Kazi nzito Yanga, Ramovic aanza na Al Hilal

HUKO Yanga ndo sasa yanaanza. Ndio, kazi inaanza upya na presha ndani ya klabu hiyo sasa inahama kutoka kwa viongozi kidogo na kuhamia kwa wachezaji ambao leo watakutana kwa mara ya kwanza na kocha mpya wa timu hiyo, Sead Ramovic, huku akiwa na kazi ya kuanza kusoma faili la mmoja mmoja mapema.

Presha ni kwamba maisha yanaanza upya ndani ya timu hiyo kwa kila mchezaji kuanza kujitengenezea ufalme mbele ya kocha huyo akitarajiwa kutoa dira mbele ya wachezaji wa mabingwa hao wa Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho na Ngao ya Jamii.

Mastaa waliokuwa wanapata nafasi mbele ya kocha aliyeondoka, Miguel Gamondi na wale ambao walikuwa wanakaa benchi watakuwa na vita mpya mbele ya Ramovic ambaye ameshawaambia mabosi wa klabu hiyo kwamba hajawahi kuishia kwa kukariri katika kupanga kikosi chake.

Ramovic anajipanga kuhakikisha mchezaji mwenye kipaji na anayejituma kuanzia mazoezini hadi katika mechi sambamba na nidhamu yake ndiye atakayekuwa kupata nafasi ya kuiwakilisha timu yake.

“Ukikaa naye na ukazungumza naye utatamni kuona anaanza kazi haraka, hebu fikiria kuanzia jana (juzi) Jumamosi, anapiga simu hata usiku mkubwa akitaka kujua kitu wakati wote akiwa anaangalia mechi mbalimbali za timu,” alisema bosi mmoja wa juu wa Yanga.

“Kuna taarifa nyingi ambazo ameshaziomba mpaka sasa ambazo kwetu zimetushtua zikiwemo taarifa za wachezaji, ratiba ya mechi za mashindano na mambo mengine ya ndani ya klabu.

Wachezaji wa Yanga walikuwa katika mapumziko ya siku mbili baada ya ratiba ya siku tano zilizopita chini ya Gamondi ambaye walifanya naye kazi hadi Alhamisi wiki iliyopita kisha usiku wake akaitwa na kusitishiwa mkataba na klabu hiyo akiwa ameiacha timu katika nafasi ya pili katika Ligi Kuu na ikitinga makundi ya CAF.

Wachezaji kama Aboutwalib Mshery, Khomein Abubakar, Denis Nkane, Duke Abuya, Jonas Mkude, Kibwana Shomari, Jean Baleke, Bakar Mwamnyeto, Aziz Andambwile, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Farid Mussa watakuwa na mwanzo mpya wa kupigania mabadiliko ya nafasi mbele ya Ramovic.

Lakini hata wale waliookuwa na uhakika wa kikosi cha kwanza kwa sasa ni lazina nao wajipange kwani inategemea na mafaili yaop yatakavyosomeka na kumridhisgha Ramovic kabla ya kuanza kutengeneza kikosi kipya cha kumbeba katika michuano ya Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho na ile ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Yanga inacheza makundi ya michuano hiyo kwa msimu wa pili mfululizo ikiwa ni rekodi kazi ikifanywa na Gamondi, baada ya klabu hiyo kusota kwa miaka 25 tangu iliposhiriki mata ya kwanza 1998 mfumo wa michuano hiyo iliyokuwa ikifahamika kama Klabu Bingwa Afrika kubadilishwa.

Mastaa waliokuwa na uhakika katika kikosi cha kwanza kama watafabnya uzembe huenda wakapishana na wenzao waliokuwa wakisota mbele ya Gamondi, ni kama ilivyokuwa kwa wale waliotamba mbele ya Nasreddine Nabi kisha kujikuta na wakati mgumu chini ya Muargentina aliyetemeshwa kibarua.

Ramovic mara baada ya kutambulishwa Ijumaa asubuhi hakutaka kusubiri kitu, haraka akafanya vikao tofauti na mabosi wa timu hiyo akitaka kujua mambo mbalimbali ya timu yake.

