Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imeonya watu kuchangisha michango nje ya utaratibu ikisema michango yote ya waathirika wa ajali ya ghorofa lililoporomoka Kariakoo itakusanywa kupitia akaunti maalumu ya maafa.
Ghorofa hilo liliporomoka juzi Jumamosi ya Novemba 16, 2024 hadi kufikia jana saa 4:00 asubuhi, vifo vilikuwa vimefikia 13 na majeruhi 84.
Shughuli ya uokoaji inaendelea ikifanywa na vyombo vya dola kwa kushirikiana na wananchi.
Leo Jumatatu, Novemba 18, 2024, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Jim Yonazi amezungumza na waandishi wa habari akiwa eneo hilo la uokozi akitaka watu kutochangisha michango nje ya utaratibu.
“Tujizuie kukusanya michango kwa mtu yeyote bila kupitia mfuko wa maafa ambako michango inakusanywa ili kutoa misaada kwa walengwa,” amesema Yonazi.
Amesema kutoa misaada ya kifedha ni jambo ambalo lipo kisheria hivyo linapaswa kuratibiwa vema.
“Wote wanaopenda kuchangia, pesa zielekezwe katika akaunti maalumu ya maafa ambayo ipo Benki Kuu ya Tanzania na inaratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu,” amesema na kuitaja ni 9921159801.
“Hii ndio akaunti pekee nchini inakusanya misaada ya kifedha,” amesisitiza.
Akizungumzia shughuli za uokozi, amesema inaendelea, “hatutaacha hadi kwa yule mtu wa mwisho.”
Msingi wa onyo hilo ni kutokana na baadhi ya watu kuanza kuchangisha fedha ili kuwasaidia waathirika wa tukio hilo ambalo mbali na kusababisha vifo na mejeruhi, watu wamepoteza mali mbalimbali.
Jana Jumapili, Rais Samia Suluhu Hassan akitoa taarifa ya jengo hilo alisema sababu za kitaalamu za jengo kuporokoka hazijachunguzwa na kubainishwa na kipaumbele chetu ni kufanya uokozi.
Aidha, Rais Samia alisema,“Serikali itabeba gharama zote za waliojeruhiwa na kuhakikisha waliopoteza maisha wanastiliwa ipasavyo, nitoe pole kwa ndugu, jamaa na marafii.”