Mchungaji akutwa amefariki na majeraha usoni, mwingine aopolewa

Morogoro. Aron Daniel (16), mkazi wa mtaa wa Msimamo, Kata ya Kihonda, Manispaa ya Morogoro amekutwa amefariki dunia katika eneo la ‘Youth Mission’ huku mwili wake ukiwa na majeraha usoni.

Baba mdogo wa marehemu, Baraka Kamele, amesema Aron alikuwa akijihusisha na uchungaji wa mbuzi, ambapo Novemba 16, aliondoka na wanyama hao kwenda machungani, lakini  jioni mbuzi hao walirudi nyumbani wenyewe bila mchungaji.

Ameongeza kuwa familia ilianza kumtafuta siku mbili zilizopita na hatimaye jana Novemba 17, mwili wake ulipatikana baada ya kupokea taarifa kutoka kwa wakazi wa eneo hilo.

“Baada ya kupata taarifa, tulikwenda eneo la tukio na kuthibitisha kuwa ni Aron ni jambo  la kusikitisha kwa sababu bado alikua kijana mdogo na hakuwa na tatizo na mtu,” amesema Kamele.

Baadhi ya wananchi waliokusanyika eneo hilo waliiomba Serikali kuchukua hatua madhubuti kudhibiti matukio ya vifo ambayo yamekuwa yakitokea mara kwa mara katika eneo hilo.

Mmoja wa wananchi ya aliyejitambulisha Kwa jina moja la Emanuel amesema vitendo hivyo vya mauaji wanavihusisha na uporaji, huku wakiiomba Serikali  kuweka mikakati thabiti vitendo vya kihalifu kama uporaji.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama, ameithibitisha Mwananchi kutokea kwa tukio hilo, huku akieleza kuwa uchunguzi wa awali unaonyesha marehemu huenda amefariki kutokana na maradhi ya kawaida.

“Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa kina kubaini chanzo halisi cha kifo cha kijana huyo,” amesema Kamanda Mkama.

Wananchi wa mtaa wa Youth Misheni kata ya Kihonda Manispa ya Morogoro wakiwa wamebeba mwili kijana, Aron Daniel (16) uliokutwa vichakani huku ukiwa na majeraha usoni. Picha Happiness Mremi

Aidha katika tukio lingine mwili wa kijana aliyefahamika kwa jina moja la Matabuki mkazi wa Mvalanyaki kata ya Tungi Manispaa ya Morogoro anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 27-28 umeopolewa na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani humo, baada ya kuzama katika bwawa alipokua akivua samaki.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo mrakibu msaidizi wa jeshi hilo,  Daniel Miyala amesema kuwa walifika katika eneo hilo baada ya kupokea simu kupitia namba ya dharura 114 kutoka kwa wananchi.

“Tulifika katika eneo la tukio na kukuta wananchi wakishirikiana na viongozi wa serikali za mtaa wakiwa wanaendelea na zoezi la kuutafuta mwili,” amesema Miyala.

Aidha ameeleza kuwa baada ya kufika hapo jeshi hilo lilianza shughuli ya kuutafuta mwili mara moja ambapo saa nane mchana walifanikiwa kuupata.

“Tunatoa rai kwa wananchi wa Kata ya Tungi kuacha shughuli wanazofanya pembezoni mwa bwawa hilo, kwani tukio hili sio la kwanza kutokea,” ameeleza Miyala

Miyala ameeleza kuwa chanzo cha tukio hilo ni kijana huyo kuteleza wakati akivua samaki na kutumbukia katika bwawa hilo.

Related Posts