Kocha huyo Mjerumani aliibuka makao makuu ya klabu hiyo zilizopo ofisi za viongozi kisha kufanya kikao na Afisa Mtendaji Mkuu Andre Mtine kisha akajifungia na meneja wa timu hiyo Walter Harrison akitaka kupata taarifa mbalimbali za timu hiyo.

Baada ya kikao hicho akaondoka huku akisema atatoa ratiba kamili ya namna atakavyoanza kazi huku Mwanaspoti linafahamu jana Jumapili kocha huyo alikuwa anatazama mechi mbalimbali za kikosi chake za ligi na hasa zile ambazo Yanga alipoteza dhidi ya Azam FC na hata Tabora United.

Ramovic atakuwa na siku nane ngumu ndani ya Yanga akitakiwa kubadilisha saikoloji ya wachezaji wake haraka warudi kwenye ushindani na kutafuta ushindi kabla haijarudi kucheza mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa hatua ya makundi nyumbani dhidi ya Al Hilal ya Sudan.

Ushindi wa Yanga kwenye mchezo huo utarudisha utulivu mkubwa ndani ya timu hito kuanzia kwa viongozi wake, benchi lake la ufundi na hata kwa wachezaji wake ambao wanatoka kupoteza mechi mbili mfululizo.

Ramovic benchi lake litakuwa na mtu mpya mmoja pekee ambaye ni raia wa kigeni kutoka Afrika Kusini anayekuwa kocha msaidizi bila uraia wake kufahamika akiwa tayari ameshawasili nchini akisubiri kutambulishwa tu.

Kocha huyo amewabakisha makocha wengine wote waliokuwa wasaidizi kwa Gamondi akiwemo kocha wa viungo Taibi Lagrouni, kocha wa makipa Alaa Meskini, mchambuzi wa mikanda ya video, Mpho Maruping.

Aliyekuwa kocha wa KMC, Abdihamid Moalin aliyetua Yanga hivi karibuni amepanda cheo akiwa Mkurugenzi wa ufundi nafasi ambayo ni mpya ndani ya timu hiyo.

Mtu wa mwisho kushika nafasi hiyo ndani ya Yanga alikuwa Kocha Mdachi Hans van Pluijm wakati timu hiyo kocha mkuu akiwa Mzambia George Lwandamina wakati huo timu hiyo ikiwa chini ya Bilionea marehemu Yusuf Manji.

Akizungumzia mabadiliko hayo Senzo Mazingiza ambaye ni mbobezi wa mambo ya utawala alisema anaamini kocha huyo atarudisha morali mpya mbele ya wachezaji wake na hata mashabiki ambao watatamani kujua kitu gani bora atakirudisha kwenye kikosi chao.

Senzo, aliyewahi kuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Yanga, alisema hana wasiwasi na ubora wa kocha huyo lakini anajua ni msimamizi mzuri wa nidhamu kwenye timu yoyote anayofundisha.

“Sijajua sababu za Yanga kufanya mabadiliko lakini naamini kuna sababu za msingi sana ambazo viongozi wa timu yetu zimewasukuma kuchukua maamuzi hayo, nawajua viongozi wote wa klabu ni watu wanaotaka mafanikio,” alisema Senzo na kuongeza;

“Kwangu mimi Ramovic ni kocha mzuri sana sijali kutoka kwake timu ndogo hapa, lakini falsafa zaje naamini zitaisaidia timu lakini huyu ni mtu anayetaka nidhamu iwe juu wakati wote sehemu ambayo anafanya kazi.

“Ujio wake tayari timu imetoka kupoteza mechi mbili lakini kwa wachezaji watarudisha morali kubwa ili wapambane kupata nafasi, nadhani hapo ndipo kutamsaidia,hata mashabiki nao watakuja kwa wingi wakitamani kuona kocha mpya ataanza vipi,ninaamini kwamba maisha mazuri yataendelea ndani ya Yanga.”

Related Posts