tunamfahamu, Neema alipata jazba akawa anahangaika ili kujitoa ndipo alipokanyaga nondo iliyofyatua kifusi kilichomkandamiza hadi akapoteza maisha, amesema huku hatima ya Buli ikiwa bado haijajulikana.