Mafaza Pamba wampiga tafu Modest

WACHEZAJI wa zamani na mashabiki wa Pamba, wameguswa na tukio la beki wa zamani wa kimtaifa wa Tanzania aliyewahi kukipiga katika timu hiyo, Simba, Yanga, Mtibwa Sugar na Taifa Stars, Alphonce Modest anayeugua kwa muda wa miaka mitano kwa kumchangia kiasi cha Sh 1 Milioni.

Modest hajiwezi kwa lolote, kiungo kinachofanya kazi katika mwili ni kichwa pekee ambapo hawezi kujigeuza kushoto wala kulia, amesumbuliwa na maradhi kwa zaidi ya miaka 14, hivyo anawategemea ndugu zake kufanya kila kitu.

Mwanaspoti lililofunga safari kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma lilifichua mateso anayopitia Modest, jambo lililowagusa wachezaji hao wa zamani pamoja na wadau wa timu hiyo kuanza kumchangia, huku wakihamasisha wengine kumpa msaada wa haraka, ili aweze kutibiwa.

Mchezaji wa zamani wa timu hiyo, Fumo Felician alisema wana kikundi cha umoja kilicho na zaidi ya watu 300 (group la WhatsApp), kila mmoja alichanga alichonacho ili kuwasaidia wenzao wanaosumbuliwa na maradhi.

“Kwa pamoja kama wachezaji wa zamani, wadau wa zamani wa Pamba kutoka mikoa mbalimbali, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, Mkurugenzi wa Jiji hilo, Mjumbe wa Bodi ya Pamba, wote kwa ujumla tukachangishana ili kuwashika mkono wenzetu,” alisema Fumo aliyewahi kukipiga pia Yanga aliyeongeza;

“Wenzetu wawili wamepata changamoto wote ni wachezaji wa zamani wa Pamba kuna Modest na David Mwakalebela ambaye alipata kiharusi, ingawa kwa sasa ameanza kuimarika, kila mmoja tumempa Sh. 1 milioni.”

Alisema mwenzao James Washokera aliyekuwa mchezaji wa zamani wa timu hiyo na sasa ni mchungaji, alisafiri kutoka Mwanza hadi Kigoma kwenda kumpa faraja Modest ambapo alikaa naye siku tatu.

“Tunamshukuru Wahokera nje na kutoa pesa aliamua kutoa muda wake, maana alicheza na Modest Pamba, hivyo alikaa naye siku tatu, mgonjwa akafarijika kwani tulikuwa tunampigia simu na kuzungumza naye,” alisema.

Wachezaji wengine wa zamani wa timu hiyo, ambao walisimamia michango hiyo ni Mao Mkami (baba yake na Himid Mao), Bitta John na Benjamin Magadula. Ukiachana na hao kuna mchungaji ambaye alitoa Sh100,000, kisha akamfanyia maombi na akaahidi akipata chochote atakuwa anamsaidia.

Baba wa staa huyo, Modest Alphonce Sr aliwashukuru wachezaji wenzake kwa kujitolea kwa ajili ya kumsaidia mwanaye.

“Mungu awabariki, nakosa meneno ya kusema, walichotupa kitatusaidia kwa sehemu, pia nalishukuru sana Mwanaspoti kwa kuja nyumbani na kuiona hali ya mwanangu kisha kuwatarifu Watanzania.”

Modest bado anahitaji msaada na yeyote atakayeguswa na hilo, atume kwa lipa namba 36526628 linatoka jina la mdogo wake Augostino Modest.

Related Posts