Mkufunzi wa kimataifa wa marefa wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (Fifa), Janny Sikazwe amesema anaamini marefa wa Tanzania watapata fursa ya kuchezesha fainali za mataifa ya Afrika (Afcon) 2025 huko Morocco.
Akizungumza wakati wa ufungaji wa mafunzo ya siku tano ya matumizi ya teknolojia ya video ya usaidizi kwa marefa (VAR) iliyoratibiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Sikazwe alisema kesho ya waamuzi wa Tanzania ni nzuri.
“Mtengeneze fursa kwa hawa watu ukizingatia wengi wanaonyesha kesho yao ni nzuri na ni vijana na katika urefa hii (VAR) ni njia mpya ya kuamua. Hivyo naiomba ofisi yako mwenyekiti uwape fursa. Tunataka kuona mtu kutoka Tanzania anaenda na kuwakilisha Tanzania.
“Kwa sasa natengeneza timu na ninasema nina watu najua kwamba Tanzania namfikiria refa huyu, huyu na yule. Naipongeza ofisi yako, tutaendelea kufanya kazi pamoja na kuona ni kwa namna gani tunaweza kuinyanyua Tanzania kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
“Jambo la msingi wanatakiwa kwenda kufanyia kazi kile ambacho wamejifunza kwa sababu kama wasipoanya hivyo watarudi katika sifuri,” alisema Sikazwe.
Mwenyekiti wa kamati ya waamuzi ya TFF, Nassor Hamduni aliwataka marefa hao kuhakikisha kile walichojifunza katika mafunzo hayo wanakwenda kukifanyia kazi kwa vitendo.
“Jamani washiriki wote ambao tumepata kozi hii, tafadhalini sana itakuwa ni aibu sana kwa mwamuzi yeyote atakayetoka humu kwenda kutufanyia ndivyo sivyo katika michezo yetu.
“Sisi kama kamati ya waamuzi tunawapongeza kwa ushiriki wenu na tunawapongeza walimu wa ndani kwa kazi kubwa wanayofanya,” alisema Hamduni.